MO Salah amwaga machozi akibeba Misri
Muktasari:
- Timu hiyo kutoka Afrika Kaskazini iliibuka na ushindi dhidi ya Australia kupitia mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi iliyochezwa jijini Dallas.
DALLAS, Marekani: MSHAMBULIAJI Mohamed Salah alishindwa kuzuia hisia zake za kutokwa na machozi baada ya kuiongoza Misri kupata ushindi wake wa kwanza kabisa katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia.
Timu hiyo kutoka Afrika Kaskazini iliibuka na ushindi dhidi ya Australia kupitia mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi iliyochezwa jijini Dallas.
Ulikuwa usiku wa kihistoria kwa Misri, ambayo ilipata ushindi wake wa kwanza kabisa katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia na pia kufuzu hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1934.
Salah, mwenye umri wa miaka 34, alikuwa mmoja wa nyota waliotoa mchango mkubwa katika ushindi huo baada ya kufunga moja ya penalti za Misri.
Nahodha huyo wa Liverpool alionyesha utulivu mkubwa kwa kufunga penalti yake kwa mtindo wa Panenka, akimpiga kipa wa akiba wa Australia, Maty Ryan.
Misri ilifunga penalti zake zote nne, huku Australia ikiangushwa na makosa ya Harry Souttar na kijana Lucas Herrington, ambao walikosa mikwaju yao.
Baada ya ushindi huo, Salah alionekana akitokwa na machozi alipokuwa akizungumza katika mahojiano hayo, aliulizwa kuhusu kukutana na Lionel Messi katika hatua ya 16 bora.
Mabingwa watetezi Argentina ilibidi kusubiri hadi dakika 120 kabla ya kupata ushindi wake muhimu wa mabao 3-2 dhidi ya Cape Verde.
Kabla ya mikwaju ya penalti kuanza, Salah alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Misri waliokuwa wakitazama video za matukio muhimu ya kipa Maty Ryan kupitia kompyuta mpakato ili kujifunza namna ya kumfunga.
Alifichua pia kuwa alibadilisha uamuzi wake katika dakika za mwisho na kuamua kupiga penalti kwa mtindo wa Panenka.
Alisema:"Kama kulikuwa na mtu wa kufanya hivyo, basi ilikuwa ni mimi.
Nina uzoefu zaidi kuliko wengine na nilitaka kuwapa wenzangu kujiamini. Niliamua katika dakika za mwisho kwamba nilipaswa kufanya hivyo."