Mmesikia!? Bruno yupo tayari kuondoka Manchester United
Muktasari:
- Bruno ambaye anapokea mshahara wa Pauni 240,000 kwa wiki akiwa na Man United, mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni mwaka 2027.
KIUNGO mshambuliaji wa Manchester United, Bruno Fernandes, 30, ambaye amekataa ofa tatu kutoka kwa timu za Saudi Arabia zilizohitaji kumsajili kaitka dirisha lililopita la majira ya kiangazi anadaiwa kuwaambia wawakilishi wake kwamba atakuwa tayari kuondoka katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani.
Bruno ambaye anapokea mshahara wa Pauni 240,000 kwa wiki akiwa na Man United, mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni mwaka 2027.
Tangu ajiunge na Man United mwaka 2020 akitokea Sporting Lisbon, amekuwa mhimili wa timu kwa akifunga mabao 99 na kutoa asisti 86 katika mechi 294 za michuano yote.
Timu za Saudi zimekuwa zikipambana kutaka kumsajili staa huyu kwa muda mrefu sasa lakini zimekuwa zikigonga mwamba kwa sababu Bruno mwenyewe hayupo tayari kuachana na mashetani wekundu kwa sasa.
Timu hizo ziliweka mezani ofa ya ada ya uhamisho inayofikia Pauni 80 milioni, pia mshahara wa zaidi ya Pauni 700,000 kwa wiki ili kumshawishi Bruno.
Cody Gakpo
BAYERN Munich ilikuwa inafikiria kumsajili winga wa Liverpool, Cody Gakpo, 26, katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kabla ya kuhamia kwa Luis Diaz.
Inaelezwa dili la Gakpo lilishindikana kutokana na ada kubwa ya uhamisho, pia mchezaji mwenyewe hakuwa tayari kuondoka Liverpool. Gakpo ambaye lijiunga na Liverpool Januari 2023 kwa ada ya takribani Pauni 44 milioni, mkataba wake unaisha 2030.
Andrey Santos
CHELSEA imepokea ofa ya Pauni 59.5 milioni kutoka klabu ya Al-Qadsiah ya Saudi Arabia kwa ajili ya staa wao kiungo, Andrey Santos, 21. Santos ambaye ni raia wa Brazil, alisajiliwa na Chelsea Januari 2023 kutoka Vasco da Gama kwa takribani Pauni 18 milioni na msimu uliopita alikuwa kwa mkopo Strasbourg ya Ufaransa. Chelsea bado haijafikia uamuzi na inaendelea kufanya majadiliano na wawakilishi wa mchezaji ila bado inamhitaji sana.
Morgan Rogers
TOTTENHAM Hotspur inamnyemelea kiungo wa Aston Villa, Morgan Rogers, 23, kuelekea dirisha dogo la Januari. Kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank, ameripotiwa kumpendekeza mchezaji huyo anayeichezea timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23. Rogers alijiunga na Villa Januari 2024 akitokea Middlesbrough kwa dau la Pauni 15 milioni.
Zain Silcott-Duberry
BOURNEMOUTH ipo katika mazungumzo ya hatua za mwisho na klabu ya Olympiakos ya Ugiriki ili kumruhusu mshambuliaji wao raia wa England, Zain Silcott-Duberry, 20, kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Ugiriki. Silcott-Duberry alikuwa akicheza katika akademi ya Arsenal kabla ya kujiunga na Bournemouth licha ya kupandishwa timu ya wakubwa hadi sasa bado hajapata nafasi EPL.
Dani Ceballos
JUVENTUS bado haijakata tamaa na inataka kufanya usajili wa staa wa Real Madrid, Dani Ceballos, 29, katika dirisha lijalo la majira ya baridi. Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania alihusishwa na Juventus katika dirisha lililopita lakini dili likakwama katika dakika za mwisho.
Ceballos ambaye alijiunga Real Madrid 2017 akitokea Real Betis kwa ada ya Euro 16.5 milioni anatamani sana kuondoka kwa sababu hapati nafasi kikosini.
Giovanni Leoni
LICHA ya kuwekewa dau nono na Newcastle, beki chipukizi wa kimataifa wa Italia, Giovanni Leoni, 18, alikataa dili la kujiunga na timu hiyo na badala yake akachagua kutua Liverpool. Newcastle inaripotiwa kuwa ilikuwa tayari kulipa Euro 40 milioni wakati Liverpool ikikamilisha usajili wake kwa Euro 31 milioni. Mkataba wa beki huyu wa taifa vijana Italia U19, unaisha 2031.