Mkataba mpya wa Ronaldo ni kufuru

Muktasari:
- Gwiji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40, amepata dili la kuongeza mshahara wake kwenye klabu ya Al-Nassr, ambako atacheza hadi akiwa na umri wa miaka 42 huku mshahara wake ukiwa ni Pauni 488,000 kwa siku.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amesaini dili la pesa nyingi likiweka historia katika michezo na mkali huyo atakwenda kuvuna Pauni 492 milioni kwa kipindi cha miaka miwili.
Gwiji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40, amepata dili la kuongeza mshahara wake kwenye klabu ya Al-Nassr, ambako atacheza hadi akiwa na umri wa miaka 42 huku mshahara wake ukiwa ni Pauni 488,000 kwa siku.
Ripoti zinafichua staa huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na Juventus amepewa ofa ya kuwa balozi wa klabu hiyo, jambo litakalomwongezea kipato chake kwa zaidi ya nusu bilioni kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.
Juu ya mshahara wake wa Pauni 178 milioni kwa mwaka, Ronaldo analipwa Pauni 24.5 milioni kama bonasi ya kukubali kusaini dili jipya - ambayo itaongezeka hadi Pauni 38 milioni katika mwaka wake wa pili wa mkataba huo.
Taarifa ya ndani kutoka Saudi Pro League inafichua Ronaldo pia atapewa asilimia 15 ya hisa za klabu hiyo, ambazo zina thamani ya Pauni 33 milioni. Na bonasi ya Pauni 4 milioni endapo kama ataibuka mfungaji bora na Pauni 8 milioni kama Al-Nassr itanyakua ubingwa, hivyo atakuwa na uwezo wa kuvuna zaidi ya Pauni nusu bilioni kabla ya dili lake kufika ukingoni.
Ronaldo na familia yake pia itakuwa ikiishi vyema kwa mambo ya nje ya uwanja. Atakuwa na wafanyakazi 16, madereva watatu, wasaidizi wa nyumbani wanne, wapishi wawili, watunza bustani watatu na wawili wanne. Hao wote watalipwa na Al-Nassr, karibu Pauni 1.4 milioni.
Kutakuwa na Pauni 4 milioni pia ambazo atatumia kwenye ndege binafsi, huku pia akiahidiwa dili za udhamini wa kibiashara kwa kampuni za Saudi Arabia, ambazo zinaweza kumwingizia hadi Pauni 60 milioni.
Ripoti zinadai mabosi wa ligi walikuwa na wasiwasi wa Ronaldo kuondoka, hasa katika kipindi hiki cha dirisha la usajili likiwa wazi na kuna fainali za Kombe la Dunia la Klabu.
Lakini, sasa amesaini dili jipya na anafurahia jambo hilo.
MKATABA MPYA WA RONALDO
-Pauni 178milioni- kwa mwaka
-Pauni 3.4milioni - kwa wiki
-15% umiliki wa hisa Al-Nassr (Pauni 33milioni)
-Pauni 24.5milioni - bonasi ya kusajili
-Pauni 80,000 - bonasi ya kila bao
-Pauni 40,000- bonais ya kila asisti
-Pauni 8milioni - Al-Nassr ikibeba ubingwa
-Pauni 4milioni - akibuka mfungaji bora
-Pauni 6.5milioni- Al-Nassr ikifuzu Mabingwa Asia na kushinda
-Wafanyakazi 16 - muda wote
-Pauni 4milioni - gharama ya ndege binafsi
-Pauni 60milioni - dili za udhamini wa kibiashara