Cristian Romero ‘amchunia’ Trump
Muktasari:
- Argentina ilimaliza kama mshindi wa pili baada ya kufungwa 1-0 na Hispania katika muda wa nyongeza, huku bao la Ferran Torres dakika ya 106 likiipa Hispania ubingwa.
LOS ANGELES, MAREKANI: BEKI wa Argentina na Tottenham, Cristian Romero, amezua gumzo baada ya kuonekana kumpuuza Rais wa Marekani, Donald Trump, wakati wa hafla ya kukabidhi medali kufuatia fainali ya Kombe la Dunia.
Argentina ilimaliza kama mshindi wa pili baada ya kufungwa 1-0 na Hispania katika muda wa nyongeza, huku bao la Ferran Torres dakika ya 106 likiipa Hispania ubingwa.
Baada ya filimbi ya mwisho, Trump akiwa sambamba na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, walikuwa jukwaani kukabidhi medali na tuzo mbalimbali kwa waamuzi na wachezaji.
Romero alipokea medali yake kutoka kwa Infantino, lakini alipofika mbele ya Trump hakumsalimia kwa kumpa mkono. Badala yake alipita moja kwa moja na kwenda kuungana na wenzake, tukio lililonaswa na kamera na kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki, wengi wakilitafsiri kama ishara ya kumkataa au kumpuuza rais huyo wa Marekani.
Baadaye, wakati wa kukabidhi kombe kwa nahodha wa Hispania, Rodri, Trump naye aliibua gumzo baada ya kubaki jukwaani wakati wachezaji wa Hispania wakisherehekea kunyanyua kombe.
Inaelezwa kuwa Infantino alionekana kumwashiria Trump aondoke ili kuwaachia mabingwa nafasi yao ya kusherehekea, lakini Rais huyo aliendelea kusimama pembeni ya kikosi cha Hispania huku akipiga makofi na kutabasamu wakati fataki na makaratasi ya shangwe yakirushwa uwanjani.
Mashabiki waliokuwepo uwanjani walisikika wakizomea wakati Trump na Infantino walipoingia uwanjani kwa ajili ya hafla ya kukabidhi tuzo.
Ndani ya uwanja, Hispania ilionekana kutawala mchezo kwa sehemu kubwa, huku Argentina ikicheza kwa ukali na kufanya makosa 24. Enzo Fernández alitolewa kwa kadi nyekundu mwishoni mwa muda wa kawaida.
Baada ya filimbi ya mwisho, hali ilichafuka uwanjani. Wachezaji na benchi la Hispania walikimbilia kusherehekea ushindi wao, jambo lililosababisha mzozo kati ya pande hizo.
Kiungo wa Argentina, Leandro Paredes, alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga Eric Garcia na baadaye kumsukuma Gavi. Naye Nahuel Molina aliripotiwa kumpiga Rodri tumboni wakati wa vurugu hizo, huku Thiago Almada pia akihusishwa katika sintofahamu hiyo.