Mido awacharukia Misri kisa Salah
Muktasari:
- Kipa Shobeir alishindwa kuudhibiti mpira, hali iliyomruhusu mshambuliaji wa Afrika Kusini, Puso Dithejane, kuunasa kisha alimpita beki wa Misri, Hossam Abdel-Meguid, kabla ya kutumbukiza mpira wavuni lililokuwa wazi na kuipa Afrika Kusini ushindi.
CAIRO, MISRI: ALIYEKUWA mshambuliaji wa timu ya taifa ya Misri na Tottenham Hotspur, Mido, ameikosoa Shirikisho la Soka la Misri (EFA) kwa kumruhusu Mohamed Salah kuondoka kambini kabla ya mchezo dhidi ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana'.
Katika mchezo huo wa kirafiki wenyeji Misri walikubali kipigo cha bao 1-0 kutokana na kosa la kipa Mostafa Shobeir liliigharimu timu yake kwenye Uwanja wa Cairo.
Kipa Shobeir alishindwa kuudhibiti mpira, hali iliyomruhusu mshambuliaji wa Afrika Kusini, Puso Dithejane, kuunasa kisha alimpita beki wa Misri, Hossam Abdel-Meguid, kabla ya kutumbukiza mpira wavuni lililokuwa wazi na kuipa Afrika Kusini ushindi.
Kabla ya mchezo huo nyota Salah aliyecheza katika mchezo wa Misri dhidi ya Angola uliomalizika kwa suluhu, lakini hakucheza katika mchezo dhidi ya Sudan Kusini baada ya kuachwa nje ya kikosi kutokana na hali ya uwanja.
Mbali na Salah, beki Mohamed Abdelmonem pia ameondoka kwenye kambi ya timu hiyo baada ya makubaliano kufikiwa kati ya EFA na klabu yake ya OGC Nice ya Ufaransa.
Hatua hiyo haijamfurahisha Mido, ambaye amehoji namna Shirikisho la Soka la Misri lilivyoshughulikia suala hilo, hasa kwa kuhusisha hali ya Abdelmonem na namna suala la Salah lilivyoshughulikiwa.
“Mohamed Abdelmonem ndiye beki bora zaidi wa Misri kwa sasa anayocheza katika ligi yenye ushindani mkubwa ya Ligue 1. Lazima kuwe na ufafanuzi kuhusu hali yake iwapo ameondolewa,” Mido aliandika kwenye mtandao wa X.
Akaongeza: “Kwa nini hakuchukua hatua hiyo hiyo kwa Salah, ikiwa sababu ni kukataa kwake na kwa klabu yake kucheza kwenye uwanja wa nyasi bandia?”
Mido pia ameibua swali kuhusu uhusiano kati ya kocha wa Misri, Hossam Hassan na baadhi ya wachezaji, akitaka kujua kama changamoto hizo zinatokana na kocha au wachezaji.
“Swali muhimu zaidi ni kama kuna tatizo kati ya kocha na idadi kubwa ya wachezaji, je, kocha ndiye chanzo au ni wachezaji? Je, tunawasaidia wachezaji wetu wanaocheza nje au tunawaua?” alihoji.
Katika mchezo huo ilishuhudia Misri ikishindwa kuvunja ngome ya Afrika Kusini iliyokuwa imejipanga vizuri.
Kocha wa Misri, Hossam Hassan, alimwingiza mshambuliaji wa NBE Club, Osama Faisal, mwanzoni mwa kipindi cha pili, akimtoa kiungo wa Al Ahly, Emam Ashour, katika jitihada za kuongeza presha.
Hata hivyo, dakika saba baada ya kuanza kipindi cha pili, Afrika Kusini ilitangulia baada ya Dithejane kutumia vyema kosa la Shobeir aliyekuwa ametoka langoni bila wakati sahihi.
Mshambuliaji huyo aliunasa mpira uliokuwa umeachwa, akampita Abdel-Meguid na kuufunga kwenye lango lililokuwa wazi.
Hassan alifanya mabadiliko mengine mawili dakika ya 69, akiwaingiza Ahmed “Zizo” Sayed na Hamza Abdelkarim kuchukua nafasi za Omar Marmoush na Marwan Attia, akilenga kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
Dakika ya 77, El-Mahdi Soliman aliingia kuchukua nafasi ya Shobeir, huku kipa huyo wa Zamalek akifanya mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 39.
Dakika mbili baadaye, Abdelkarim alikaribia kuisawazishia Misri baada ya kichwa chake akiwa ndani ya eneo la hatari kuokolewa na kipa wa Afrika Kusini.
Misri iliendelea kusaka bao la kusawazisha katika dakika za mwisho, lakini shuti la Ibrahim Adel akiwa ndani ya eneo la hatari liligonga mwamba, huku Afrika Kusini ikidhibiti ushindi huo hadi filimbi ya mwisho.