Singida Black Stars yaipania Dodoma Jiji
Muktasari:
- Timu hiyo iliyoweka kambi Arusha ya wiki mbili, imecheza mechi mbili za kirafiki, ikianza kwa kuichapa Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara bao 1-0, Oktoba 1, 2026, kisha ikaichapa Mbuni FC ya Championship mabao 2-1, Oktoba 3, 2026.
KIKOSI cha Singida Black Stars kimeendelea na maandalizi yake jijini, Arusha kwa ajili ya kujiandaa na mechi kali na ya kuvutia dhidi ya Dodoma Jiji ‘Walima Zabibu’, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Oktoba 9, 2026.
Timu hiyo iliyoweka kambi Arusha ya wiki mbili, imecheza mechi mbili za kirafiki, ikianza kwa kuichapa Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara bao 1-0, Oktoba 1, 2026, kisha ikaichapa Mbuni FC ya Championship mabao 2-1, Oktoba 3, 2026.
Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Mkongomani Papy Kimoto amesema ameridhika na maendeleo ya wachezaji wa kikosi hicho, licha ya baadhi yao kujiunga na timu za taifa katika kipindi hiki cha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
“Tumekuwa na maandalizi mazuri na yenye kuridhisha hapa jijini, Arusha, wachezaji wengi tulikuwa nao ukiachana na wale waliokuwa katika timu mbalimbali za taifa, jambo lililotusaidia kutengeneza muunganiko wa kiuchezaji,” amesema Kimoto.
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida, Hussein Massanza amesema tangu timu hiyo imeweka kambi jijini, Arusha kumekuwa na maendeleo mazuri ya mchezaji mmoja mmoja, kutokana na programu mbalimbali za Kocha Mkuu, Papy Kimoto.
Katika mechi sita ilizocheza hadi sasa Singida za Ligi Kuu, imeshinda tatu, ikitoka sare moja na kupoteza mbili, ikiwa nafasi ya nne na pointi zake 10, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.