Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtego wa namba, ubora utakavyoamua Ballon d’Or

Muktasari:

  • Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Oktoba 26, 2026 jijini London, Uingereza, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nje ya Ufaransa tangu zilipoanzishwa Desemba 18, 1956, zikilenga kutambua mchango wa wachezaji wa ligi za Ulaya, ingawa waandaaji, France Football, walibadilisha wigo na kuamua zianze kuwatambua mastaa kutoka sehemu mbalimbali duniani kuanzia 2007.

PARIS, UFARANSA: WAKATI tuzo za Ballon d’Or mwaka huu zikiendeleza mjadala mpana wa ni nani atayechukua kwa mara ya kwanza zinapofanyika nje ya Paris, Ufaransa, mastaa sita wameendelea kung’ang’ania katika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa wanaopewa nafasi kubwa ya kunyakua kutokana na kura ambazo zinaendelea kupigwa.

Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Oktoba 26, 2026 jijini London, Uingereza, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nje ya Ufaransa tangu zilipoanzishwa Desemba 18, 1956, zikilenga kutambua mchango wa wachezaji wa ligi za Ulaya, ingawa waandaaji, France Football, walibadilisha wigo na kuamua zianze kuwatambua mastaa kutoka sehemu mbalimbali duniani kuanzia 2007.

Na tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia 2026, kura zinazoendelea kupigwa zimeendelea kuvuta hisia za wadau wa soka, huku majina ya Harry Kane, Lamine Yamal, Rodri, Ousmane Dembele, Kylian Mbappe na Lionel Messi yakibadilishana katika nafasi za juu kila wiki, hivyo kuwapa nafasi zaidi ya moja wao kunyakua tuzo hiyo.

Wakati wiki hii inapomalizika leo, bado Yamal anaongoza kwa kura kwenye msimamo ikiwa ni wiki ya tatu mfululizo ingawa haina maana kwamba ndiye atakayechukua tuzo kwani kuna vigezo vingine ambavyo majaji huvizingatia na ndivyo vinavyobeba siri ya nyota anayebeba siku ya siku. Lakini, kwa kuzingatia mfululizo wa nyota hao watano kuwa juu ya msimamo dhidi ya wengine kwa muda mrefu sasa, endelea kujikumbusha namba zinazowatetea na kushawishi huenda mmojawao akabeba tuzo hiyo.


LAMINE YAMAL

“Ni kuhusu kuwa mtulivu. Ninapokuwa eneo la hatari na mpira mguuni, mimi ndiye ninaamua kitakachotokea,” alisema Lamine Yamal, Februari mwaka huu baada ya kufunga hat-trick yake ya kwanza katika ushindi wa Barcelona wa mabao 4-1 dhidi ya Villarreal kwenye Ligi Kuu Hispania.

Kwa vijana wengi wenye umri wa miaka 19 kauli kama hiyo ingeweza kuonekana kama majivuno, lakini Yamal si mchezaji wa kawaida mwenye umri huo. Alifanya yake tena kabla ya msimu uliopira alipokuwa mchezaji wa kwanza kucheza fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya na fainali ya Kombe la Dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka 20, na akashinda mashindano yote mawili.

Alifunga bao moja pekee katika Kombe la Dunia, kiwango ambacho kinaonekana kidogo ukilinganisha na viwango vyake vya juu, lakini mchango wake ulikuwa mkubwa katika mashindano yote.

Alisababisha penalti muhimu katika nusu fainali dhidi ya Ufaransa, huku akipiga chenga nyingi zilizofanikiwa kuliko Lionel Messi katika mashindano hayo, na alikuwa sehemu muhimu ya kuvunja ufalme wa Argentina ambayo ilijaribu kumvuta kwenye mipambano ya nguvu katika fainali.

Alifanya yote hayo akiwa amecheza mashindano akiwa na majeraha ya misuli ya paja na baada ya fainali, staa wa zamani wa Man City, Joe Hart, ambaye sasa ni mchambuzi wa soka alikaririwa akisema: “Lamine Yamal ana miaka 19. Ni siku nzuri sana kwake. Ana miaka 19 na amekamilisha soka.” Mbali na mafanikio ya timu ya taifa, Yamal pia alifunga mabao 24 na kutoa pasi za mabao 18 katika mechi 45 akiwa na Barcelona, wakati klabu hiyo ikitwaa La Liga na Supercopa. Ana nafasi kubwa ya kwenda hatua moja zaidi baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ballon d’Or mwaka jana.


HARRY KANE

Mabao 73 katika mechi 64 akiwa na klabu na timu ya taifa, ikiwa ni kiwango cha pili kwa ubora katika historia kwa mchezaji mmoja nyuma ya msimu wa Lionel Messi wa kufunga mabao 82 ule wa 2011/12. Siyo rekodi mbaya kwa mchezaji ambaye wakati fulani alikuwa akikaa benchi akiwa pamoja na Jamie Vardy kwenye Ligi Daraja la Championship.

Kane hakuwa kipaji cha mapema kama baadhi ya wachezaji wengine waliopo kwenye orodha hii, lakini akiwa na umri wa miaka 33 sasa amejiweka kwenye orodha ya mastaa wakubwa zaidi duniani.

Inaonekana kuwa jambo la kushangaza kwamba mchezaji aliyefunga angalau mabao 24 katika kila msimu kati ya 12 iliyopita, aliyeshinda tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu England mara mbili mfululizo, Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia na tuzo mbili za Kiatu cha Dhahabu Ulaya, hajawahi kumaliza zaidi ya nafasi ya 10 kwenye upigaji kura wa Ballon d’Or.

Takwimu zake zimekuwa zikijieleza kwa muda mrefu, lakini sasa ameanza kuongeza mataji kwenye historia yake. Ukame wake wa kutwaa vikombe uliisha baada ya Bayern Munich kushinda Bundesliga msimu uliopita, na ushindi huo umefungua milango ya mafanikio zaidi.

Msimu huu Bayern iliongeza taji jingine la Bundesliga, pamoja na Kombe la Ujerumani (DFB-Pokal) na Super Cup ya Ujerumani. Ingawa England haikufanikiwa kuvunja ukame wake wa mataji katika Kombe la Dunia, nahodha huyo alifunga mabao sita na kumpita Gary Lineker kuwa mfungaji bora wa England katika historia ya mashindano hayo, jambo lililomweka bado kwenye kinyang’anyiro cha Ballon d’Or.


LIONEL MESSI

Lionel Messi alikaa peke yake chini kwenye Uwanja New York New Jersey, Marekani wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 80,000, akiwa amevua viatu na akitazama mbali huku wachezaji wa akiba wa Hispania wakisherehekea ushindi wa ubingwa wa Kombe la Dunia 2026.

Haikuwa picha ya mwisho ambayo nahodha huyo wa Argentina alikuwa ameifikiria alipokuwa akiondoka kwenye jukwaa kubwa la soka duniani.

Kwa kuzingatia kiwango chake katika wiki sita zilizopita za mashindano, wengi walihisi alistahili zaidi hata kama timu yake haikufanikiwa.

Baadhi walitarajia Kombe la Dunia lingekuwa safari ya kumbukumbu kwa Messi, nyota ambaye huenda alishiriki mashindano yake ya mwisho kabla ya kutimiza umri wa miaka 40. Lakini, alianza kwa kufunga hat-trick katika mchezo wa kwanza wa Argentina, kisha alifunga mabao mawili dhidi ya Austria, halafu akaongeza lingine dhidi ya Jordan.

Aliiongoza Argentina hatua kwa hatua katika hatua za mtoano; bao dhidi ya Cape Verde, bao na asisti dhidi ya Misri, asisti dhidi ya Uswisi na pasi mbili za mabao katika ushindi dhidi ya England kwenye nusu fainali.

Kama siyo mabao mawili ya Mbappe kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu, huenda Messi angeondoka na Kiatu cha Dhahabu. Lakini, je, anaweza kushinda Ballon d’Or licha ya kupoteza fainali ya Kombe la Dunia?

Katika miaka 19 iliyopita, ni mara nne pekee tuzo hiyo imekwenda kwa mchezaji ambaye hakushinda Ligi ya Mabingwa, Kombe la Dunia, Euro au Copa America katika mwaka husika wa michuano.

Lakini, mara tatu kati ya hizo zilikuwa kwa Messi. Ballon d’Or ya tisa inaonekana kuwa ngumu, lakini ukweli kwamba bado anatajwa kwenye mjadala huu akiwa na miaka 39, akicheza Inter Miami ya Ligi Kuu Marekani (MLS) na baada ya kupoteza fainali, unaonyesha ukubwa wa kipaji na mafanikio yake.


RODRI

“Tutamuona Rodri halisi kwenye fainali za Kombe la Dunia,” alisema Pep Guardiola, kocha wa zamani wa Manchester City, mwezi Oktoba, mwaka jana baada ya nahodha huyo wa kikosi hicho kurejea uwanjani kufuatia majeraha makubwa ya goti. Kulikuwa na shaka kama mshindi huyo wa Ballon d’Or 2023 angeweza kurejea kwenye kiwango chake bora, lakini kama ilivyo mara nyingi kwenye soka, Guardiola alikuwa sahihi.

Rodri alikuwa moyo wa timu ya taifa ya Hispania na mchezaji aliyeihakikishia usalama eneo la kiungo. Alidhibiti kila hatua ya mchezo, akaongoza umiliki wa mpira na kuondoa karibu kila tishio lililoelekezwa kwenye lango lao. Hispania iliruhusu bao moja pekee katika mechi nane za mashindano hayo.

Rodri alikamilisha pasi 756, nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye mashindano hayo. Pia alikuwa kinara kwa kugusa mpira, pasi zilizovunja mistari ya wapinzani na zilizofika kwenye eneo la mwisho la wapinzani.

Katika fainali pekee alikamilisha pasi 101, akiinyima Argentina nafasi ya kucheza itakavyo hadi timu hiyo ikashindwa hata kupata shuti moja lililolenga lango. Aliinua kombe akiwa nahodha wa Hispania, akatwaa tuzo ya Golden Ball kama mchezaji bora wa mashindano na kuingia kwenye orodha maalumu ya wachezaji wachache waliowahi kushinda Kombe la Dunia, Euro, Kombe la Klabu Bingwa Ulaya na Ballon d’Or.

Ni mchezaji wa nne tu katika historia kufanya hivyo baada ya Gerd Muller, Franz Beckenbauer na Zinedine Zidane.


OUSMANE DEMBELE

Je, Ousmane Dembele atakuwa mchezaji wa kwanza kutetea tuzo ya Ballon d’Or tangu Lionel Messi alipofanya hivyo mwaka 2021?

Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa alikosa sehemu kubwa ya nusu ya kwanza ya msimu wa 2025/26 katika kikosi cha PSG kutokana na majeraha, lakini katika miezi ya karibuni amerejea kwenye kiwango chake bora kabisa.

Bao lake la mkwaju wa kuinua mpira (chip) dhidi ya Lille lilitajwa mapema kuwa miongoni mwa yale yanayogombea Tuzo ya Puskas 2026 ya bao bora la mwaka. Baadaye alifunga mabao mawili, likiwemo bao la kuvutia alilofunga kwa juhudi binafsi wakati PSG ilipoichapa Marseille kwa nyundo 5-0 mwezi Februari.

Kiwango hicho kilimrudisha kwenye nafasi za juu za wagombea wa Ballon d’Or, na nafasi yake ya kutwaa tuzo hiyo iliongezeka zaidi baada ya PSG kufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika kampeni hiyo, Dembele aliandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga angalau bao moja katika kila hatua ya mashindano hayo, kuanzia hatua za mwanzo hadi fainali. Hata hivyo, kushindwa kwa Ufaransa kuiondoa Hispania katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 kunaweza kuwa pigo kubwa kwa matumaini yake ya kushinda Ballon d’Or.

Ufaransa ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa dunia, lakini ilizidiwa ubora na Hispania na kuishia kutolewa. Licha ya hayo, Dembele alikuwa na mashindano mazuri akimaliza Kombe la Dunia akiwa amefunga mabao sita na kutoa pasi mbili za mabao.

Takwimu zake msimu wa 2025/26 zinaonyesha kuwa amecheza mechi 40 PSG akifunga mabao 20 na asisti 11, huku katika Kombe la Dunia 2026 akicheza mara nane akifuga mabao sita na asisti mbili, ilhali mataji aliyobeba ni lile la Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) na Ligi ya Mabingwa Ulaya.


KYLIAN MBAPPE

Kylian Mbappe alipambana bega kwa bega na aliyekuwa staa mwenzake Paris Saint-Germain (PSG), Lionel Messi, katika Kombe la Dunia.

Nyota hao waligombea taji la dunia, Kiatu cha Dhahabu, Golden Ball na nafasi kwenye historia ya mashindano hayo. Mbappe alishinda mawili kati ya hayo manne. Mabao yake mawili katika mchezo wa kutafuta nafasi ya tatu dhidi ya England yalimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia mara mbili.

Pia alifikisha mabao 22 katika historia ya Kombe la Dunia, moja zaidi ya Messi, na kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao zaidi ya 10 katika msimu mmoja wa mashindano hayo tangu Gerd Müller 1970. Hata hivyo, haikuwa kile alichotamani.

“Ningependelea kutokuwa mfungaji bora na badala yake ningekuwa nimecheza fainali,” alisema nahodha huyo wa Ufaransa ambaye msimu wake wa klabu ulikuwa bora kwa upande wa mabao, lakini haukuwa na mafanikio ya mataji.

Alifunga mabao 42 katika mechi 44, akiwa mfungaji bora wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hakushinda taji lolote. Mabao yalikuwepo, lakini medali hazikufuata. Kama Kane alivyogundua, kufunga mabao pekee mara nyingi hakutoshi kushinda Ballon d’Or.