Messi anunua timu nyingine Hispania
Muktasari:
- Messi anatarajiwa kununua hisa zinazomilikiwa kwa sasa na kundi la uwekezaji la Colombia, Grupo TH, jambo litakalomfanya kuwa mbia mwenye hisa nyingi zaidi katika klabu hiyo.
ELDA, HISPANIA; NYOTA wa kimataifa wa Argentina na Inter Miami ya Marekani, Lionel Messi amefikia makubaliano ya awali ya kuwa mmiliki wa Klabu ya Eldense inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Hispania, Daily Mail Sport imethibitisha.
Messi anatarajiwa kununua hisa zinazomilikiwa kwa sasa na kundi la uwekezaji la Colombia, Grupo TH, jambo litakalomfanya kuwa mbia mwenye hisa nyingi zaidi katika klabu hiyo. Mkataba huo unatarajiwa kukamilishwa ndani ya siku chache zijazo baada ya taratibu za mwisho za kisheria na kimkataba kukamilika, pamoja na kupata idhini kutoka Baraza Kuu la Michezo la Hispania (CSD). Masharti ya kifedha ya muamala huo hayajawekwa wazi.
Klabu hiyo yenye maskani yake Valencia ilipanda daraja kwenda ligi ya pili mwishoni mwa msimu uliopita na imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu huu, ikikusanya pointi mbili katika mechi nne za mwanzo, suala lililosababisha kocha Claudio Barragan kufutwa kazi wiki iliyopita, hivyo kuiacha bila kocha.
Ununuzi wa Eldense wa Messi ni hatua ya hivi karibuni katika kuendelea kukua kwa himaya ya soka ya staa huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 39 ambaye miezi michache iliyopita alinunua asilimia 100 ya hisa za klabu nyingine ya Hispania, UE Cornella, ambayo ni nusu ridhaa na nusu ya kulipwa iliyopo pembezoni mwa Barcelona.
UE Cornella iliyoanzishwa 1951, inashiriki Ligi Daraja la Tano Hispania, na iliwahi kukaririwa ikisema kuwasili kwa Messi kuliashiria mwanzo wa mpya katika historia yake katika kukuza maendeleo ya soka na kitaasisi, kuimarisha misingi a kuendelea kuwekeza katika vipaji.
Messi, ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu kuichezea Argentina pia ana uwekezaji mwingine ingawa haulingani na ukubwa wake katika klabu hizo mbili za Hispania, ambapo anamiliki kwa pamoja klabu ya Deportivo LSM ya Uruguay pamoja na mshambuliaji mwenzake wa Inter Miami, Luis Suarez.
Pia ana haki ya moja kwa moja ya kununua hisa katika klabu yake ya Ligi Kuu Marekani, Inter Miami, inayomruhusu kuwa sehemu ya umiliki baada ya kumaliza maisha yake ya kucheza soka. Hata hivyo, wakati himaya yake ikiendelea kukua, Messi anaweza kukutana na kikwazo fulani.
Eldense na Cornella kwa sasa zinatenganishwa na madaraja matatu, lakini kuna uwezekano mkubwa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) lisiruhusu timu zote mbili kushiriki katika daraja moja endapo klabu hizo mbili zitafikia hatua hiyo siku zijazo.
Eldense iliyoanzishwa 1921, imetumia sehemu kubwa ya historia yake nje ya madaraja mawili ya juu ya soka la Hispania. Ilipanda hadi daraja la pili kwa mara ya kwanza tangu 1964 mwaka 2023, ikashuka daraja 2025 na kufanikiwa kurejea haraka msimu uliopita. Inacheza mechi zake za nyumbani katika Uwanja wa Nuevo Pepico Amat wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 5,776, uliopo katika Jiji la Elda.