Messi kuwaaga mashabiki Argentina Oktoba 6
Muktasari:
- Rais wa Shirikisho la Soka la Argentina (AFA), Claudio Tapia, amethibitisha kuwa mchezo huo utakuwa kwa ajili ya kumuaga Messi, huku akisema nahodha huyo anastahili kupewa nafasi ya kuagana na mashabiki wa timu ya taifa akiwa nyumbani.
Lionel Messi ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin utakaochezwa Oktoba 6, 2026 katika Uwanja wa Monumental, Buenos Aires, ukiwa maalum kwa kumuaga baada ya kustaafu soka la kimataifa.
Rais wa Shirikisho la Soka la Argentina (AFA), Claudio Tapia, amethibitisha kuwa mchezo huo utakuwa kwa ajili ya kumuaga Messi, huku akisema nahodha huyo anastahili kupewa nafasi ya kuagana na mashabiki wa timu ya taifa akiwa nyumbani.
Tapia amesema baada ya mazungumzo na kocha Lionel Scaloni, waliamua kumwalika Messi ambaye amemtaja kuwa mchezaji bora duniani na nembo ya timu ya taifa.
Baada ya Messi kukubali mwaliko huo, AFA pia imewaalika wachezaji wote wa Argentina waliotwaa Kombe la Dunia mwaka 2022 pamoja na familia zao kushiriki tukio hilo.
Kabla ya mchezo dhidi ya Benin, Argentina itacheza na Bolivia Septemba 30 kisha itakutana na Burkina Faso Oktoba 3.
Messi alitangaza kustaafu soka la kimataifa Agosti 31 kupitia ujumbe alioandika kwenye mtandao wake wa Instagram.