Messi anunua boti ya kifahari, Alcaraz ameagiza ya aina hiyo
Muktasari:
- Miongoni mwa wanamichezo hao ni nyota wa tenisi Rafael Nadal, bingwa mara mbili wa mashindano ya Formula One, Fernando Alonso, pamoja na dereva wa zamani wa Formula One, Nico Rosberg.
MIAMI, MAREKANI: MWANASOKA maarufu wa Argentina, Lionel Messi, ameagiza boti mpya ya kifahari aina ya Ultima 88 catamaran inayouzwa kati ya Sh22,44 bilioni na Sh28.25 bilioni kutoka Sunreef nchini Poland, akiungana na orodha ya wanamichezo mashuhuri wanaomiliki boti za kampuni hiyo.
Miongoni mwa wanamichezo hao ni nyota wa tenisi Rafael Nadal, bingwa mara mbili wa mashindano ya Formula One, Fernando Alonso, pamoja na dereva wa zamani wa Formula One, Nico Rosberg.
“Ni furaha kubwa kujiunga na familia ya Sunreef. Mimi na familia yangu tumekuwa tukipenda kutumia muda baharini kila tunapopata nafasi,” alisema Messi katika taarifa yake baada ya kutoa oda kwa kampuni husika ili kununua usafiri huo.
Nyota wa tenisi wa Hispania, Carlos Alcaraz, naye ameagiza boti ya aina hiyo ya Ultima 88 na anasubiri kukabidhiwa kwake.
BOTI YENYE UREFU WA FUTI 88
Boti hiyo yenye urefu wa futi 88, sawa na takribani mita 26.8, ilionyeshwa kwa mara ya kwanza kama wazo la usanifu 2023 na kampuni ya Sunreef na ni miongoni mwa boti kubwa zaidi katika kundi la Ultima, linalojumuisha miundo sita.
Ultima 88 imeundwa katika mfumo unaoifanya ipendeze zaidi ikiwa na nakshinakshi za kuvutia za madini mbalimbali katika eneo la juu sambamba na nafasi kubwa, utulivu pamoja na faraja inayopatikana ndani yake.
Boti ya kwanza ya aina hiyo ilizinduliwa Aprili mwaka huu, huku nyingine kadhaa zikiendelea kutengenezwa. Messi anapanga kuiingiza boti hiyo katika kundi la boti za kukodisha za MIM Ocean, mradi anaouendeleza kwa kushirikiana na kampuni ya Med Cat Yachts.
Kwa sasa, kundi hilo lina boti tatu ndogo zenye mwonekano wa kisasa zinazotengenezwa na Bali Catamarans, kampuni iliyo chini ya Catana Group. Kuingia kwa Ultima 88 ni ongezeko la ufahari kwa vyombo hivyo vya majini na hasa kutokana na ukubwa wa ndani na uwezo wake wa kuhimili misukosuko ya mawimbi.
Hata hivyo, Messi hatakuwa akiitumia kwa biashara ya ukodishaji pekee, kwani pia amepanga kuitumia yeye mwenyewe.
“Sunreef Yachts wana mtindo na vipengele ninavyovipenda, na wanaendana kikamilifu na kile ninachokitafuta. Ninasubiri kwa hamu kuifurahia Ultima 88 pamoja na familia yangu,” aliongeza Messi.
VYUMBA VYA KULALA, ENEO LA MAPUMZIKO
Boti hiyo inaundwa ikiwa na nafasi ya kutosha kumhudumia Messi pamoja na watu watakaokuwa naye, ambapo ina chumba kikuu cha kulala kinachokuwa na upana sawa wa boti kwa chini na vyumba vingine vinne vya kawaida kwa ajili ya wageni.
Pia ina eneo kubwa la kubarizi nje na la juu linalojulikana, ambalo linaweza kutumika kwa ajili ya burudani, mapumziko au kufanya mazoezi huku watumiaji wakifurahia mazingira ya baharini. Sehemu ya nyuma ya boti ina eneo maalumu la mapumziko linaloitwa ocean lounge. Eneo hilo lina matuta yanayoweza kufunguliwa pembeni ili kuongeza nafasi ya kukaa karibu na maji au kushiriki michezo ya majini.
Karibu na eneo hilo kuna sehemu maalumu ya kuhifadhi pikipiki za majini aina ya Jet Ski na vifaa vingine vinavyofanana navyo.
INJINI ZENYE NGUVU 2,000
Ultima 88 inaweza kutengenezwa kwa mfumo wa kawaida wa injini za dizeli au mfumo mseto unaosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.
Pia inaweza kuwekwa teknolojia ya 'solar skin' inayotumia nishati ya jua kuzalisha umeme kwa njia rafiki kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
Kwa mujibu wa Sunreef, boti aliyoagiza Messi itakuwa na injini mbili zenye nguvu za farasi 1,000 kila moja, hivyo kuwa na jumla ya nguvu za farasi 2,000. Kampuni hiyo inasema mfumo huo utaiwezesha boti hiyo kuwa na mchanganyiko mzuri wa kasi na uwezo wa kugeuka au kubadilisha mwelekeo kwa urahisi.
Kwa sasa, boti ya Messi inaendelea kujengwa katika kiwanda cha kisasa cha Sunreef kilichopo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).