Mbappe afunika, Hispania wafagia tuzo
Muktasari:
- Mbappe alimaliza mashindano ya Kombe la Dunia 2026 akiwa mfungaji bora kwa mabao 10 katika mechi nane, akimzidi Lionel Messi aliyefunga mabao nane.
NEW YORK, MAREKANI: NAHODHA na mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe, ameweka rekodi mpya katika historia ya Kombe la Dunia baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda Kiatu cha Dhahabu mara mbili mfululizo, huku mabingwa Hispania wakifagia tuzo nyingine zote za binafsi.
Mbappe alimaliza mashindano ya Kombe la Dunia 2026 akiwa mfungaji bora kwa mabao 10 katika mechi nane, akimzidi Lionel Messi aliyefunga mabao nane.
Baada ya kutwaa Kiatu cha Dhahabu pia kwenye Kombe la Dunia la Qatar mwaka 2022 akiwa na mabao nane, nyota huyo wa Real Madrid sasa ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo katika Kombe la Dunia mbili mfululizo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, pia ameweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia kwa wanaume akiwa na mabao 22, akimpita Messi aliyebaki na mabao 21.
Mbappe pia amekuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 10 katika Kombe la Dunia moja tangu Gerd Muller wa Ujerumani Magharibi alivyofanya hivyo mwaka 1970.
Ni Just Fontaine wa Ufaransa aliyefunga mabao 13 mwaka 1958 na Sandor Kocsis wa Hungary aliyefunga 11 mwaka 1954 pekee waliofunga mabao mengi zaidi katika mashindano moja ya Kombe la Dunia.
Rekodi tamu, lakini...
Mbappe aliifikia rekodi hiyo baada ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu dhidi ya England, ingawa Ufaransa ilipoteza kwa mabao 6-4 na kumaliza katika nafasi ya nne.
"Ukifunga mabao mengi kiasi hiki kwenye Kombe la Dunia, ni jambo kubwa sana kwa historia yako," alisema Mbappe.
"Lakini ningependelea nisiwe mfungaji bora kama tungefika fainali. Rekodi hii itanisaidia baada ya kustaafu, lakini kwa sasa hicho si kitu ninachokiwaza."
Mbappe alifunga mabao mawili dhidi ya Senegal na Iraq katika hatua ya makundi, kabla ya kuongeza mengine dhidi ya Sweden, Paraguay na Morocco.
Messi alikuwa na nafasi ya kumpiku Mbappe kama angefunga hat-trick kwenye fainali dhidi ya Hispania, lakini alishindwa kuifumania nyavu katika mchezo ambao Argentina ilipoteza kwa bao 1-0.
Jude Bellingham wa England na Erling Haaland wa Norway walimaliza mashindano wakiwa na mabao saba kila mmoja, huku Ousmane Dembele wa Ufaransa na Harry Kane wa England wakifunga mabao sita.
Rodri atwaa Mpira wa Dhahabu
Nahodha wa Hispania, Rodri, alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano na kutunukiwa Golden Ball baada ya kuiongoza timu yake kutwaa ubingwa wa dunia.
Kiungo huyo wa Manchester City alipokea tuzo hiyo kutoka kwa Rais wa FIFA, Gianni Infantino, mara baada ya fainali kumalizika kwenye Uwanja wa MetLife.
Ni tuzo ya tatu kubwa binafsi kwa Rodri baada ya kushinda Ballon d'Or mwaka 2023 na kuwa Mchezaji Bora wa Euro 2024.
Lionel Messi alishinda Silver Ball kama mchezaji wa pili bora wa mashindano, huku Mbappe akitunukiwa Bronze Ball.
Unai Simon aangaza langoni
Kipa wa Hispania, Unai Simon, alitwaa tuzo ya Golden Glove baada ya kuwa kipa bora wa mashindano.
Simon aliruhusu bao moja pekee katika mechi nane, huku akimaliza michezo saba bila kuruhusu bao.
Kipa huyo wa Athletic Club alimshinda David Raya katika kinyang'anyiro cha kuwa namba moja wa Hispania na akalipa imani ya kocha Luis de la Fuente kwa kiwango bora kilichochangia ubingwa wa dunia.
Cubarsi nyota chipukizi
Beki wa Barcelona mwenye umri wa miaka 19, Pau Cubarsi, alitangazwa kuwa Mchezaji Bora Kijana wa Kombe la Dunia.
Cubarsi alicheza kila dakika ya mashindano hayo na kuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya Hispania iliyofungwa bao moja tu katika mashindano yote.
Katika fainali dhidi ya Argentina, safu hiyo iliruhusu wapinzani kupiga mashuti mawili pekee, huku hakuna hata moja lililolenga lango.
Kwa kiwango hicho, Cubarsi ameendelea kuthibitisha kuwa mmoja wa mabeki wenye mustakabali mkubwa zaidi katika soka la dunia.