Mayele aagana na Pyramids FC, atajwa Libya, Saudia
Muktasari:
- Katika msimu wa 2024/2025, Mayele aliondoka na tuzo binafsi ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya kuitumikia Pyramids FC kwa miaka imitatu, mshambuliaji Fiston Mayele ameiaga rasmi klabu hiyo huku akishindwa kuweka wazi ni klabu ipi atajiunga nayo.
Mayele mwenye umri wa miaka 32, anaondoka Pyramids FC akiwa mchezaji huru na mwenyewe ametoa shukrani kwa klabu hiyo.
"Kila stori ina mwisho wake lakini kumbukumbu zinadumu milele. Asante kwa Rais, wafanyakazi, wachezaji wenzangu, mashabiki na kila mmoja aliyekuwa na imani na mimi tangu ujio wangu.
"Tumeandika ukurasa mzuri wa historia pamoja sambamba na mataji, hisia na nyakati zisizosahaulika. Leo ni muda wangu kukabiliana na changamoto mpya. Ninaiacha klabu hii kwa shukrani na heshima kubwa. nawatakia kila la kheri kwa hapo baadaye," amesema Mayele.
Akiwa na Pyramids FC, Mayele ameshinda mataji manne ambapo kati ya hayo, moja ni la mashindano ya ndani na matatu ya kimataifa.
Taji la ndani ambalo Mayele ameshinda akiwa na Pyramids FC ni Kombe la Misri ambalo wamelichukua mwaka jana.
Kimataifa, mataji matatu ambayo Mayele ametwaa akiwa na Pyramids FC ni Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025, taji la CAF Super Cup 2025 na taji la Kombe la Mabara 2025.
Katika msimu wa 2024/2025, Mayele aliondoka na tuzo binafsi ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pia Mayele alikuwa Mfungaji Bora wa Kombe la Mabara akipachika mabao matatu.
Licha ya kuaga Pyramids FC, bado Mayele hajaweka wazi ni wapi ataelekea huku kukiwa na ofa kutoka klabu mbalimbali nje na ndani ya Afrika.
Inaripotiwa kwamba Mayele ana ofa kadhaa kutoka klabu za Libya na Saudi Arabia.
Mayele anaondoka Pyramids FC akiwa ameichezea timu hiyo idadi ya michezo 125. akifunga mabao 54 na kupiga pasi tisa za mwisho.