Mawinga wanne ubaoni Barcelona

Muktasari:
- Mabingwa hao wa La Liga walishuhudia safu yao ya ushambuliaji ikiwa tishio msimu uliopita kwa wakali wawili wanaotajwa kwenye tuzo ya Ballon d'Or, Lamine Yamal na Raphinha kuwasha moto kwa kuchangia mabao 102 kwa ama kufunga wenyewe na kuasisti kwa wachezaji wenzao.
BARCELONA, HISPANIA: SUPASTAA, Marcus Rashford ni moja ya mawinga wanne wanaotajwa kuwa kwenye rada za Barcelona inaowasaka kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mabingwa hao wa La Liga walishuhudia safu yao ya ushambuliaji ikiwa tishio msimu uliopita kwa wakali wawili wanaotajwa kwenye tuzo ya Ballon d'Or, Lamine Yamal na Raphinha kuwasha moto kwa kuchangia mabao 102 kwa ama kufunga wenyewe na kuasisti kwa wachezaji wenzao.
Hata hivyo, kocha wa Barcelona, Hansi Flick anataka fowadi yake kuwa ya moto zaidi msimu ujao hasa baada ya kuona timu hiyo imekomea kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan.
Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, baada ya usajili wa kipa Joan Garcia kwa ada ya Pauni 21 milioni kutoka Espanyol, kipaumbele kwa sasa kimehamia katika kuongeza mshambuliaji anayetumia mguu wa kushoto.
Na kwenye hilo, kuna orodha ya washambuliaji wanne imewekwa ubaoni ili kuwafukuzia kupata saini ya mmoja wao.
Kwenye orodha hiyo, kipaumbele cha kwanza cha Barcelona ni staa wa Liverpool, Luis Diaz, ambaye amekuwa kwenye rada za timu hiyo kwa muda mrefu, wakati staa wa Manchester United, Rashford naye yuko kwenye orodha.
Winga mwingine kwenye orodha hiyo anayesakwa na Barcelona ni mkali wa Athletic Bilbao, Nico Williams - huku kukiwa na mchezaji ambaye ni chaguo jepesi zaidi kwao kwa maana ya kumpata bure, mkali wa Croatia, Ivan Perisic, ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kutemwa na PSV ya Uholanzi.
Diaz ni shabiki wa Barca tangu utotoni, hivyo bila shaka atakuwa tayari kwenda kukipiga kwenye La Liga, akijiandaa kuondoka Anfield baada ya kufunga mabao 17 na asisti nane kwenye michuano yote msimu ulioisha. Liverpool inafungua milango kwa sababu tayari imeshamnyakua Florian Wirtz kwa ada ya Pauni 116.5 milioni kutoka Bayer Leverkusen.
Diaz anaweza kugharimu Pauni 51 milioni. Rashford naye ataweza kupatikana sokoni kwa sababu kocha wa Man United, Ruben Amorim hamwoni kama ana kitu anachoweza kukifanya kwenye timu yake na ndio maana alimtoa kwa mkopo kwenye dirisha la Januari kwenda Aston Villa, ambako alichangia mabao 10 katika mechi 17.
Huduma yake inaweza kupatikana kwa Pauni 40 milioni na bosi wa usajili wa Barcelona, Deco alikiri mchezaji huyo anafaa kwenda kukipiga kwenye kikosi hicho cha miamba hiyo ya Hispania.
Williams naye amekuwa kwenye rada, huku Mhispaniola huyo ni swahiba mkubwa wa winga wa sasa wa miamba hiyo, Yamal, wakicheza kwa mafanikio makubwa kwenye soka la timu ya taifa ya Hispania.