Matajiri Saudi Arabia wanamtaka Andre Onana
Muktasari:
- Onana aliyesajiliwa kwa Pauni 47.2 milioni kutoka Inter Milan katika dirisha la majira ya joto mwaka 2023, amekuwa akisemwa sana na mashabiki kutokana na makosa ambayo amekuwa akiyafanya tangu msimu uliopita.
MANCHESTER United iko tayari kumruhusu kipa wake wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana, 29, kujiunga na klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Onana aliyesajiliwa kwa Pauni 47.2 milioni kutoka Inter Milan katika dirisha la majira ya joto mwaka 2023, amekuwa akisemwa sana na mashabiki kutokana na makosa ambayo amekuwa akiyafanya tangu msimu uliopita.
Mbali ya Al Nassr huduma ya kipa huyu pia inahitajika na Neom SC ya Saudi Arabia ambayo inadaiwa kuweka mezani ofa ya mshahara wa zaidi ya Pauni 15 milioni kwa msimu.
Awali, Man United ilisitisha mpango wa kumuuza kwa sababu ilitaka kwanza kuona kama Altay Bayındır ataonyesha kiwango bora au laa.
Hata hivyo, katika mechi kadhaa za mwanzo wa msimu, Onana na Bayındır wote wameonyesha viwango ambayo haviridhishi jambo lililosababisha mashetani hao wekundu kumsajili Senne Lammens kutoka Royal Antwerp ili akawe kipa wao namba moja.
Kitendo cha Lammens kusajiliwa kinasababisha Onana ambaye tangu msimu kuanza alikuwa kipa namba mbili, kwenda kuwa kipa namba tatu jambo ambalo ameonyesha kuwa halitaki na kuwasilisha ombi la kuuzwa ambalo limekubaliwa na vigogo wa Man United.
Murillo
BEKI kisiki wa Nottingham Forest na Brazil, Murillo, 23, ameziingiza vitani Arsenal na Barcelona zinazohitaji saini yake kuelekea dirisha lijalo. Murillo alijiunga na Forest kutoka Corinthians mwaka 2023 kwa Euro 12 milioni amekuwa akihusishwa na vigogo wengi barani Ulaya tangu Januari mwaka hii. Forest inaweza kumruhusu kwa dau la kuanzia Pauni 45 hadi 50 milioni. Arsenal wanamwona kama mrithi wa muda mrefu wa Gabriel Magalhaes, huku Barcelona ikimtaka azibe pengo la Araujo.
Casemiro
KIUNGO wa kimataifa wa Brazil, Casemiro, 33, anayeichezea Manchester Unied ameamua kubaki timu hiyo licha ya kupata ofa kubwa kutoka Al-Nassr hivi karibuni. Inaelezwa Casemiro ameamua kusalia kwa sababu anataka kuendelea kucheza katika ligi yenye ushindani ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuitwa katika kikosi cha Brazil kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Antony
WINGA wa timu ya taifa ya Brazil, Antony, 25, amefichua kuwa alizungumza na viongozi wa Bayern Munich kabla ya kujiunga na Real Betis, ambayo aliichezea kwa mkopo msimu uliopita. Antony alinunuliwa na Man United kutoka Ajax mwaka 2022 kwa ada ya takribani Pauni 82 milioni, lakini hakuonyesha kiwango bora kwenye EPL, hali iliyosababisha muda mwingi awe nje ya uwanja.
Gabriel Martinelli
INAELEZWA Arsenal ilikuwa tayari kumuuza winga wake wa kimataifa wa Brazi, Gabriel Martinelli, 24, kwa Pauni 60 milioni katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, dili hilo lilishindikana kufanyika kwa sababu timu nyingi zilizojitokeza kumhitaji zilikuwa tayari kulipa Pauni 40 milioni tu kiasi ambacho Arsenal haikuonekana kukubaliana nacho.
Martinelli ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Arsenal amekuwa akirudishwa sana nyuma na majeraha.
Jota Silva
BAADA ya dili lake la kurejea Ureno kujiunga na Sporting Lisbon kufeli, mshambuliaji wa Wolves, Jota Silva, 26, ameingia katika rada za klabu za Saudi Arabia na Uturuki. Klabu ya Neom SC kutoka Saudi Pro League ndio inaongoza katika vita hiyo ikipewa nafasi kubwa kutokana na ofa ya mshahara mnono wa Euro 8 milioni kwa mwaka iliyoweka mezani.
Randal Kolo Muani
JUVENTUS imekuwa ilikuwa ikimfuatilia mshambuliaji wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa, Randal Kolo Muani, 26, kwa miezi kadhaa kabla ya dirisha lililopita kufungwa lakini ilishindikana kumpata kwa sababu ofa iliyoweka mezani ilikuwa ndogo zaidi ya ile ambayo Tottenham Hotspur iliweka mezani.
Kolo Muani, ambaye alijiunga na PSG akitokea Eintracht Frankfurt kwa Euro 95 milioni mwaka 2023, ametua Spurs kwa mkopo wa msimu mmoja.
Nathan Ake
TOTTENHAM inafikiria kuanzisha mazungumzo na Manchester City ifikapo Januari mwakani kwa ajili ya kuipata saini ya beki wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Uholanzi, Nathan Ake. Spurs ilikuwa ikihitaji saini ya staa huyu katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini mchakato ulifeli. Ake ni mmoja kati ya wachezaji ambao kocha wa Man City, Pep Guardiola amewapa ruhusa ya kuondoka wakipata timu.