Ronaldo ataja mwisho wake
Muktasari:
- Mreno huyo amefunga mabao 953 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, alisema atastaafu soka katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili.
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amethibitisha kwamba fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakuwa za mwisho kwake kwenye mchezo wa soka.
Mreno huyo amefunga mabao 953 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, alisema atastaafu soka katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili.
Ronaldo, 40, anajiandaa kwenda kuweka rekodi ya kucheza fainali za sita za Kombe la Dunia katika michuano hiyo itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico majira yajayo ya kiangazi.
Ureno inaongoza Kundi F na itakamatia tiketi ya kucheza fainali hizo za Kombe la Dunia 2026 endapo itafanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Republic of Ireland, Alhamisi.
Ronaldo aliulizwa kama fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakuwa za mwisho kwake kwenye soka.
Staa huyo, ambaye hivi karibuni alisaini dili la pesa nyingi huko Al-Nassr, ambapo atakuwa na timu hiyo hadi 2027, alisema: “Bila shaka. Nitakuwa na miaka 41 kipindi hicho.
“Kwenye soka, najaribu kufurahia nyakati. Nina umri wa miaka 40, hivyo najaribu kufurahia kila nyakati. Nataka kuendelea kucheza kwa sababu najisikia vizuri, mwili wangu upo vizuri na kiwango chake kipo vizuri, kila kitu kinajieleza uwanjani.”
Ronaldo anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi na kucheza mechi nyingi kwenye soka la kimataifa, akifunga mara 143 katika mechi 225.
Katika mabao hayo, 83 alifunga baada ya kutimiza miaka 30 ya kuzaliwa, ikiwa ni zaidi ya aliyofunga kinara wa mabao wa muda wote wa England, Harry Kane, aliyefunga 76.
Kocha wa sasa wa Ureno, Roberto Martinez amekuwa mwenye imani kubwa na Ronaldo na hilo limelipa akifunga mabao 25 katika mechi 29 alizocheza chini yake. Kwenye mahojiano yake ya siku za hivi karibuni, Ronaldo alisema anataka kucheza walau hadi hapo atakapofikisha mabao 1,000.