Marcus Rashford mambo magumu Barcelona
Muktasari:
- Rashford alitua Barca dirisha la usajili la majira ya kiangazi lililopita kwa mkopo akitokea Manchester United baada ya kushindwa kuingia kwenye kikosi cha Kocha Ruben Amorim kutokana na kutokuelewana kwa wawili hao, ikiwamo kutoendana na mfumo wake.
BARCELONA, HISPANIA: LICHA ya kutimiza ndoto yake ya kucheza Barcelona, lakini mpango uliopo wa mabosi wa miamba hiyo ya Ligi Kuu Hispania, La Liga, ni kumrudisha mshambuliaji Marcus Rashford England kutokana na kutokuridhika na kiwango chake.
Rashford alitua Barca dirisha la usajili la majira ya kiangazi lililopita kwa mkopo akitokea Manchester United baada ya kushindwa kuingia kwenye kikosi cha Kocha Ruben Amorim kutokana na kutokuelewana kwa wawili hao, ikiwamo kutoendana na mfumo wake.
Ripoti iliyotolewa na vyombo vya habari vya Hispania inaeleza nyota huyu, 27, aliyekuwa na ndoto ya kucheza Nou Camp hajawaridhisha mabosi wa Barca kutokana na kiwango cha chini alichoonyesha katika mechi zake tatu za mwanzo na wanajadili uwezekano wa kumsitishia mkataba wake kabla ya Krismasi.
Awali kulikuwa na kipengele kitakachoiruhusu Barca kumnunua jumla kwa Pauni 30 milioni mwisho wa msimu, lakini kutokana na kiwango duni, huenda akarudi Old Trafford licha ya kwamba miamba hiyo ya Catalonia bado italazimika kuilipa Man United Pauni 4.3 milioni kama fidia ya kuvunja makubaliano.
Rashford alipambana sana kuhakikisha anatua Barca baada ya kocha Amorim kumwondoa yeye na wachezaji wengine katika kikosi akidai hawaendani na mifumo yake na miamba hiyo ya La Liga kumgeukia baada ya kushindwa kumsajili Luis Diaz wa Liverpool na Nico Williams wa Athletic Bilbao kutokana na ada kubwa za uhamisho.
Kocha Hans Flick alikuwa na matarajio ya kuona kiwango bora cha Rashford ambacho aliwahi kukionyesha hapo awali na alikuwa mmoja ya wachezaji waliowika sana Ulaya kwa wakati huo na matumaini hayo yalikuja zaidi baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi za maandalizi ya msimu huu.
Lakini katika ligi hali ni tofauti. Rashford hajafunga wala kutoa pasi ya bao katika michezo yake mitatu ya mwanzo na aliondolewa uwanjani wakati wa mapumziko katika ushindi wa kusisimua wa Barca wa mabao 3-2 dhidi ya Levante.
Katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Mallorca, aliingia akitokea benchi, kisha akapewa nafasi ya kuanza kwa mara ya kwanza Agosti 23, lakini akatolewa mapumziko wakati Barca ikiwa inaongozwa kwa mabao 2-0.
Mabadiliko yaliyofanywa na Flick kwa kumwingiza Dani Olmo yalisaidia, kwani Barca ilisawazisha kwa mabao ya Pedri na Ferran Torres kabla ya Levante kujifunga bao la tatu.
Akieleza sababu za kumtoa Rashford katika mchezo huo, Flick alisema: "Ni wazi kipindi cha pili tulihitaji kubadilisha kitu. Sikuweza kumtoa Raphinha upande wa kushoto kwa sababu ndiye namba 11 wetu. Anajua kila kitu tunachotaka kufanya.
Hata hivyo, kocha huyo Mjerumani alisisitiza bado hajakata tamaa na nyota huyo wa Manchester United: "Nadhani Marcus alikuwa na baadhi ya nafasi kipindi cha kwanza na alionyesha jinsi alivyo mzuri na jinsi anavyoweza kutusaidia. Hapo ndipo tunapaswa kuendelea."
Licha ya maneno hayo ya kocha ripoti zinadai klabuni mambo yapo tofauti.
Tovuti ya El Nacional inaeleza rais wa klabu Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo Deco hawakuwa wanampigia hesabu staa huyo na ilitokea tu kumsajili baada ya kuwakosa Diaz na Williams, hivyo wanafikiria kusajili mchezaji mwingine Januari.