Manchester United inashangaa ishu ya kuuzwa
Muktasari:
- Usiku wa Jumatano, bosi mmoja wa Saudi Arabia, Turki Al-Sheikh, aliposti kwenye mtandao wa kijamii akidai kwamba Man United imepata mwekezaji mpya, jambo ambalo mashabiki na wafanyakazi kwa klabu hiyo kusubiri kwa hamu kupata taarifa ya kinachoendelea.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeripotiwa kupigwa butaa baada ya kuibuka kwa madai kwamba kuna mwekezaji mpya anatarajia kuichukua timu hiyo na kila kitu kipo kwenye hatua za mwisho kukamilika.
Usiku wa Jumatano, bosi mmoja wa Saudi Arabia, Turki Al-Sheikh, aliposti kwenye mtandao wa kijamii akidai kwamba Man United imepata mwekezaji mpya, jambo ambalo mashabiki na wafanyakazi kwa klabu hiyo kusubiri kwa hamu kupata taarifa ya kinachoendelea.
Posti hiyo kwenye mtandao wa X kutoka kwa Al-Sheikh ilibainisha: “Taarifa nzuri nilizosikia ni kwamba Manchester United ipo kwenye hatua nzuri ya mazungumzo ya kuuzwa kwa mwekezaji mpya. Natumaini atakuwa bora kuliko wawekezaji waliopita.”
Posti hiyo ya Al-Sheikh imekuja saa kadhaa baada ya mmiliki mwenza wa Man United, Sir Jim Ratcliffe kufanyiwa mahojiano, ambayo hakuzungumza chochote kama kuna mpango wa kuondoka Old Trafford.
Mwaka 2023, Sheikh Jassim na Ratcliffe walikuwa kwenye mazungumzo na The Raine Group, iliyokuwa inapiga mnada sehemu ya hisa za umiliki wa klabu hiyo kutoka kwa familia ya Glazers.
Baada ya mchuano mkali, hatimaye Ratcliffe aliibuka mshindi kwa kununua hisa chache za umiliki wa klabu hiyo. Sheikh Jassim aliwasilisha ofa yake ya Pauni 5.5 bilioni kwa ajili ya kuinunua klabu hiyo, lakini tajiri huyo wa Qatar alishindwa kuwasilisha uhakika wa pesa hizo katika kipindi cha majadiliano. Sheikh Jassim aliahidi pia kulipa madeni yote ya Man United.
Bado hakuna uhakika kama Sheikh Jassim atarudi tena na ofa nyingine ya kuinunua Man United.
Lakini, Turki Alalshikh alitoa ufafanuzi wa posti yake, aliposema: “Ipo posti yangu ya kuhusu Man United kuuzwa ilikuwa na maana moja: klabu ipo kwenye hatua ya juu ya mazungumzo ya kuhusu mwekezaji mpya. Nataka kuweka wazi tu hilo, mimi sio mwekezaji na wala hatokei kwenye nchi yangu. Nimeposti hiyo kama shabiki na napenda mambo mazuri yatokee, pengine inaweza kuwa sio lazima pia itokee.”
Kwa mujibu wa Daily Mail kuna kundi moja la washirika la kutoka UAE linafikiria kupeleka ofa ya kuinunua Man United kwa dili litakalozidi Pauni 5 bilioni.
Kinachoelezwa ni kwamba kundi hilo tayari limeshazungumza na wachezaji wa zamani wa Man United ili kusapoti mpango huo kama mabalozi. Hata hivyo, kinachoelezwa ni kwamba bado hakuna mawasiliano na mabosi wa Man United, ambao wamekanusha kwamba mazungumzo yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Chanzo cha karibu na mabosi wa klabu hiyo kilibainisha taarifa hizo zimekuwa sapraizi kwao na hawafahamu zimelenga nini hasa.
Wamiliki wa klabu ya Man United familia ya Glazer iligomea ofa kubwa ya Pauni 5 bilioni kutoka kwa Sheikh Jassim Al Thani karibu miaka miwili iliyopita.
Badala yake ilikubali ofa ya tajiri Ratcliffe ya Pauni 1.25 bilioni kwa ajili ya kumiliki asilimia 27.7 ya hisa za klabu hiyo. Man United ipo kwenye mazungumzo ya kwenda kucheza mechi huko Saudi Arabia kwa ajili ya kupata pesa, huku mechi hizo zikidaiwa kuandaliwa na Alalshikh.