Manchester derby... Wagonjwa Ni wengi!
Muktasari:
- Hisia za wengi zitakuwa huko Manchester, wakati itakapopigwa dabi ya mahasimu, Manchester City na Manchester United uwanjani Etihad, Jumapili hii.
MANCHESTER, ENGLAND: MAPUMZIKO ya mechi za kimataifa yanafika ukingoni na sasa mastaa wanarudi kujiunga na timu zao za klabu kwa ajili ya kuendelea na mchakamchaka wa ligi ikiwamo Ligi Kuu England.
Hisia za wengi zitakuwa huko Manchester, wakati itakapopigwa dabi ya mahasimu, Manchester City na Manchester United uwanjani Etihad, Jumapili hii.
Timu hizo mbili zimeanza msimu huu wa Ligi Kuu England katika kasi hafifu sana, hasa kwa chama la Pep Guardiola, Man City ambalo limepoteza mechi mbili mfululizo.
Man City ilipoteza uongozi wake wa bao 1-0 na kuchapwa 2-1 dhidi ya Brighton kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa, hiyo ikifuatia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tottenham.
Guardiola atahitaji kurekebisha mambo kwenye kikosi chake, lakini sasa atakabiliana na Man United huku akiwa na majeruhi kibao kwenye kikosi chake.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim, alikwenda mapumziko ya ligi kupisha mechi za kimataifa akiwa mwenye furaha baada ya timu yake kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Burnley. Lakini, kwenye ushindi huo wa 3-2 uliwashuhudia wachezaji wake wawili wakipata majeraha uwanjani Old Trafford. Kutokana na hilo, kuna mastaa kadhaa wa timu zote mbili wanaweza kukosa kipute hicho cha Manchester Derby kitakachopigwa Jumapili kutokana na kuwa majeruhi.
Omar Marmoush hatakuwapo kwenye kikosi cha Man City baada ya kuumia goti kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Misri dhidi ya Burkina Faso, Jumanne iliyopita.
Staa huyo aliyeanzishwa kwenye mechi mbili zilizopita za Man City, alilazimika kutoka uwanjani dakika ya tisa wakati Misri na Burkina Faso zikiwa hazijafungana huko Ouagadougou.
Man City itaendelea kumkosa Rayan Cherki, ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili baada ya kuumia paja kwenye mechi ya Brighton. Kuna tatizo jingine pia kwenye fowadi hiyo ya Man City, Phil Foden alikosa mechi ya Brighton na Savinho naye hakuwapo. Klabu inaamini Foden anaweza kurudi kwenye mechi hiyo ya Jumapili, lakini bado hakuna uhakika.
Man City shida haishii hapo, Mateo Kovacic na Kalvin Phillips hawapo uwanjani kwa muda mrefu, huku John Stones naye akiwa kwenye hatihati baada ya maumivu ya misuli kumwondoa kwenye kikosi cha England. Abdukodir Khusanov alitolewa kwenye dakika za mwisho dhidi ya Brighton baada ya kuhisi maumivu, lakini anaweza kucheza dhidi ya Man United, huku Josko Gvardiol akiwa hajacheza mechi yoyote msimu huu.
Man United yenyewe ina shida chache ya kuzifikiria, lakini Lisandro Martinez ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa sababu bado hajapona vizuri maumivu yake ya goti.
Amorim anaamini Diogo Dalot atakuwa amepona baada ya kujiondoa kikosini Ureno kutokana na maumivu ya misuli, wakati kocha huyo akisubiri kwa hamu kuweka hadharani hali ya kiafya ya mastaa wake wawili, Mason Mount na Matheus Cunha ambao wote walipata majeraha kwenye mechi dhidi ya Burnley.
“Tutawafanyia vipimo,” alisema Amorim na kuongeza. “Tunawahitaji sana hawa watu ili tuweze kushindana.” Kuna ishara chanya kwa Cunha kutokana na ujumbe wake aliotua kwenye mitandao ya kijamii kwamba anaweza kuwa fiti kwa ajili ya kipute hicho cha Manchester derby.