Man United yatafuta kipa
Muktasari:
- Kocha mpya wa Man United, Ruben Amorim ameanza kuwa na mashaka juu ya kiwango cha Andre Onana, ambaye aliruhusu mpira wa kona uingie kwenye nyavu zake moja kwa moja bila ya kuguswa na yeyote katika kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wolves kwenye Boxing Day.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inafikiria kusajili kipa mpya, huku kinda wa Kibelgiji, Senne Lammens akiwekwa kwenye mpango.
Kocha mpya wa Man United, Ruben Amorim ameanza kuwa na mashaka juu ya kiwango cha Andre Onana, ambaye aliruhusu mpira wa kona uingie kwenye nyavu zake moja kwa moja bila ya kuguswa na yeyote katika kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wolves kwenye Boxing Day.
Kipa Mturuki Altay Bayindir, naye alifungwa kwa kona ya moja kwa moja kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Tottenham na sasa, anaweza kufunguliwa mlango kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili akajiunge na timu nyingine itakayompa nafasi.
Licha ya kwamba kipa mpya si kipaumbele dirisha la Januari, lakini Man United inafikiria kufanya maboresha eneo hilo mwisho wa msimu.
Na sasa, wanamfuatilia kipa wa Royal Antwerp, Lammens, 22, ambaye anaweza kuigharimu timu hiyo hadi Pauni 20 milioni.
Kipa huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji ya Under-21 alinaswa na timu yake ya sasa akitokea Club Brugge 2023 na tayari ameshazivutia timu nyingi ikiwamo Leeds United ya England. Licha ya kutokuwa na uzoefu wa kutosha, Man United inaamini huduma yake itakuwa bora wakimnasa. Kiwango cha Onana kimekuwa cha kupanda na kushuka. Kipa huyo Mcamerooni, alinaswa kwa Pauni 47 milioni akitokea Inter Milan miezi 18 iliyopita.