Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United mara saba mastaa wameipinga hadharani

MASTAA Pict

Muktasari:

  • Wiki moja kabla ya hapo, Martinez alitaka mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo afanye zaidi, akionekana pia kuikosoa menejimenti baada ya United kufungwa mabao 2-0 ugenini na Atletico Madrid.

LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imekuwa ikikumbana na kauli za ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wachezaji wake, huku Bruno Fernandes na Lisandro Martinez wakiibua mjadala kuhusu mbinu za ufundishaji na uongozi wa klabu hiyo katika siku za hivi karibuni.

Fernandes alihoji mbinu za timu baada ya kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Como Jumatano iliyopita, akielekeza lawama kwa uamuzi ya kocha na benchi lake la ufundi.

Wiki moja kabla ya hapo, Martinez alitaka mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo afanye zaidi, akionekana pia kuikosoa menejimenti baada ya United kufungwa mabao 2-0 ugenini na Atletico Madrid.

Hata hivyo, wawili hao si wa kwanza miongoni mwa wachezaji wa United kueleza hadharani kutoridhishwa kwao na mambo yanayoendelea ndani ya klabu hiyo. Katika historia yake, klabu hiyo imewahi kushuhudia mastaa wakikosoa uongozi, makocha na wenzao wa timu.

Hawa hapa wachezaji saba waliowahi kuibua mikwaruzano ya wazi na Manchester United.


MASTA 01

1. CRISTIANO RONALDO — 2022

Cristiano Ronaldo alitikisa dunia ya soka Novemba 2022 baada ya kufanya mahojiano na Piers Morgan, ambamo aliikosoa klabu hiyo na familia ya Glazer inayomiliki United.

“Wamiliki wa klabu, familia ya Glazer, hawajali klabu wala mchezo wa kulipwa,” alisema Ronaldo.

Pia aliitaja United kuwa klabu inayojali zaidi masoko na kueleza kuwa ingekuwa vigumu kurejea kileleni ndani ya miaka miwili au mitatu iliyofuata.

Ronaldo alisema alitaka kuiona klabu hiyo ikifanikiwa, lakini akakiri kuwa hakuwa na heshima kwa aliyekuwa kocha, Erik ten Hag.

Muda mfupi baadaye, mkataba wake na United ulivunjwa kwa makubaliano ya pande zote.


MASTA 02

2. JADON SANCHO — 2023

Jadon Sancho alipingana hadharani na Ten Hag Septemba 2023 baada ya kocha huyo kueleza kuwa mchezaji huyo aliachwa nje ya kikosi kilichocheza dhidi ya Arsenal kutokana na kiwango chake mazoezini.

Ten Hag alisema: “Jadon, kutokana na kiwango chake mazoezini, hatukumchagua. Unapaswa kufikia kiwango kinachotakiwa kila siku ukiwa Manchester United.”

Sancho alijibu kupitia mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa asingekubali kusemwa mambo ambayo hayakuwa ya kweli.

“Sitakubali watu kusema mambo ambayo si ya kweli kabisa. Kwa muda mrefu nimekuwa nikifanywa wa kulaumiwa, jambo ambalo si la haki,” aliandika.

Mvutano ulipozidi, Sancho aliondolewa katika shughuli za kikosi cha kwanza. Alikwenda kwa mkopo Borussia Dortmund Januari 2024, kabla ya kupata mikopo mingine Chelsea na Aston Villa.


MASTA 03

3. WAYNE ROONEY — 2010

Wayne Rooney aliwashangaza mashabiki wa United Oktoba 2010 alipohoji matarajio ya klabu hiyo na uwezo wake wa kusajili wachezaji bora duniani baada ya kuondoka kwa Cristiano Ronaldo na Carlos Tevez mwaka uliotangulia.

Rooney alifichua kuwa alikataa kusaini mkataba mpya kwa sababu hakupata uhakikisho alioutaka kutoka kwa aliyekuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, David Gill.

“Katika mazungumzo ya Agosti, niliomba uhakikisho kuhusu uwezo wa klabu kuendelea kuvutia wachezaji bora duniani,” alisema Rooney.

Amesisitiza kuwa maswali yake yalikuwa na msingi kwa sababu kwake, jambo muhimu lilikuwa kushinda mataji.

Hata hivyo, aliyekuwa kocha Sir Alex Ferguson aliingilia kati na Rooney akasaini mkataba mpya wa miaka mitano siku chache baadaye.


MASTA 04

4. ROY KEANE — 2005

Roy Keane aliandika ukurasa mwingine wa historia ya United Oktoba 2005 baada ya kuikosoa vikali timu hiyo kufuatia kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Middlesbrough.

Katika mahojiano yaliyofanyika kwa ajili ya kituo cha televisheni cha klabu hiyo, MUTV, Keane aliwakosoa wachezaji kadhaa, akiwamo Rio Ferdinand.

Kuhusu Ferdinand alisema: “Kwa sababu tu unalipwa pauni 120,000 kwa wiki na kucheza vizuri kwa dakika 20 dhidi ya Tottenham, unadhani wewe ni supastaa.”

Pia aliwakosoa Darren Fletcher, John O'Shea, Edwin van der Sar, Alan Smith na Kieran Richardson.

Keane alihitimisha kwa kusema kikosi kilikuwa kimeiangusha klabu, kocha na mashabiki.

Mahojiano hayo yaliondolewa kabla ya kurushwa hewani kwa ukamilifu. Wiki chache baadaye, Keane alikubali kujiunga na Celtic kabla ya kuondoka United wakati wa dirisha la usajili la Januari 2006.


MASTA 05

5. ZLATAN IBRAHIMOVIC — 2021

Zlatan Ibrahimovic aliikosoa baadaye namna United ilivyoendesha mambo yake, akieleza kuwa klabu hiyo ilikuwa na utamaduni uliotanguliza taratibu za kampuni kuliko mahitaji ya wachezaji.

Katika kitabu chake cha maisha, Ibrahimovic aliandika: “Nilipofika huko, nilikuta mtazamo mdogo na uliojifungia.”

Mswede huyo alikumbuka tukio la kutozwa pauni moja kwa juisi ya matunda aliyochukua kwenye friji ya hoteli wakati akiwa katika majukumu ya klabu.

Alipouliza kuhusu makato hayo, aliambiwa alipaswa kulipia kile alichoagiza.

Ameongeza: “Haya ndiyo mambo madogo yanayoleta tofauti na kuwafanya wachezaji waheshimiwe.”

Tofauti na wengine, ukosoaji wa Ibrahimovic ulitolewa baadaye kupitia kitabu chake, badala ya kuwa makabiliano ya moja kwa moja wakati akiwa mchezaji wa United.


MASTA 06

6. PAUL POGBA — 2018

Paul Pogba alihoji mbinu za United baada ya kutoka sare ya mabao 1-1 na Wolves katika Uwanja wa Old Trafford Septemba 2018, akitaka timu hiyo icheze kwa kushambulia zaidi chini ya kocha Jose Mourinho.

“Tuko nyumbani na tunapaswa kucheza vizuri zaidi dhidi ya Wolves. Tuko hapa kushambulia,” alisema Pogba.

“Naamini timu zinapoiona Manchester United ikishambulia mfululizo, zinaogopa. Hilo ndilo kosa letu.

“Pengine tunapaswa kuwa na mtazamo bora na kucheza vizuri zaidi kwa sababu tuko Old Trafford na tunapaswa kushambulia.”

Siku chache baadaye, Pogba na Mourinho walihusishwa na mabishano makali katika uwanja wa mazoezi, tukio lililonaswa kwa kamera na kusambaa kwenye televisheni na mitandao ya kijamii.

Mourinho alimvua Pogba nafasi ya unahodha msaidizi kabla ya kocha huyo kutimuliwa chini ya miezi mitatu baadaye. Pogba aliendelea kuitumikia United hadi 2022, aliporejea Juventus.


MASTA 07

7. ROMELU LUKAKU — 2019

Romelu Lukaku aliishutumu United kwa kushindwa kumlinda dhidi ya tetesi kuhusu mustakabali wake katika klabu hiyo wakati wa majira ya kiangazi ya 2019.

“Mambo mengi yalisemwa na sikuhisi kuwa nilikuwa nikilindwa,” alisema Lukaku.

“Niliona tetesi nyingi, ‘Rom anaenda kule’, ‘Hawamtaki Rom’, lakini hakuna aliyesimama hadharani na kuzikanusha.”

Ameongeza kuwa haikuwa vizuri kwake kubaki mahali ambapo alihisi hakutakiwa.

Lukaku pia alidai kuwa yeye na Paul Pogba walikuwa wakifanywa wa kulaumiwa mara kwa mara wakati timu ilipokuwa ikipitia kipindi kigumu.

Mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji aliondoka United na kujiunga na Inter Milan katika majira ya kiangazi ya mwaka huo.