Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United, Bruno kukaa mezani

Muktasari:

  • Kikao hicho kinakaliwa ikiwa ni baada ya sintofahamu na ripoti nyingi zilizodai staa huyu anataka kuondoka dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi.

MABOSI wa Manchester United wanatarajiwa kufanya kikao na nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes, 31, ili kumweleza bado wanamhitaji aendelee kusalia Old Trafford kwa angalau msimu mmoja zaidi.

Kikao hicho kinakaliwa ikiwa ni baada ya sintofahamu na ripoti nyingi zilizodai staa huyu anataka kuondoka dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi.

Katika kikao hicho, Man United inataka pia kumpa Bruno muda wa kujifikiria na kuwapa jibu kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu ikiwa atataka kubaki au ataondoka.

Uongozi wa Man United unaamini uzoefu, uongozi na mchango wa Bruno bado ni muhimu katika kipindi hiki cha mpito, hasa wakati huu klabu ikiendelea kujenga upya kikosi chake.

Kiungo huyo wa Ureno amekuwa mhimili wa timu kwa miaka kadhaa, akiongoza kwa mabao na asisti, lakini  mwishoni mwa mwaka jana alifunguka timu hiyo ilikuwa tayari kumwacha aende baada ya kupokea ofa nono kutoka kwa Al-Hilal ya Saudi Arabia jambo ambalo anadai lilimhuzunisha sana kwa sababu aliona timu haimhitaji.

Hata hivyo, kwa kuzingatia umri wake na masilahi yanayoendelea kujitokeza kutoka klabu nyingine Ulaya na nje ya bara hilo, Man United bado haitosita kumuuza ikiwa atahitaji kuondoka. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.


Ruben Loftus-Cheek

ASTON VILLA inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa AC Milan, Ruben Loftus-Cheek, 29, ikilenga kuimarisha safu yao ya kiungo baada ya pigo kubwa la kuumia kwa Boubacar Kamara, 26, aliyepata jeraha baya la goti litakalomuweka nje kwa muda mrefu. Loftus-Cheek, aliyewahi kupita Ligi Kuu England na Serie A, anaonekana ni chaguo linalofaa sana kwa Villa, lakini haijajulikana ikiwa Milan itakuwa tayari kumuuza. Pia yupo katika rada za Manchester United na mazungumzo ya awali yameshafanyika.


Crysencio  Summerville

TOTTENHAM Hotspur inataka kutoa takribani Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumsajili winga wa West, raia wa Uholanzi, Crysencio Summerville, 24, dirisha hili la usajili. Summerville amekuwa akionyesha kiwango kizuri katika kikosi cha West Ham licha ya timu hiyo kutofanya vizuri na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mech 18 za michuano yote na kutoa asisti nne. Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.


Micky van de Ven

LIVERPOOL imeonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa Tottenham, Micky van de Ven, 24, ambaye bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Spurs licha ya kupewa ofa. Mkataba wa sasa wa Van de Ven unatarajia kumalizika mwaka 2029 na mwenyewe ameonyesha nia ya kuondoka akivutiwa zaidi na ofa ambayo Liverpool imeweka mezani. Iwapo Tottenham hawataharakisha mazungumzo ya mkataba mpya, Liverpool inaweza kutumia fursa na kumpata bure.


Cuiabano

NOTTINGHAM FOREST imeamua kumruhusu beki wa kushoto,  Mbrazil, Cuiabano, 22, kuondoka kwa mkopo dirisha hili la Januari ili apate muda mwingi zaidi wa kucheza na kuendelea kukuza kiwango chake. Hatua hiyo imewafanya Forest kuanza kuangalia mbadala wake ili kuimarisha nafasi ya beki wa kushoto, huku Kostas Tsimikas, 29, wa Liverpool  ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo AS Roma  akiwa miongoni mwa majina yanayotajwa.


Ruben Neves

REAL MADRID wanatajwa kufikiria kumsajili kiungo wa Al-Hilal, Ruben Neves, 28, ambaye yuko tayari kuondoka Al-Hilal ikiwa ofa sahihi itawasilishwa. Neves, aliyewahi kuwa nahodha wa Wolves, hivi karibuni pia alitajwa huenda angetua Manchester United lakini dili hilo linaonekana kuwa gumu kwa sasa, sababu kubwa ikitajwa ni kiasi cha pesa ambacho Al-Hilal inakinitaji. Ushindani wa kuiwania saini ya Neves unatarajiwa kuwa mkali.


Bernardo Silva

BARCELONA imeweka mkakati wa kumsajili bure nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, 31, mkataba wake utakapomalizika mwisho wa msimu. Silva ni miongoni mwa wachezaji muhimu zaidi katika mafanikio ya Man City kwa miaka yote ambayo amekuwa katika viunga hivyo. Kutokana na changamoto za kifedha, Barcelona wanaona dili la uhamisho wa bure kuwa chaguo bora.


Edin Dzeko

Schalke 04 imeripotiwa kufikia makubaliano binafsi ya kumsajili mshambuliaji mkongwe wa Bosnia na Herzegovina,  Edin Dzeko, 39, dirisha hili, licha ya nyota huyo kujiunga na Fiorentina, Julai maka jana. Dzeko, ambaye amewahi kucheza ligi nyingi kubwa za Ulaya ikiwemo Bundesliga, Serie A na Ligi Kuu England, anaonekana kuwa chaguo la muda mfupi kwa Schalke ambayo inaandamwa na majeraha.