Man City, Man United… Utamu upo huku!
Muktasari:
- Miamba hiyo itakutana kwa mara 57 kwenye Ligi Kuu England na katika mechi 56 zilizopita, Man City imeshinda 20, wakati Man United imeshinda 26 na mara 10 mechi zao zilimalizika kwa sare.
LONDON, ENGLAND: MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu England unarudi wikiendi hii, lakini macho ya wengi yatakuwa huko Etihad, wakati Manchester City itakapokwaana na mahasimu wao Manchester United kwenye kipute cha Manchester derby uwanjani Etihad, Jumapili.
Miamba hiyo itakutana kwa mara 57 kwenye Ligi Kuu England na katika mechi 56 zilizopita, Man City imeshinda 20, wakati Man United imeshinda 26 na mara 10 mechi zao zilimalizika kwa sare.
Katika mechi za Man City ilizoshinda, imefanya hivyo mara 11 ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, wakati Man United kwenye mechi ilizoshinda, ugenini imefanya hivyo mara 14. Jambo hilo linafanya mechi hiyo itakayokutanisha makocha wawili wanaohitaji ushindi kwa nguvu zote, Pep Guardiola na Ruben Amorim kutarajia kuwa na ushindani mkali uwanjani.
Ukiweka kando kipute hicho cha Manchester derby, mechi nyingine ya Jumapili, itawakutanisha mabingwa watetezi Liverpool watakaokuwa ugenini kukipiga na Burnley. Rekodi zinaonyesha, Burnley na Liverpool zimekutana mara 18 kwenye Ligi Kuu England, huku wenyeji wa mechi hiyo wakiwa wameshinda mbili tu, sare mbili na jeshi la Arne Slot limeshinda mechi 14 na ilifanya hivyo mara nane ugenini kwenye Uwanja wa Burnley, Turf Moor.
Lakini, kasheshe la ligi hiyo litaanzia Jumamosi kwa mechi nane kwenye viwanja tofauti, huku Arsenal itakapokuwa nyumbani Emirates kukipiga na Nottingham Forest itakayokuwa chini ya kocha wa zamani wa mahasimu wao, Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou. Patachimbika.
Arsenal na Forest zimekutana mara 16 kwenye Ligi Kuu England, huku sare ni nne tu na Forest ikishinda mbili na mara 10 ushindi ulikwenda kwa The Gunners na mara sita ilifanya hivyo uwanjani Emirates.
Bournemouth itakuwa nyumbani kucheza na Brighton, wakati Crystal Palace itajimwaga huko Selhurst Park kucheza na Sunderland. Everton ya David Moyes itaonyesha ubabe na Aston Villa ya Unai Emery katika mechi inayotazamiwa kuwa na upinznai mkali, wakati Fulham itakuwa nyumbani kucheza na Leeds United.
Newcastle United itakuwa na shughuli pevu nyumbani bila ya huduma ya Yoane Wissa kucheza na Wolves, huku kukiwapo na kipute cha London derby, wakati West Ham United itakapokuwa nyumbani kucheza na Tottenham Hotspur ya kocha Thomas Frank.
Kasheshe jingine litakuwa huko Brentford, wakati itakapokuwa nyumbani kucheza na Chelsea, ambayo kocha Enzo Maresca alitangaza atakosa huduma ya straika wake Liam Delap kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya pesa itakayomweka nje ya uwanja kwa kipindi kisichopungua wiki 10.
Ligi Kuu England inarejea wikiendi hii baada ya kukosakana kwa wiki mbili kupisha michuano ya kimataifa.