Makipa kumi wa bei mbaya duniani
Muktasari:
- Miamba hiyo ya Old Trafford ilirudi tena kwenye mchakato wa kumnasa kipa wa Royal Antwerp, Senne Lammens, 23, anayedaiwa kuuzwa Pauni 17 milioni.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United iliingia kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi huko Ulaya jana Jumatatu, ikiwa bize kusaka kipa mpya.
Miamba hiyo ya Old Trafford ilirudi tena kwenye mchakato wa kumnasa kipa wa Royal Antwerp, Senne Lammens, 23, anayedaiwa kuuzwa Pauni 17 milioni.
Kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kilifanya mawasiliano pia na Aston Villa juu ya uwezekano wa kumsajili kipa Emiliano Martinez na kwa ripoti za asubuhi ya Jumatatu, Man United ilikuwa na mpango wa kumjumuisha winga Jadon Sancho kwenye dili hilo.
Martinez, 32, aliwekwa kando na kocha Unai Emery kwenye kikosi chake cha Aston Villa wakati wa kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Crystal Palace jambo lililochochea uwezekano wa uhamisho huo wa kwenda Old Trafford, huku timu yake ikimthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 40 milioni. Hata hivyo, bila ya kujali ni kipa gani kati ya hawa watakuwa wamenaswa, hii ni orodha ya makipa ghali kabisa Ulaya kwa sasa.
10. Giorgi Mamardashvili (Liverpool, 2024) - Pauni 29milioni
Liverpool ililipa Pauni 29 milioni kunasa huduma ya kipa Giorgi kwenda kuwa chaguo la pili kwenye kikosi hicho cha Anfield. Staa huyo wa kimataifa wa Georgia alinaswa kutokewa Valencia mwaka 2024 kwa ada ya awali ya Pauni 25 milioni na nyongeza ya Pauni 4 milioni.
9. David Raya (Arsenal, 2024) - Pauni 30milioni
Usajili wa kipa David Raya kutoka Brentford, ambaye awali alitua Emirates kwa mkopo mwka 2023 kabla ya kubebwa jumla kwa ada ya Pauni 30 milioni, ikilipwa Pauni 27 milioni za awali pamoja na nyongeza ya Pauni 3 milioni. Alitua kushindania namba na Aaron Ramsdale.
8. James Trafford (Man City, 2025) - Pauni 31milioni
Manchester City ilikubali kulipa Pauni 31 milioni kumrudisha kikosini kipa aliyewahi kuibukia kwenye akademia yao na jambo hilo linamfanya kuwa miongoni mwa makipa ghali Ulaya kwa sasa. Kipa huyo alinyakuliwa kutokea Burnley alikoonyesha kiwango bora kabisa.
7. Jasper Cillessen (Valencia, 2019) - Pauni 31.4milioni
Barcelona ilifanya dili tamu hapa baada ya kumsajili Jasper Cillessen kutoka Ajax kwa ada ya Pauni 12.8 milioni mwaka 2016, ilitumia kwenye mechi 32 ndani ya miaka mitatu, kabla ya kumuuza Valencia kwa ada ya Pauni 31.4 milioni mikaka mitatu baadaye.
6. Ederson (Man City, 2017) - Pauni 34.7milioni
Baada ya kuanza na makipa Joe Hart na Claudio Bravo kwenye klabu ya Manchester City, kocha Pep Guardiola alikwenda kunasa huduma ya ipa Ederson, ambaye alimnasa kutoka Benfica kwa ada ya Pauni 34.7 milioni. Ni mmoja wa makipa mahiri kabisa kuwahi kutokea Ulaya.
5. Thibaut Courtois (Real Madrid, 2018) - Pauni 35milioni
Baada ya kusubiri kwa muda kupata nafasi Chelsea baada ya kuonyesha kiwango bora Atletico Madrid, misimu minne ilitosha kwa Thibaut Courtois kuonyesha kiwango bora huko The Vlues na kuwafanya Real Madrid kulipa Pauni 35 milioni kumsajili mwaka 2018.
4. Andre Onana (Man United, 2023) - Pauni 47.2milioni
Manchester United ikiwa chini ya kocha Erik ten Hag iliamua kuachana na David de Gea na kwenda kunasa huduma ya kipa Andre Onana kwa ada ya Pauni 47.2 milioni akitokea Inter Milan. Kiwango cha Mcamerooni huyo kimezua maswali mengi kuona kama anafaa.
3. Lucas Chevalier (PSG, 2025) - Pauni 47.7milioni
PSG ilikuwa timu iliyo kwenye midomo ya kila shabiki wa soka baada ya kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wa 2024/25 na wachache walitarajia usajili mkubwa na badala yake wamemsajili kipa Lucas Chevalier kwa Pauni 47.7 milioni.
2. Alisson (Liverpool, 2018) - Pauni 67milioni
Linapotakiwa kutajwa kipa bora duniani, jina la Alisson linaweza kuwa miongoni mwao kutokana na kile anachokifanya uwanjani, akiisaidia Liverpool kwenye michuano mingi, ikiwamo kubeba Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alinaswa kwa Pauni 67 milioni.
1. Kepa Arrizabalaga (Chelsea, 2018) - Pauni 71.6milioni
Chelsea ilivunja rekodi ya dunia ya kumsajili kipa kwa pesa nyingi, wakati ilipolipa Pauni 71.6 milioni kumnyakua Mhispaniola Kepa Arrizabalaga. Kipa huyo alisajiliwa kuja kuchukua mikoba ya Courtois huko Stamford Bridge, kabla naye kuondoka na sasa yupo Arsenal.