Madogo janja 20 EPL walioanza mapema
Muktasari:
- Dogo Ethan Nwaneri alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya EPL mnamo Septemba 19 2022, akiwa na uri wa miaka 15 na siku 181, alipopewa nafasi uwanjani kama mchezaji wa akiba dakika za mwisho kwenye ushindi wa Arsenal wa mabao 3-0 dhidi ya Brentford ugenini.
LONDON, ENGLAND: KUNA kizazi cha wachezaji wadogo wengi waliowahi kupita katika Ligi Kuu England (EPL) tangu 1992. Lakini, ni kina nani waliocheza wakiwa na umri mdogo zaidi katika historia? Hawa hapa ni 20 walioanza mapema tu kukiwasha.
Ethan Nwaneri (miaka 15, siku 181)
Dogo Ethan Nwaneri alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya EPL mnamo Septemba 19 2022, akiwa na uri wa miaka 15 na siku 181, alipopewa nafasi uwanjani kama mchezaji wa akiba dakika za mwisho kwenye ushindi wa Arsenal wa mabao 3-0 dhidi ya Brentford ugenini.
Nwaneri alikuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri wa chini ya miaka 16 kucheza ligi hiyo, na pia mchezaji wa kwanza wa umri huo kuichezea Arsenal katika mashindano yoyote. Alivunja rekodi ya mashindano iliyokuwa imewekwa na Harvey Elliott tangu Mei 2019.
Nwaneri, ambaye ni mdogo kwa umri kuliko Uwanja wa Emirates wa Arsenal, alizaliwa 2007. Rekodi ya Arsenal ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza mechi ya ushindani ilikuwa inashikiliwa na Cesc Fabregas (miaka 16, siku 177), huku Nwaneri pia akimzidi Jack Wilshere (miaka 16, siku 256) kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza mechi ya ligi kwa Arsenal.
Kocha Mikel Arteta alimpa Nwaneri nafasi ya kujiunga na kikosi cha kwanza baada ya kufanya vizuri katika mechi za Arsenal chini ya miaka 18, na kuonekana kwake kulikuja wiki moja baada ya rekodi ya England kuvunjwa na dogo kutoka Ireland Kaskazini, Christopher Atherton aliyekuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza soka la wakubwa nchini kwake alipoichezea Glenavon akiwa na miaka 13 na siku 329.
Max Dowman (miaka 15, siku 235)
Max Dowman alikuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kucheza EPL katika ushindi wa Arsenal dhidi ya Leeds United, Agosti 23, 2025.
Baada ya kufanya vizuri katika maandalizi ya msimu, Dowman alipewa nafasi katika mechi ya pili ya Arsenal msimu wa 2025/26 licha ya kuwa na umri wa miaka 15 na siku 235 pekee. Aliingia dakika ya 64 wakati Arsenal ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 4-0, na baadaye akaifungia timu yake penalti katika muda wa nyongeza na kufanya matokeo kuwa 5-0. Katika siku ya mwisho ya msimu wa 2025/26, Dowman alichaguliwa kuanza katika kikosi cha Arsenal dhidi ya Crystal Palace, na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuanza EPL akiwa na miaka 16 na siku 144.
Jeremy Monga (miaka 15, siku 271)
Ulikuwa usiku wa kusikitisha kwa Leicester City Aprili 7, 2025. Ikiwa ilikuwa katika mfululizo wa kupoteza mechi saba za ligi ilikumbana na Newcastle United nyumbani na kujikuta ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 12, kabla ya kuwa nyuma kwa mabao 3-0 wakati wa mapumziko. Timu hiyo ya Ruud van Nistelrooy pia ilikuwa imefikisha zaidi ya saa 12 tangu ilipofunga bao lake la mwisho la ligi. Ilikuwa ikikabiliwa na hatari kubwa ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu England. Miongoni mwa mambo machache yaliyowapa mashabiki wa nyumbani furaha ilikuwa kumuona kinda wa akademi mwenye umri wa miaka 15, Jeremy Monga, akiingia uwanjani katika mazingira magumu kwa Leicester dakika ya 74 kwenye Uwanja wa King Power, akichukua nafasi ya Bilal El Khannouss.
Monga, ambaye ni winga, hakuweza kuleta mabadiliko makubwa Leicester ilipokumbana na kipigo kingine cha kuvunja moyo, lakini aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya mashindano hayo wakati huo. Angalau kulikuwa na jambo moja la kufurahia katika usiku huo.
Harvey Elliott (miaka 16, siku 30)
Harvey Elliott alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika ligi hiyo wakati huo alipocheza mechi yake ya kwanza mnamo Mei 4, 2019, akiingia dakika ya 88 kama mchezaji wa akiba katika kipigo cha Fulham cha mabao 1-0 dhidi ya Wolves kwenye Uwanja wa Molineux. Rekodi hiyo ilivunjwa Septemba 2022 na Ethan Nwaneri wa Arsenal. Kwa sasa akiwa mchezaji aliyekomaa katika EPL, Elliott alikuwa na umri wa miaka 16 na siku 30 siku alipocheza mechi yake ya kwanza, lakini kocha wa Fulham, Scott Parker, aliamua kumjumuisha kwenye kikosi cha siku ya mechi kwa timu ambayo tayari ilikuwa imeshuka daraja. Takribani miezi mitatu baada ya mechi hiyo, Elliott alisajiliwa na Liverpool kwa ada ambayo haikuwekwa wazi, na akacheza mechi yake ya kwanza ya ligi Anfield katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sheffield United Januari 2020, akiingia dakika ya 90 kama mchezaji wa akiba. Kwa kufanya hivyo, akawa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kuichezea Liverpool katika EPL(miaka 16, siku 273), nyuma ya Jack Robinson, aliyefanya hivyo Mei 2010. Alianza mechi yake ya kwanza katika wiki ya pili ya msimu wa 2021/22, wakati Liverpool ilipoibuka na ushindi dhidi ya Burnley.
Matthew Briggs (miaka 16, siku 68)
Alipoingia uwanjani katika kipigo cha Fulham cha mabao 3-1 dhidi ya Middlesbrough Mei 13, 2007, katika siku ya mwisho ya msimu wa 2006/07, Matthew Briggs alikuja kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza EPL akiwa na miaka 16 na siku 68. Rekodi hiyo baadaye ilivunjwa, lakini Briggs aliishikilia kwa miaka 12 hadi Elliott alipocheza Mei 2019.
Mchezaji huyo alilazimika kusubiri zaidi ya miaka mitatu kabla ya kupewa nafasi ya kuanza mechi ya kwanza ya EPL, na pia kucheza mechi yake nyingine ya kwanza katika mashindano hayo, katika kipigo cha Fulham cha bao 1-0 dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Briggs, ambaye alicheza beki wa kushoto, aliichezea Fulham mechi 13 katika ligi hiyo kwa misimu mitano, zote akiwa na klabu hiyo. Hata hivyo, muda wake mwingi Fulham aliutumia kwa mkopo katika klabu nyingine kabla ya baadaye kushuka madaraja ili kupata nafasi zaidi ya kucheza mara kwa mara.
HAWA HAPA WENGINE
Ukiachana na waliotajwa juu, hawa ni wengine walioanza kukipiga EPL wakiwa na umri wa miaka 16; Izzy Brown (West Brom miaka 16, siku 117), Aaron Lennon (Leeds United miaka 16, siku 129), Jose Baxter (Everton miaka 16, siku 191), Joel Drakes-Thomas (Crystal Palace miaka 16, siku 194), Rushian Hepburn-Murphy (Aston Villa miaka 16, siku 198), Gary McSheffrey (Coventry City miaka 16, siku 198) na Jake Evans (Leicester City miaka 16, siku 234).
Wengine ni Reece Oxford (West Ham United miaka 16, siku 236), Jerome Abbey (Wolves miaka 16, siku 250), Jack Robinson (Liverpool miaka 16, siku 250), Mahdi Nicoll-Jazuli (Chelsea miaka 16, siku 255), Jack Wilshere (Arsenal miaka 16, siku 256), Angel Gomes (Manchester United miaka 16, siku 263), Mark Platts (Sheffield Wednesday miaka 16, siku 263) na James Vaughan aliyekuwa Everton aliyeanza kukiwasha akiwa na umri wa miaka 16 na siku 270.