Mabosi Crystal Palace wamuweka ‘mtu kati’ Guehi
Muktasari:
- Liverpool ina mpango wa kutaka kumsajili staa huyo katika dirisha la majira ya baridi au kiangazi mwakani.
MWENYEKITI wa Crystal Palace, Steve Parish, amefanya mazungumzo ya ana kwa ana na beki wa kimataifa wa England Marc Guehi, 25, pamoja na familia yake baada ya kuzuia uhamisho wake wa kujiunga na Liverpool katika dirisha lililopita.
Liverpool ina mpango wa kutaka kumsajili staa huyo katika dirisha la majira ya baridi au kiangazi mwakani.
Bayern Munich, Real Madrid na Barcelona pia zinahitaji saini yake. Parish alifanya mazungumzo hayo ili kumshawishi asaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika kikosi hicho kwa sababu mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu. Bosi huyo hataki kuona Guehi anaondoka bure, hivyo anataka asaini mkataba mpya ili hata akiuzwa mwisho wa msimu auzwe kwa pesa nyingi kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine.
Guehi ambaye pia alishafanya hadi vipimo vya afya anadaiwa kuwa alikasirishwa dili lake la kujiunga Liverpool kufeli katika dakika za mwisho za dirisha la usajili.
Michael Olise
LIVERPOOL inamtazama winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Michael Olise, 23, kama mrithi wa muda mrefu wa Mohamed Salah, 33, ambaye licha ya kusaini mkataba mpya miezi kadhaa iliyopita, taarifa zinadai anaweza kuondoka mwakani kwani timu nyingi za Saudi Arabia zinahitaji huduma yake. Liverpool inaamini Olise atakuwa mbadala sahihi kwa sababu ana uzoefu wa kutosha katika ligi hiyo.
Harry Maguire
BEKI wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Harry Maguire, 32, anawindwa na klabu mbili za Saudi Arabia ambazo kwa sasa zipo katika mazungumzo na wawakilishi wake. Maguire ambaye amepoteza nafasi ya kudumu kikosi cha kwanza cha Man United chini ya Ruben Amorim ameonyesha nia ya kuwa tayari kuondoka kutokana na mkwanja wa kutosha ambao matajiri hao wamemuwekea mezani.
Conor Gallagher
MANCHESTER United ilijaribu kumsajili kiungo wa Atletico Madrid na England, Conor Gallagher, 25, dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, lakini ofa ilikataliwa na Atletico ambayo bado inahitaji huduma ya fundi huyu kutokana na kiwango chake katika timu. Inaelezwa Gallagher mwenyewe alitamani sana kurudi England katika dirisha lililopita lakini changamoto ilikuwa kwa Atletico yenyewe.
Altay Bayindir
MANCHESTER United ipo tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza mmoja kati ya makipa wawili, Altay Bayindir, 27 na Andre Onana ikiwa wataamua kuondoka katika kipindi hiki ambacho timu za Saudi Arabia na Uturuki zinaonyesha nia kubwa ya kutaka kuwasajili makipa hao, lakini anayeonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuondoka ni Onana ambaye nafasi yake katika kikosi cha kwanza inaonekana kupotea.
Jean-Philippe Mateta
KATIKA siku ya mwisho ya dirisha la usajili lililopita, Tottenham Hotspur iliulizia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa Jean-Philippe Mateta, 28, kutoka Crystal Palace. Mateta ambaye alifunga maba 16 katika Ligi Kuu England msimu uliopita, awali alitajwa kuwa katika rada za Manchester United lakini vigogo hao waliachana na mpango huo.
Dusan Vlahovic
JUVENTUS inafanya majadiliano na wawakilishi wa mshambuliaji wa kimataifa wa Serbia, Dusan Vlahovic , 25, ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika katika majira ya kiangazi 2026. Mabosi wa Juventus wanataka kufanya hivyo kwa sababu kuanzia Januari 2026 anaweza kukubaliana na timu za nje ya Italia na kusaini mkataba wa awali aondoke bure.
Jan Paul van Hecke
LIVERPOOOL, Tottenham Hotspur na Newcastle United zinamfuatilia kwa karibu beki wa Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi, Jan Paul van Hecke, 25, ili kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya baridi au kiangazi mwakani. Brighton imekuwa ikitoa wachezaji wenye kiwango cha juu katika miaka ya karibuni ikiwemo Moise Caicedo, Alexis Mac Allister na Marc Cucurella ambao wameonekana kuwa tegemeo kwenye timu ambazo wamesajiliwa.