Luke Littler ‘alipuka’ Usyk kumshinda Verhoeven kwa utata
Muktasari:
- Wadau wengi wa ngumi wamepinga uamuzi huo, na Verhoeven mwenyewe anapanga kukata rufaa. Bondia Anthony Joshua, aliyekuwepo ukumbini, alikiri kuwa pambano hilo lilikatishwa mapema mno.
Mchezaji nyota wa mchezo wa mishale (darts), Luke Littler, ametoa ya moyoni kuhusu ushindi wa Oleksandr Usyk dhidi ya Rico Verhoeven katika pambano lililounguruma nchini Misri Jumamosi, Mei 23, 2026. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 ameeleza kusikitishwa kwake na uamuzi ya mwisho ya pambano hilo zito la masumbwi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Littler ameandika ujumbe mfupi uneosema, "Ndondi zimeisha rasmi, mchezo umeharibika kabisa."Mtanange huo wa uzani wa juu uliingia kwenye vurugu baada ya mwamuzi Mark Lyson kusitisha pambano ikiwa imesalia sekunde moja kumalizika kwa raundi ya kumi na moja.
Usyk alikuwa amerejea kwa kasi kwenye mchezo na kumwangusha Verhoeven, ambaye ni mtaalamu wa kickboxing. Hata hivyo, baada ya Mholanzi huyo kusimama, mwamuzi aliingilia kati na kulimaliza pambano haraka bila kumpa nafasi ya kupumzika kuelekea raundi ya mwisho.
Wadau wengi wa ngumi wamepinga uamuzi huo, na Verhoeven mwenyewe anapanga kukata rufaa. Bondia Anthony Joshua, aliyekuwepo ukumbini, alikiri kuwa pambano hilo lilikatishwa mapema mno.
Verhoeven pia alieleza kusikitishwa kwake akisema, "Mwamuzi alijua raundi ilikuwa inaisha. Angeniacha nipambane hadi mwisho au asubiri kengele ilie." Mashabiki na watu maarufu mitandaoni walionyesha hasira zao baada ya matokeo hayo.
Bondia Jake Paul amekosoa akisema Rico alikuwa akishinda raundi zote na maamuzi hayo yalikuwa ya kichaa. Mchambuzi wa ngumi Mike Coppinger ameonyesha kuwa Verhoeven alikuwa mbele kwa alama, ingawa majaji walikuwa wameweka matokeo yakiwa sawa kabla ya raundi hiyo ya mwisho kukatizwa.