Oleksandr Usyk kuzichapa na nguli wa Kickboxing
Muktasari:
- Pambano hilo linapewa jina la "Glory in Giza" na litafanyika katika eneo la kihistoria la Mapiramidi ya Giza nchini Misri, likiwa ni moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo kushuhudiwa mwaka huu.
Mfalme asiyepingika wa uzani wa juu duniani, Oleksandr Usyk, atarejea ulingoni wikiendi hii Mei 23, 2026 kukabiliana na bingwa wa zamani wa dunia wa mchezo wa kickboxing, Rico Verhoeven, katika pambano la kihistoria linalosubiriwa kwa hamu kubwa.
Pambano hilo linapewa jina la "Glory in Giza" na litafanyika katika eneo la kihistoria la Mapiramidi ya Giza nchini Misri, likiwa ni moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo kushuhudiwa mwaka huu.
Usyk (39) ataingia ulingoni akiwa na rekodi ya kutoshindwa kabisa, akishinda mapambano yote 24 ya kulipwa. Katika pambano lake lililopita, mpambanaji huyo kutoka Ukraine alimchakaza Daniel Dubois kwa KO ya raundi ya tano na kuwa bingwa asiyepingika wa dunia kwa mara ya tatu.
Baada ya kuwachapa Tyson Fury na Anthony Joshua mara mbili kila mmoja, gazeti la SunSport limemweka Usyk katika nafasi ya kwanza kwenye orodha ya mabondia bora duniani.
Akizungumzia pambano hilo, Usyk amesema: "Nawaheshimu watu wanaofika kileleni mwa mchezo wao. Rico ni mmoja wao, ni mwanamichezo mwenye nguvu na bingwa mkubwa."
Kwa upande mwingine, bondia wa Uholanzi, Rico Verhoeven ni gwiji wa kickboxing ambapo ameshikilia taji la dunia la mashindano ya Glory kwa miaka 12, akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 28 na kupoteza moja.
Hata hivyo, Rico hajapigana pambano la ngumi za kawaida (boxing) tangu mwaka 2014, ambapo alishinda kwa KO kwenye pambano lake pekee la masumbwi. Kuelekea pambano hili, Rico anapewa nafasi ndogo sana ya kushinda dhidi ya fundi wa masumbwi Usyk.