Lookman afurahia changamoto kubwa
Muktasari:
- Nyota huyo wa Atalanta amekuwa kiungo muhimu zaidi wa mashambulizi ya Nigeria kwenye mashindano haya na mara nyingine tena akatambuliwa kama Mchezaji Bora wa Mechi.
MARRAKECH, MOROCCO: MSHAMBULIAJI wa Nigeria, Ademola Lookman, amesema imani ya timu yake inaongezeka kila siku katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huku Super Eagles wakijitayarisha kukutana na Algeria mabingwa wa mwaka 2019 Jumamosi hii Marrakech.
Nyota huyo wa Atalanta amekuwa kiungo muhimu zaidi wa mashambulizi ya Nigeria kwenye mashindano haya na mara nyingine tena akatambuliwa kama Mchezaji Bora wa Mechi.
Lookman tayari amefunga mabao matatu na kutoa pasi tano za mabao (assists) kwenye AFCON hii na kufikisha jumla ya mabao saba katika historia yake ya mashindano ya Afrika.
“Ni jambo zuri sana,” amesema Lookman. “Timu inaendelea kuwa bora katika kila mechi. Sasa hivi kila kitu ni mabao na hilo ni jambo chanya kwetu.”
Akicheza katika mfumo wa washambuliaji watatu wanaotembea kwa uhuru, Lookman ameshirikiana vyema na Akor Adams na Victor Osimhen na kuhakikisha Nigeria inakuwa tishio kila wakati katika eneo la hatari.
Ingawa alionekana akiingia katika mzozo na Osimhen katika mechi iliyopita, Lookman alieleza kuwa hakuna mvutano wowote ndani ya kikosi.
“Hakuna kilichotokea, ilikuwa ni tu mjadala uwanjani. Ndiyo yote. Katika soka mambo kama haya hutokea na unasonga mbele,” amesema.