Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utamu AFCON 2025 ndo unaanza sasa

AFCON Pict

Muktasari:

  • Ndio, Brahim Díaz amekuwa mchezaji muhimu kwa wenyeji Morocco baada ya kufunga mabao manne katika michezo minne aliyocheza na leo Ijumaa atakuwa na kazi ya kuiongoza timu hiyo kuitafuta tiketi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

RABAT, MOROCCO: FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zimepigwa mechi zaidi ya 40 katika siku 20 zilizopita tangu ilipoanza Desemba 21 mwaka jana, lakini unaambiwa kuanzia leo Ijumaa uhondo wa michuano hiyo ndo unaanza sasa.

Ndio, Brahim Díaz amekuwa mchezaji muhimu kwa wenyeji Morocco baada ya kufunga mabao manne katika michezo minne aliyocheza na leo Ijumaa atakuwa na kazi ya kuiongoza timu hiyo kuitafuta tiketi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.

Ndio, leo zinaanza mechi za robo fainali za michuano hiyo ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957 ikishirikisha mechi mbili na kesho Jumamosi zitapigwa nyingine mbili ili kusaka timu za kwenda nusu fainali ikiwa ni msako wa taji la AFCON 2025.

Mechi za leo zitahusisha majirani, Mali dhidi ya Senegal kuanzia saa 1:00 usiku kabla ya saa 4:00 usiku wenyeji Morocco kuvaana na Cameroon na kesho Jumamosi zitapigwa mechi nyingine mbili ya mapema saa 1 usiku itakuwa ni kati ya Algeria na Nigeria kabla ya Misri na watetezi Ivory Coast kuhitimisha ratiba saa 4:00 usiku.

Hapa chini ni dondoo fupi ya mechi hizo za robo fainali na namna ambvavyo rekodi zinazohusu timu hizo nane, huku saba zikiwa zimeshawahi kubeba taji la michuano hiyo kwa misimu tofauti ukiiondoa Mali inayosaka taji la kwanza mwaka huu, lakini ni pale itakapotoboa mbele ya mabingwa wa mwaka 2021.

AFCO 01

MALI v SENEGAL

Mechi hii ya kukata utepe kwa hatua ya robo fainali ya AFCON 2025 itapigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki (kwa Morocco ni saa 11 jioni) na ngoma itapigwa kwenye Uwanja wa Grand de Tanger maarufu kama Stade Ibn Batouta, uliopo mjini Tangier.

Huu ni mtanange wa Afrika Magharibi kati ya wapinzani wanaofahamiana vizuri. Senegal inaonekana kuwa na ubora wa nyota wengi, lakini Mali imejijengea sifa ya kuwa timu yenye wapiganaji wanaoweza kupindua matarajio. Kocha wa Mali, Tom Saintfiet, amejijengea jina kwa uwezo wake wa kuzinoa timu ndogo na kuzifanya zishindane na wakubwa. Kiufundi, Mali itakuwa imejiandaa vyema; kitakachoamua ni utekelezaji uwanjani.

Senegal ina ubora katika maeneo yote ya uwanja na imeendelea kuimarika kadri mashindano yanavyoendelea. Katika historia ya mechi za kimataifa, Senegal imecheza dhidi ya Mali mara 40, ikiongoza rekodi ya ushindi wa mechi 19 dhidi ya 8 za Mali, huku mechi 13 zikimalizika kwa sare.

Senegal haijapoteza dhidi ya Mali tangu 1997, mfululizo wa mechi 13, ikishinda nne na sare tisa. Kukutana kwao pekee AFCON kulikuwa mwaka 2004 walipotoa sare ya 1-1 katika hatua ya makundi.

Mali imefika robo fainali katika fainali hizi za 2025 baada ya sare nne na ina rekodi nzuri katika hatua hii, ikishinda mechi sita kati ya saba za robo fainali ilizowahi kucheza. Kipigo chao pekee kilitokea miaka miwili iliyopita walipopoteza kwa wenyeji Ivory Coast baada ya muda wa nyongeza.

Senegal haijapoteza mechi 15 mfululizo katika historia ya AFCON (bila kuhesabu mikwaju ya penalti), mfululizo mrefu zaidi kuwahi kuwa nao. Kipigo chao cha mwisho kilikuwa fainali ya 2019 dhidi ya Algeria.

Mali ni timu pekee iliyobaki michuanoni kwa sasa bila ushindi, baada ya kutoa sare katika michezo yake yote minne iliyoicheza hadi kufika robo fainali. Hata hivyo, huenda wakahitaji kurudia mbinu hiyo tena mjini Tangier, ambako watakutana na Senegal ambayo haijapoteza mchezo wowote katika mechi 26 za mashindano rasmi.

Simba wa Teranga hawajapoteza katika michezo 15 ya AFCON na watakuwa mabingwa wa karatasi katika pambano hili. Hata hivyo, kiwango chao katika mchezo wa 16 Bora dhidi ya Sudan hakikuwa cha kuridhisha kabisa.

Waliruhusu bao la mapema na hawakudhibiti mchezo kikamilifu hadi waliposawazisha. Hata baada ya hapo, waliendelea kutoa nafasi chache za hatari kwa wapinzani wao. Ubora wao mkubwa, ndani ya kikosi cha kwanza na kutoka benchi, uliwawezesha kushinda mwishoni, lakini safu imara zaidi ya ulinzi ingeweza kuwapa changamoto kubwa zaidi.

Timu ya Tom Saintfelt itaamini ina uwezo wa kufanya hivyo baada ya ushindi wao wa jasho dhidi ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora. Mali walibaki na wachezaji 10 ndani ya dakika 30 za mwanzo, lakini waliruhusu nafasi chache sana katika dakika 90 zilizofuata na muda wa nyongeza. Zaidi ya hapo, waliweza kusawazisha bao katika dakika za mwisho baada ya kufungwa bao lililoonekana kuwa la ushindi kwa Tunisia, kabla ya kukamilisha comeback hiyo kwa ushindi wa mikwaju ya penalti.

AFCO 03

CAMEROON v MOROCCO

Pambano hili la kukata na shoka litapigwa pia leo Ijumaa kuanzia saa 4:00 usiku katika jiji la Rabat, kwa wenyeji Morocco kuvaana na Cameroon kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, jijini Rabat

Shinikizo kubwa litakuwa kwa wenyeji Morocco kadri mashindano yanavyoingia katika hatua nyeti. Hadi sasa, Morocco haijaonyesha kiwango chake bora kabisa, ikitegemea zaidi uwezo wa kufumania nyavu wa Brahim Diaz na Ayoub El Kaabi, ambao ndio wachezaji pekee waliowafungia mabao katika michezo minne ya awali.

Cameroon imekuwa kimya lakini madhubuti, ikiwa na kundi zuri la wachezaji vijana waliowasukuma kufika hatua hii. Kwa muda mrefu Morocco imekuwa ikipewa nafasi kubwa AFCON, lakini mara nyingi hushindwa kutimiza matarajio, licha ya kuwa na vikosi bora.

Ubingwa wao wa mwisho ulikuwa miaka 50 iliyopita. Hata hivyo, hivi karibuni wamekuwa wagumu kushindwa nyumbani na wana wachezaji wengi wenye uzoefu wa soka la Ulaya.

Timu hizi zimekutana mara 13 tu katika historia, Cameroon ikiongoza kwa ushindi sita dhidi ya mbili za Morocco, huku sare zikiwa tano.

Zimekutana mara tatu AFCON, mara ya mwisho mwaka 1992, Cameroon ikishinda mechi mbili na kutoa sare moja. Cameroon ina wastani mdogo zaidi wa umiliki wa mpira katika mashindano haya (asilimia 43.2) kati ya timu zote za robo fainali.

Inashangaza kwamba, ukizingatia historia yao, hii ni robo fainali ya tano tu kwa Morocco katika michuano ya bara. Kati ya robo fainali nne zilizopita, walivuka hatua hiyo mara moja tu, mwaka 2004, walipomaliza kama washindi wa pili.

Simba Wasioshindika wa Cameroon walikuwa wakijiandaa kwa mashindano yasiyoridhisha kutokana na vurugu na migogoro ya nje ya uwanja kabla ya mashindano kuanza.

Hata hivyo, wamefanikiwa kuyageuza mashindano haya kuwa mafanikio. Kocha mpya David Pagou ameiongoza timu yenye wastani mdogo zaidi wa umri katika mashindano haya, huku wachezaji kama kiungo wa Brighton, Carlos Baleba, na mshambuliaji kijana Christian Kofane wakicheza nafasi muhimu.

Kwa kiasi fulani kutokana na ujana wao, Cameroon imekuwa miongoni mwa timu zenye burudani zaidi kuangaliwa AFCON 2025. Michezo yao imekuwa wazi, ya kasi na ya kushambuliana pande zote, hali inayowawezesha kuwa hatari mbele ya lango, lakini pia kuwaacha wazi nyuma.

Morocco itajaribu kutumia udhaifu huo kwa kuwaweka washambuliaji wao katika nafasi sahihi. Brahim Díaz amekuwa nyota wa mashindano, akifunga mabao katika michezo yote minne aliyocheza kwenye AFCON yake ya kwanza.

Kurejea kwa Achraf Hakimi kunaimarisha zaidi upande wa kulia wa Atlas Lions katika hatua za mtoano, jambo litakalompa kazi ngumu nahodha wa Cameroon, Nouhou Tolo, upande wa kushoto wa safu ya ulinzi ya watu watatu.

Mchango wa mashabiki katika Uwanja wa Prince Moulay Abdallah utaendelea kuwa kipengele cha kuangaliwa. Morocco ilionekana kushtushwa na presha ya nyumbani walipoanza vibaya dhidi ya Tanzania katika mchezo wao wa mwisho, lakini waliweza kujipanga, kudhibiti mchezo na kulinda ushindi wao kwa ustadi baada ya kupata bao. Hata hivyo, mpinzani mwenye nguvu kama Cameroon anaweza kunufaika endapo hali ya wasiwasi itajitokeza tena.

AFCO 02

MZIKI WA KESHO ALGERIA v NIGERIA

Hii ngoma itapigwa mapema saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Marrakech, huku timu zote zikiwa ndizo pekee zilizoshinda mechi zao za msimu huu kwa asilimia zote kuanzia makundi hadi 16 Bora.

Hata hivyo, Nigeria imeonekana kuwa timu bora zaidi katika mashindano hadi sasa, licha ya migogoro midogo ya ndani ya uwanja. Imefika robo fainali kwa kishindo, ikifunga jumla ya mabao 12 na inaonekana bora zaidi kuliko kikosi kilichoshindwa hata kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Algeria haijang’ara sana, lakini imeshinda mechi zote nne ilizocheza, ikiruhusu bao moja tu. Huu ni mtanange unaovutia kwa kulinganisha mitindo tofauti ya uchezaji. Timu hizi zimekutana mara 23, Algeria ikiongoza kwa ushindi wa mechi 10 dhidi ya nane za Nigeria, huku sare zikiwa tano. Ushindi wa mwisho wa Nigeria ulikuwa mwaka 2016 katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.

Mechi hii ni kama marudiano ya nusu fainali ya AFCON 2019, ambayo Algeria ilishinda 2-1 kwa bao la kujifunga la William Troost-Ekong na bao la dakika ya 95 la Riyad Mahrez.

Tangu kutwaa taji la AFCON kwa mara ya kwanza mwaka 1990, Algeria imefika robo fainali mara sita na kuvuka mara mbili tu, ikimaliza nafasi ya nne mwaka 2010 na kunyanyua taji tena mwaka 2019. Kabla ya hapo, ilitolewa katika makundi katika matoleo mawili mfululizo bila kushinda mechi yoyote.

Nigeria ni mabingwa wa robo fainali. Tangu hatua hiyo ilipoanzishwa mwaka 1992, imecheza robo fainali 11 na kushinda 10. Kipigo chao pekee kilikuwa dhidi ya wenyeji Ghana mwaka 2008 kwa mabao 2-1. Ademola Lookman ni mchezaji hatari zaidi wa Nigeria, akiwa na mchango wa mabao saba (mabao matatu na pasi nne za mabao) katika michezo minne ya mashindano haya.

Nigeria imeendelea kujiimarisha kama timu bora zaidi ya AFCON 2025 hadi sasa baada ya ushindi mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya Msumbiji katika hatua ya 16 Bora.

Dosari pekee ilikuwa mabishano ya uwanjani kati ya nyota wao Victor Osimhen na Ademola Lookman, lakini hilo linaonekana kuwa tukio la muda mfupi katika joto la pambano.

Washambuliaji hao, pamoja na safu nzima ya ushambuliaji, wamekuwa katika kiwango bora, huku Super Eagles wakiongoza kwa mabao 12 kwenye mashindano. Lookman peke yake amehusika katika zaidi ya nusu ya mabao hayo, akijiweka kwenye mbio kali za kuwania mchezaji bora wa mashindano.

Timu ya Éric Chelle imeonekana kuwa na uwiano mzuri, huku Alex Iwobi akiwa mhimili muhimu kutokana na pasi zake kutoka kiungoni. Hata hivyo, sasa wanakabiliwa na mtihani mgumu zaidi dhidi ya timu nyingine pekee ambayo pia imeshinda mechi zake zote.

Nguvu ya Algeria iko kwenye ulinzi. Ni timu pekee, pamoja na wenyeji, iliyoruhusu bao moja tu. Pia wana idadi ndogo zaidi ya mabao tarajiwa (xG) waliyokubali, licha ya kucheza takribani dakika 500 ikiwa ni pamoja na muda wa nyongeza dhidi ya DR Congo.

Safu ya ushambuliaji ya Algeria imepata ugumu dhidi ya timu zenye ulinzi mgumu, lakini kina cha kikosi chao kinaweza kuleta tofauti. Mchezaji aliyeingia akiba, Adil Boulbina, alifunga bao la ushindi la kuvutia katika mchezo uliopita, huku Anis Hadj Moussa naye akionyesha dalili njema baada ya kumrithi Riyad Mahrez.

Kiungo muhimu Ismaël Bennacer alipata majeraha katika mchezo huo, jambo linaloweza kuwa wasiwasi mkubwa kwa kocha Vladimir Petkovic kuelekea robo fainali. Kwa vyovyote vile, pambano kali linatarajiwa mjini Marrakesh.

AFCO 04

MISRI v IVORY COAST

Hili ndilo pambano la kufungia hesabu za robo fainali litakalopigwa kuanza saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Adrar, mjini Agadir, watetezi Ivory Coast kuonyeshana kazi na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Misri iliyotwaa mara saba tangu 1957.

Misri, inakutana na Ivory Coast iliyojaa kasi na ufundi. Misri imecheza kwa nidhamu na juhudi kubwa hadi sasa, lakini bado inaonekana kuwa na hatua kadhaa za ziada za kuongeza kiwango. Ivory Coast, watetezi na walionyesha kiwango bora katika ushindi wao wa hatua ya 16 Bora dhidi ya Burkina Faso.

Misri imeshinda robo fainali tano mfululizo na sita kati ya 10 ilizocheza katika hatua hii. Tayari imeruhusu mabao 99 katika historia ya fainali za AFCON na inaweza kufikisha mabao 100 endapo itaruhusu bao katika mchezo huu. Ivory Coast imekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka katika robo fainali, ikicheza mara 11 na kushinda saba.

Huu ni marudiano ya fainali ya AFCON 2006, ambapo Misri ilishinda kwa penalti baada ya sare ya bila kufungana. Misri inatafuta kuongeza rekodi yake ya mataji hadi nane, baada ya kushindwa kunyanyua taji tangu iliposhinda mara tatu mfululizo mwaka 2010. Baadaye, ilishindwa kufuzu matoleo matatu mfululizo, na tangu hapo imepoteza fainali za 2017 na 2021.

Kwa karatasi, huu unaweza kuwa mchezo mkubwa zaidi wa robo fainali, ukiwakutanisha mabingwa wa kihistoria, Misri, dhidi ya mabingwa watetezi Ivory Coast.


Ni haki kusema wenyeji wa fainali zilizopita Ivory Coast wameonyesha kiwango cha kuridhisha zaidi hadi sasa. Kikosi cha Emerse Faé kinapata motisha kubwa kutoka ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burkina Faso, mchezo ambao Amad Diallo aling’ara kwa kufunga bao moja na kutoa pasi ya bao. Yan Diomande naye aliendelea kung’ara upande wa pili wa winga, hali itakayowalazimu Misri kuwa na mpango madhubuti wa kuwadhibiti wachezaji hao wawili.

Misri mara nyingi hutumia mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza katika michezo mikubwa kama hii, hivyo watategemea ubora wa Mohamed Salah na Omar Marmoush kuleta tofauti.

Hata hivyo, wamekuwa na ugumu wa kudhibiti na kutawala michezo, jambo lililoonekana wazi katika ushindi wao wa tabu dhidi ya Benin kwenye hatua ya 16 Bora uliowalazimu kucheza hadi muda wa nyongeza.

Ivory Coast inatarajiwa kupewa umiliki mkubwa wa mpira, hivyo safu ya kiungo inaweza kuwa ufunguo wa kuamua hatima ya mchezo.

Kijana Christ Inao Oulai aliendelea kuaminiwa katika kikosi cha kwanza kutokana na uwezo wake mzuri wa kusogeza mpira mbele, akitoa uwiano mzuri kati ya tishio la Franck Kessié katika eneo la mwisho na uimara wa ulinzi wa Ibrahim Sangaré. Endapo watakuwa katika siku yao, Misri inaweza kupata wakati mgumu sana.