Liverpool sasa kumsubiri Mark Guehi mwakani, Chelsea, Man U zaingilia dili
Muktasari:
- Liverpool iliripotiwa kuweka mezani ofa ya Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumpata Guehi ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Liverpool imepanga kumsajili beki kisiki wa Crystal Palace, Marc Guehi kwa usajili huru ifikapo mwisho wa msimu huu baada ya harakati zao za kutaka kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi kufeli katika siku ya mwiso ya usajili.
Liverpool iliripotiwa kuweka mezani ofa ya Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumpata Guehi ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Palace iligoma kumuuza Guehi kwa ofa hiyo ikisisitiza inahitaji walau Pauni 30 milioni kiasi ambacho Liverpool haikuwa tayari kukutoa.
Baada ya kufeli kwa dili la Guehi, Liverpool ilikataa kumruhusu Joe Gomes mwenye umri wa miaka 28 kujiunga na AC Milan dakika za mwisho.
Kanda ya video ya kuaga kwa Guehi katika kikos cha Palace ilivuja kwenye mitandao ya kijamii, ikionyesha kila kitu kilikuwa sawa kabla ya mambo kuharibika mwishoni.
Hata hivyo, licha ya mpango wa Liverpool kutaka kumchukua bure mwisho wa msimu, Januari mwakani huenda Chelsea na Manchester United zikatuma ofa kwenda Palace kwani hizo pia zinahitaji saini yake.
Liverpool inamtaka fundi huyu ikiamini atakuwa mbadala sahihi wa Virgil van Dijk ambaye umri ushakuwa unamtupa mkono.
Emiliano Martinez
MABOSI wa Aston Villa wamesisitiza hawakupokea ofa yoyote kutoka Manchester United kwa ajili ya kipa wao wa kimataifa wa Argentina, Emiliano Martínez, 32, licha ya kuhusishwa sana na uhamisho wa kwenda Manchester United dirisha lililomalizika. Kwa mujibu wa Sky Sports, Man United ilibadilisha mawazo kwa sababu ya umri wake na mshahara mkubwa wa takribani Pauni 200,000 kwa wiki (zaidi ya TSh 640 milioni) aliokuwa akiuhitaji.
Ademola Lookman
Bayern Munich ilikuwa na nia ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Ademola Lookman, 27, kwa mkopo kutoka Atalanta siku ya mwisho ya dirisha lililopita la usajili, baada ya kuona uwezenano wa kumpata Nicolous Jackson ambaye Chelsea ilibadilisha mawazo haya kumtoa kwa mkopo kabla ya kukubali kumwachia. Lookman alifunga mabao 17 katika mashindano yote msimu wa 2023/24 na aling’ara fainali za AFCON 2023.
Raheem Sterling
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England, Raheem Sterling, 30, ataendelea kubaki Stamford Bridge, baada ya kushindwa kupata timu iliyokuwa tayari kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Licha ya ropoti kudai baadhi ya timu kutoka Uturuki, Saudi Arabia na Marekani zinataka huduma yake, Sterling bado anataka kuendelea kusalia England na ikishindikana basi aende Hispania, Italia, Ujerumani au Ufaransa.
Manor Solomon
CRYSTAL Palace ilijiondoa katika dili la kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Israeli, Manor Solomon, 26, kutoka Tottenham Hotspur, katika dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kushindwa kufikia mwafaka na Spurs ya ulipaji wa mshahara wake. Spurs ilikuwa inataka Palace ilipe mshahara wote wa staa huyo pia itoe ada ya uhamisho wa mkopo jambo ambalo Palace haikuwa imelikubali.
Harry Wilson
UHAMISHO wa kiungo wa kimataifa wa Wales, Harry Wilson 28, kwenda Leeds ulishindikana baada ya Fulham kubadili msimamo wao dakika za mwisho kabla dirisha la usajili halijafungwa usiku wa Jumatatu. Kuvunjika kwa dili hilo kulisababisha pia kuanguka kwa mpango wa Fulham kumsajili chipukizi wa Chelsea Tyrique George, 19 na sasa itasubiri hadi dirisha la Januari.
Will Osula
MSHAMBULIAJI wa Newcastle United, Will Osula, 22, atasalia Newcastle United, licha ya kuhitajika na Eintracht Frankfurt kwa mkopo wa msimu mzima. Newcastle ndio imegoma kumuuza fundi huyu sababu kubwa ni kutohitaji kuendelea kuharibu timu zaidi kwani licha ya kwamba Osula sio mchezaji wao tegemeo.
Alexander Isak
VYANZO vya ndani Newcastle vinadai mabosi wa Newcsstle United walilazimika kumuuza mshambuliaji, Alexander Isak , 25, kwa sababu alionekana hana tena uchungu na timu na hakuonekana kucheza kwa kujituma tangu Aprili mwaka huu na ni kana hakutaka timu ifuzu Ligi ya Mabingwa. Isak aliyejiunga na Liverpool kwa Pauni 130 milioni ndiye mchezaji ghali zaidi kuwahi kusajiliwa England.