Ligi ya mabingwa Ulaya: Arsenal, PSG wanajambo lao
Muktasari:
- Nguvu kubwa ya kifedha ya Ligi Kuu England imeifanya timu zake kuwa miongoni mwa zinazotarajiwa kufanya vizuri, huku Arsenal ikiwa moja ya zinazotajwa zaidi.
PARIS, UFARANSA: Ligi ya Mabingwa Ulaya inarejea leo na kesho kwa kuanza kwa hatua ya ligi, wakati Arsenal ikiwa na ndoto ya kutwaa taji lake la kwanza huku Paris Saint-Germain (PSG) ikiwinda kutengeneza historia ya kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo.
Nguvu kubwa ya kifedha ya Ligi Kuu England imeifanya timu zake kuwa miongoni mwa zinazotarajiwa kufanya vizuri, huku Arsenal ikiwa moja ya zinazotajwa zaidi.
Katika misimu mitatu iliyopita, Arsenal imeishia robo fainali, nusu fainali na hatimaye fainali msimu uliopita.
Hivyo, hatua inayofuata kwa kikosi cha Mikel Arteta ni wazi sasa matamanio ni kutwaa taji.
Arsenal ilimaliza kileleni mwa hatua ya ligi msimu uliopita ikiwa na rekodi nzuri, lakini safari yake ya msimu huu inaanza kwa mtihani mgumu dhidi ya Napoli ugenini kesho Jumatano.
England ina jumla ya timu tano katika mashindano hayo, huku Manchester City na Liverpool zikiongozana na Manchester United na Aston Villa ambazo zimerudi kwenye jukwaa hilo.
Upande wa pili PSG ilifanikiwa kutetea ubingwa wake msimu uliopita baada ya kuifunga Arsenal kwa penalti mjini Budapest, Hungary, na kubaki na kombe ililolitwaa kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo mwaka mmoja uliotangulia.
Chini ya kocha Luis Enrique, PSG tayari imejiweka kwenye orodha ya timu kubwa zaidi kuwahi kushiriki mashindano hayo baada ya kutwaa mataji mawili mfululizo.
Kabla yao, ni Real Madrid pekee iliyowahi kufanya hivyo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa kisasa wa Ligi ya Mabingwa mwaka 1992.
Hata hivyo, kutwaa mataji matatu mfululizo ni jambo la kiwango kingine kabisa.
Real Madrid ilifanya hivyo chini ya Zinedine Zidane kati ya 2016 na 2018. Timu nyingine zilizowahi kufanikisha hilo ni Ajax iliyotwaa mataji kati ya 1971 na 1973, pamoja na Bayern Munich iliyofanya hivyo mwaka 1974 hadi 1976.
Madrid pia ilitengeneza rekodi ya kihistoria kwa kutwaa matoleo matano ya kwanza ya Kombe la Mabingwa Ulaya, kuanzia 1956 hadi 1960.
“Malengo yetu yako wazi. Nataka kushinda mataji makubwa na hakuna taji kubwa zaidi ya Ligi ya Mabingwa,” alisema Luis Enrique, ambaye pia aliiongoza Barcelona kutwaa ubingwa huo mwaka 2015.
PSG NA FORMAT MPYA
Mafanikio ya PSG ya kutwaa mataji mawili mfululizo yamekuja sambamba na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa.
Kwa sasa, timu 36 hushiriki hatua ya ligi, ambapo kila moja hucheza mechi nane dhidi ya wapinzani nane tofauti.
Pamoja na mafanikio yao, PSG haikufanya vizuri katika hatua hiyo ya ligi katika misimu miwili iliyopita, ikimaliza nje ya nafasi nane bora na kulazimika kucheza mechi za mchujo ili kufuzu hatua ya 16 bora.
Ratiba ngumu ilichangia hali hiyo, na msimu huu mabingwa hao wa Ufaransa watakutana tena na wapinzani wakubwa, akiwamo Manchester City, Barcelona na Aston Villa.
Kadiri miaka inavyokwenda, inaonekana kuwa vigumu zaidi kwa timu nje ya vigogo wa soka la Ulaya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.
Bayern Munich ni miongoni mwa vigogo wanaotazamwa, huku Jose Mourinho akirejea Real Madrid akiwa na jukumu la kuirudisha klabu hiyo kwenye utukufu wa Ulaya.
Barcelona nayo ina hamu kubwa ya kurejesha mikononi mwake taji hilo.
Kwa mtazamo wa sasa, ni vigumu kutazama nje ya vigogo hao, ingawa Inter Milan inaweza kuwa na sauti yake katika mbio hizo, huku Atletico Madrid ikiwa na kiu kubwa ya kufika fainali ambayo itachezwa katika uwanja wake.
WAGENI WAKULETA LADHA MPYA
Timu pekee nje ya Hispania, England, Ujerumani, Italia na Ufaransa iliyowahi kutwaa taji hilo katika miaka 30 iliyopita ni Porto ya Jose Mourinho mwaka 2004.
Msimu huu, majina mapya yanaingia kwenye mashindano hayo na kuongeza mvuto, akiwamo Como iliyomaliza nafasi ya nne Serie A msimu uliopita chini ya kocha Cesc Fabregas na kufuzu huku AC Milan na Juventus zikikosa nafasi.
Viking Stavanger nayo itashiriki kwa mara ya kwanza baada ya kutwaa ubingwa wa Norway kwa mara ya kwanza katika miaka 34.
Sabah ya Azerbaijan itaanza kampeni yake kwa safari ya kwenda Old Trafford kukabiliana na Manchester United, baada ya kutwaa ubingwa wa kwanza wa Azerbaijan na kupita hatua nne za mchujo.
Kocha wao, Valdas Dambrauskas aliingia kwenye ulimwengu wa ukocha akitumia fedha alizopata baada ya kushiriki toleo la Lithuania la kipindi cha televisheni cha Who Wants to be a Millionaire.
“Tangu nilipokuwa na miaka 12, nilipotambua kwamba sitakuwa mchezaji wa kulipwa, nilijua nataka kuwa kocha wa soka,” alisema katika mahojiano na Flashscore.
“Sijui nini kingetokea bila mchezo huo, lakini naamini ningepata njia nyingine ya kutimiza ndoto yangu.”
Sabah huenda ikashindwa kufuzu hatua inayofuata, ingawa Qarabag ya Azerbaijan ilifanya hivyo msimu uliopita.
Hata hivyo, kushiriki tu hatua ya ligi kunaweza kuiingizia klabu hiyo karibu euro20 milioni (zaidi ya Sh 60bilioni) kwa kiwango cha chini, fedha kubwa kwa timu zinazotoka kwenye ligi ndogo.
Mshindi wa Ligi ya Mabingwa hupata karibu euro90 milioni yza zawadi, kabla ya kuongezewa mamilioni mengine kupitia vyanzo kama haki za televisheni.
Inaripotiwa kuwa PSG ilipata takribani euro150 milioni kwa mataji yake mawili iliyotwaa.
RATIBA KESHO, JUMANNE
AEK Athensv LASK (Saa 19:45 Usiku)
Club Bruggev Aston Villa (Saa 19:45 Usiku)
Real Madrid vInter Milan (Saa 22:00 usiku)
Dortmund v Villarreal (Saa 22:00 usiku)
FC Porto v Manchester City(Saa 22:00 usiku)
Lille v Real Betis (Saa 22:00 usiku)
KESHOKUTWA, JUMATANO
Napoli v Arsenal(Saa 22:00 usiku)
Liverpool v Atletico Madrid(Saa 22:00 usiku)
PSG v Slovan Bratislava(Saa 22:00 usiku)
Sporting CP v Galatasaray(Saa 22:00 usiku)
Barcelona v Feyenoord (Saa 19:45 Usiku)
VfB Stuttgart v Viking(Saa 19:45 Usiku)