Mtanzania aanza na bao Arsenal
Muktasari:
- Baum, mwenye umri wa miaka 19, alifunga bao hilo dakika ya 10 baada ya kupenya vizuri safu ya ulinzi ya Brighton kabla ya kupiga shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kutikisa nyavu za wapinzani.
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI mpya wa Arsenal ya Wanawake, Lisa Baum mwenye asili ya Tanzania, ameanza vizuri maisha yake klabuni hapo baada ya leo Jumapili Septemba 6, 2026 kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake England (WSL) dhidi ya Brighton, uliochezwa Broadfield.
Baum, mwenye umri wa miaka 19, alifunga bao hilo dakika ya 10 baada ya kupenya vizuri safu ya ulinzi ya Brighton kabla ya kupiga shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kutikisa nyavu za wapinzani.
Mchezaji huyo amejiunga na Arsenal akitokea RB Leipzig katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi ambapo ameanza mchezo huo sambamba na wachezaji wengine wapya, kipa Misa Rodriguez, beki Ona Battle na kiungo Georgia Stanway.
Arsenal ilipata nafasi ya kuongeza bao muda mfupi baada ya Baum kufunga, lakini Alessia Russo alikosa nafasi hiyo baada ya kupiga mpira juu huku lango likiwa wazi.
Brighton nayo ilitengeneza nafasi kadhaa za kusawazisha. Kiko Seike alilazimika kuona shuti lake likiokolewa na Rodriguez, wakati Fran Kirby akipiga mpira wa juu kutoka umbali wa karibu na lango. Charlie Rule naye alishindwa kulenga kona ya juu baada ya kujaribu kutoka nje ya boksi.
Arsenal ilikaribia kufunga bao la pili kupitia Stina Blackstenius, lakini kipa wa Brighton, Chiamaka Nnadozie, alifanya kazi nzuri kwa kuuzuia mpira uliokuwa ukielekea kona ya chini na kuutoa nje.
Ushindi huo unaifanya Brighton kupoteza mchezo wake wa kwanza wa msimu kwa mara ya pili pekee katika misimu nane iliyopita ya WSL.
Baum aliyeichezea timu ya taifa ya Ujerumani U-20 kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2022, alizaliwa mwaka 2006 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo amewahi kunukuliwa akisema yeye ni Mtanzania halisi upande wa mama yake wakati baba ni Mjerumani, huku akibainisha kwamba hajakata tamaa kuichezea timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
Kiungo huyo alianza kucheza soka katika klabu za vijana za MTV Ahrensbök na baadaye TSV Pansdorf kabla ya kujiunga na akademi ya Hamburger SV mwaka 2021.
Akiwa HSV alisaidia timu ya vijana kutwaa ubingwa wa Ujerumani, kisha akapandishwa kikosi cha wakubwa na kuchangia kupanda kutoka Regionalliga hadi 2. Bundesliga na baadaye kufuzu Bundesliga ya wanawake.
Mwaka 2025 alijiunga na RB Leipzig, ambako alipata nafasi ya kucheza Bundesliga kwa mara ya kwanza alipocheza mechi 25 za ligi na kufunga mabao sita.