KUZIMIA
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa na klabu ya Tenerife imethibitisha kuwa mshambuliaji huyo amelazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Nuestra Señora de Candelaria, huku hali yake ikielezwa kuwa imetengemaa licha ya ukubwa wa tatizo alilolipata.
TENERIFE, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa CD Tenerife, Jesus de Miguel, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kupata tukio la kutisha lililotokana na kugongana vibaya na kipa wa Andorra, Jesus Owono, katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili Hispania uliofanyika Jumatatu iliyopita.
De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alizimia uwanjani dakika za nyongeza za kipindi cha pili, hali iliyosababisha mwamuzi kusitisha mchezo huo ukiwa sare ya mabao 2-2.
Taarifa iliyotolewa na klabu ya Tenerife imethibitisha kuwa mshambuliaji huyo amelazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Nuestra Señora de Candelaria, huku hali yake ikielezwa kuwa imetengemaa licha ya ukubwa wa tatizo alilolipata.
"Mchezaji wa CD Tenerife, Jesús de Miguel, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Nuestra Señora de Candelaria. Hali yake ni thabiti licha ya uzito wa hali yake."
Kwa mujibu wa taarifa za chombo cha habari cha Marca nchini Hispania, De Miguel alidaiwa kupata mshtuko wa moyo akiwa safarini kuelekea hospitalini na ilibidi afanyiwe huduma za kumrejesha katika hali ya kawaida ndani ya gari la wagonjwa.
Ripoti hizo zinaeleza kuwa licha ya hali yake kutengamaa, mshambuliaji huyo bado alikuwa hajapata fahamu, ingawa alikuwa akipumua vizuri.
Tukio hilo lilitokea dakika ya saba ya nyongeza, wakati De Miguel akijaribu kuanzisha shambulizi la kushtukiza kwa upande wa Tenerife baada ya kuupokea mpira mrefu.
Hata hivyo, katika harakati za kuokoa lango lake, kipa Owono aliruka kuondoa mpira lakini goti lake lilionekana kumpiga De Miguel kifuani.
Mshambuliaji huyo alionekana kuumia na kujiviringisha chini kabla ya baadaye kutulia bila kusogea, jambo lililowalazimu madaktari kukimbilia uwanjani kutoa huduma ya kwanza.
Kwa zaidi ya dakika tano, wahudumu wa afya walikuwa wakipambana kuokoa hali ya mchezaji huyo huku wachezaji wenzake wakionekana kushtushwa na tukio hilo. Baadhi yao walionekana wakitokwa na machozi.
Kipa Owono alionyeshwa kadi nyekundu kufuatia tukio hilo, kabla ya mwamuzi kuamua kuumaliza mchezo kutokana na uzito wa hali iliyokuwa ikiendelea.
Uwanja mzima ulitawaliwa na ukimya wakati De Miguel akipatiwa matibabu, lakini alipoondolewa kwa machela, mashabiki walimuaga kwa makofi ya heshima wakiwa wamesimama.
Baada ya kupelekwa kwenye gari la wagonjwa, ilielezwa kuwa kulikuwa na takribani dakika 15 za kusubiri kabla ya safari ya kuelekea hospitalini kuanza.
Kwa upande wake, klabu ya Andorra ilitoa ujumbe wa kumtakia nafuu mshambuliaji huyo na kuonesha mshikamano kwa familia yake pamoja na klabu ya Tenerife.
"Tunamtumia nguvu zetu zote na kumtakia kila la heri Jesús de Miguel baada ya tukio kubwa lililotokea katika mchezo wa leo. Tunatumaini atapona haraka. Tunamtakia kila la kheri yeye, familia yake na klabu ya Tenerife," ilisema taarifa hiyo.