Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mourinho: Ningekuwa Vinicius ningelazimisha kusepa Real Madrid

Muktasari:

  • Miongoni mwa matukio hayo ni kutolewa kwa kadi nyekundu kwa Vinicius Jr katika mchezo dhidi ya Villarreal, adhabu iliyofuata aliyopewa Mbrazili huyo ambayo ilitangazwa saa chache kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Roma, pamoja na uamuzi wake wa kukaa kimya baada ya mechi dhidi ya timu hiyo ya Castellon.

MADRID, HISPANIA: JOSE Mourinho alikutana na waandishi wa habari katika chumba cha mikutano na waandishi cha Valdebebas. Matukio ya hivi karibuni yalimpa sababu nyingi za kufanya hivyo.

Miongoni mwa matukio hayo ni kutolewa kwa kadi nyekundu kwa Vinicius Jr katika mchezo dhidi ya Villarreal, adhabu iliyofuata aliyopewa Mbrazili huyo ambayo ilitangazwa saa chache kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Roma, pamoja na uamuzi wake wa kukaa kimya baada ya mechi dhidi ya timu hiyo ya Castellon.

Kama ilivyoelezwa wakati huo, ilionekana kuwa bora kwake kutokuzungumza na waandishi wa habari ili kuepuka kutoa kauli ambazo zingeweza kumfanya apewe adhabu nyingine na kumzuia kusimama katika mechi ya El Clasico.

Kauli za kocha huyo Mreno katika Uwanja wa Stadio Olimpico mjini Roma kabla na baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopita, pamoja na kauli za rais wa La Liga, Javier Tebas kwenye mitandao ya kijamii ambapo aliishambulia Real Madrid TV na klabu yenyewe, zilizidisha mvutano huo. Hali hiyo ingeweza kumfanya Mourinho ajibu kwa ukali, lakini alitoa maelezo yake kwa utulivu. Twende pamoja!

Swali: Unaionaje timu yako?

Mourinho: Wachezaji wamechoka, lakini hawatakuwa wamechoka watakapocheza mechi ijayo. Kwa kuzingatia nilichoona katika kitengo cha matibabu, nadhani wamechoka kidogo, lakini tutakuwa sawa. Pia tuna chaguo zuri iwapo tutaamua kufanya mabadiliko na kuwaingiza wachezaji wenye nguvu.


Swali: Unataka nini kutoka kwa viungo wako?

Mourinho: Nawaomba viungo wawe viungo. Nawaomba wafanye kazi za kiungo. Mchezaji anayejihusisha na ulinzi pekee ana uwezo wenye mipaka. Ukiwa unashambulia pekee ni bora kucheza pembeni au kama kiungo mshambuliaji namba 10. Ni nafasi ngumu sana kucheza. Ili ufanye vizuri katika kiwango cha juu kabisa unahitaji ubora wa aina tofauti.


Swali: Kuhusu Tebas na ulinganisho wake na Real Madrid TV?

Tayari mmeona nachofikiri. Nawaomba msizungumzie suala hili kwa sababu kuna mipaka, na sasa limeingia katika eneo ambalo maelezo pekee yanayowezekana ni suala la kitabibu. Ikiwa sivyo, hakuna sababu inayoweza kuhalalisha jambo hilo wala kuomba msamaha. Nadhani mashabiki wa Madrid wanazidi kuelewa wanachokabiliana nacho.

Kama nilivyosema awali, kwa kuzingatia heshima na hadhi kubwa ambayo soka la Hispania linayo nje ya nchi, ni bora tujaribu kulishughulikia suala hili hapa badala ya kuliacha livuke mipaka na kuenea nje ya nchi.


Swali: Wakati wa maandalizi ya msimu ulisema Arda Guler angeweza kucheza kama kiungo wa chini, ikoje?

Mourinho: Anafanya kazi kwa bidii. Inaonekana kwangu kuwa mnapata shida kutambua na kuthamini juhudi zake. Mambo mabaya yanaonekana kuwa na mtu wa kulaumiwa, lakini mazuri yanaelezwa kuwa yametokana na bahati. Arda ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Kwa bahati nzuri, bado hajafikia ukamilifu wa uwezo wake. Ana sifa zinazomwezesha kucheza katika nafasi mbalimbali. Nina furaha sana naye.


Swali: Ni nini ambacho hukukipenda kuhusu Vinicius katika bao la pili la Roma?

Mourinho: Vinicius alikuwa na mchezo mgumu sana. Kwa maoni yangu, sababu kuu ilikuwa Gasperini (kocha wa Roma), kwa sababu aliendelea kushambulia kupitia upande wa Vinicius. Ilikuwa vigumu sana kwangu kama kocha kufanya mabadiliko.

Katika kipindi cha pili, Roma ilibadilisha mambo, na kilichonisumbua ni namna bao la pili lilivyofungwa. Mchezo ulikuwa na ushindani sawa, na hatukuwa na matatizo yoyote. Hakupaswa kufanya alichofanya, lakini sasa limepita. Hakuna tatizo. Nilifanya mabadiliko matano, siyo badiliko moja tu. Mabadiliko ni sehemu ya mchezo wa soka. Vinicius anatakiwa kufanya kazi kwa bidii zaidi na, bila kuahidi chochote kwa sababu sipendi kutoa ahadi, nadhani ataanza katika kikosi cha kwanza Jumatano.

Kuhusu adhabu ya kufungiwa mechi nne, ninafurahi kwa sababu walikuwa wanataka kumpa adhabu kubwa zaidi. Nilidhani wale watu wanaofanya mambo kwa siri wangeongeza mechi moja au mbili zaidi.


Swali: Unadhibiti vipi tabia na hisia za Vinicius?

Mourinho: Ni kijana mzuri sana, na ni rahisi kuwa na uhusiano naye mzuri. Natumia muda kuwa naye faraghani kila siku. Namheshimu na kumthamini sana kwa sababu daima anaweza kuendelea na maisha na kustahimili changamoto akiwa na tabasamu.

Kama ningekuwa katika nafasi yake, huenda nisingekuwa hapa. Ningelazimisha kuhamia nchi ambayo watu wananiheshimu. Lakini kwa sababu ya kujitoa kwake kwa Madrid na mapenzi yake kwa klabu, aliamua kubaki.

Anaamini mambo yanaweza kubadilika na kuwa bora, na anaendelea kutabasamu. Hakuna kitu wala mtu anayeweza kumnyang’anya tabasamu hilo.


Swali: Una mipango gani kwa Endrick?

Mourinho: Nadhani wakati mwingine tunapata shida kuwapongeza watu wanaofanya mambo vizuri. Tunawakosoa wale wanaofanya vibaya. Kijana huyo anastahili pongezi kwa jinsi anavyojitokeza kwa nguvu kubwa.

Kuna wachezaji wengi wanaostahili kucheza. Wanaostahili kucheza ni zaidi ya 11. Wapo 15 au 16. Lunin anastahili kucheza, na sisemi kwa utani. Anafanya mazoezi kila siku akiwa pamoja na kipa bora zaidi duniani na anaendelea kuwa na mtazamo chanya, lakini hachezi. Siwezi kuwaweka wote wawili uwanjani kwa wakati mmoja.

Hali ni hiyo hiyo kwa wachezaji wa nje ya uwanja. Sote tutakubaliana kuwa wachezaji wanaoingia na kubadilisha mchezo wanastahili kucheza, lakini vipi kuhusu wengine? Je, Diomande hastahili kucheza? Je, Cucurella hastahili kucheza? Je, Valverde hastahili kucheza? Je, Mbappé hastahili kucheza?

Hilo ndilo linalofanya sehemu hii ya kazi ya ukocha kuwa ngumu sana. Wenzangu wanaofundisha timu zenye rasilimali chache zaidi watasema nina bahati. Ni bahati na wakati mwingine siyo bahati kuwa na waandishi wa habari kama ninyi, ambao mnafanya kazi hii kuwa ngumu zaidi.


Swali: Unafikiria kuingia katika soko la usajili la majira ya baridi?

Mourinho: Kuhusu usajili, siombi chochote. Nina furaha na kikosi pamoja na wachezaji nilionao. Nina hisia kwamba katika mazingira ya kawaida, wachezaji huboresha uwezo wao mmoja mmoja na kwa pamoja, hasa tunapokuwa na muda na utulivu wa kufanya kazi. Kazi ya kocha ni kuwaendeleza wachezaji wake.

Sidhani kama mnaniona kama mtu anayeomba wachezaji. Napenda kuwa na vikosi vidogo, na ikiwa mchezaji mpya atakuja, basi mwingine atalazimika kuondoka. Ikiwa uongozi wa masuala ya michezo utaona kuna jambo la kufanya, tupo tayari kulijadili na kulitathmini. Lakini halitakuwa wazo litakaloanzishwa na mimi.


Swali: Unampa Vinicius ushauri kuhusu mambo mengine?

Mourinho: Hayo ni mazungumzo ya faragha. Alipoongeza mkataba wake, alisaini kwa kuzingatia kwamba Madrid ni nyumbani kwake, akiwa na nia ya kuendelea kuandika historia na kushinda mataji. Anaelewana vizuri na kila mtu katika chumba cha kubadilishia nguo na ni chanzo kikubwa cha furaha kwa wenzake.

Nina mashaka makubwa kama ningekuwa na nguvu ya kubaki hapa kama ningekuwa katika nafasi yake, hasa kwa kuzingatia ofa zote alizokuwa nazo.


Swali: Una maoni gani kuhusu Valverde kucheza kiungo?

Mourinho: Nipo hapa kufanya kile nachoamini kuwa bora kwa timu. Nadhani siku itafika ambapo akili mnemba (AI) na tafiti zitakuwa zikiambia timu nini cha kufanya, huku makocha wakibaki na jukumu la kufanya kazi uwanjani pekee. Lakini hadi sasa, makocha bado ndio wanaofanya uamuzi.

Kocha ambaye hayupo tayari kusikiliza maoni ya wengine ni kocha mwenye uwezo wenye mipaka. Kwa heshima zote naamini baadhi ya watu hutoa maoni kwa sababu wanapenda soka, huku wengine wakifanya hivyo kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao. Lakini maoni hayo hayana thamani kubwa kuliko uchambuzi wangu mwenyewe. Wakati huohuo, kocha aliye tayari kusikiliza maoni ya wengine siyo lazima awe kocha mzuri.

Niko tayari kusikiliza maoni ya wafanyakazi wenzangu katika benchi la ufundi. Naweza kubadilisha mawazo yangu, lakini nafanya hivyo kwa kutegemea uchambuzi wangu, siyo kwa kuzingatia maoni ya watu walio nje ya klabu.

Naweza kuchagua njia tofauti, kama ilivyo katika suala la Tchouameni (Aurelien) na Valverde (Federico). Mchezo una nyakati na vipengele vinavyotofautiana. Uwepo wa nafasi tano za kufanya mabadiliko kwa timu zenye vikosi imara muhimu sana.