Mbappe arejea kwa kishindo, ReaL Madrid yaendeleza ubabe Ulaya
Muktasari:
- Nyota huyo alikosa kwa tofauti ndogo tu kutwaa tuzo ya Ballon d’Or baada ya kushindwa na Harry Kane wa Bayern Munich Jumatatu iliyopita. Baadaye alilazimika kuomba radhi kufuatia taharuki iliyozuka kwenye mitandao ya kijamii kutokana na video aliyokuwa akitania kuhusu aliyekuwa kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong.
MADRID, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe ameweka kando wiki yenye misukosuko aliyopitia baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti na kuisaidia Real Madrid kupata ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Racing Santander, juzi Jumapili usiku, katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania (La Liga).
Nyota huyo alikosa kwa tofauti ndogo tu kutwaa tuzo ya Ballon d’Or baada ya kushindwa na Harry Kane wa Bayern Munich Jumatatu iliyopita. Baadaye alilazimika kuomba radhi kufuatia taharuki iliyozuka kwenye mitandao ya kijamii kutokana na video aliyokuwa akitania kuhusu aliyekuwa kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong.
Mechi ya Real Madrid, pamoja na michezo mingine ya soka nchini Hispania iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita haikuonyeshwa na televisheni ya taifa ya China kutokana na athari za tukio hilo.
Jude Bellingham na Yan Diomande nao walifunga mabao na kuiwezesha Madrid inayoshika nafasi ya tatu kuendelea kubaki ndani ya pointi tatu dhidi ya vinara wa La Liga, Barcelona, ambao waliichakaza Alaves kwa mabao 6-1. Real Madrid ya Jose Mourinho imeshinda mechi sita mfululizo katika mashindano yote na sasa inazidiwa kwa pointi moja na Atletico Madrid, ambayo iliifunga Levante mabao 2-0.
Mfululizo wa Real Sociedad wa kushinda mechi nne mfululizo ulifikia mwisho baada ya kufungwa mabao 2-1 na Athletic Bilbao, kutokana na mabao ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Inaki Williams na Alex Berenguer, ambaye alifunga kwa mkwaju wa penalti.
SERIE A HAKUPOI
Nchini Italia katika Serie A, Lazio inayofundishwa na Gennaro Gattuso imeimarisha nafasi yake kileleni mwa Serie A baada ya kuichapa Cagliari mabao 2-1, na kuipiku Inter Milan ambayo kabla ya kuanza kwa michezo ya mwishoni mwa wiki ilikuwa imefungana nayo pointi.
Lazio ilianza vibaya mchezo huo baada ya Cagliari kupata bao kupitia kwa M’Bala Nzola dakika ya 20, kabla ya mabao ya Gustav Isaksen na Andrea Pinamonti, yaliyofungwa katika kila kipindi kuipa ushindi wake wa sita mfululizo katika Serie A.
Como, wababe wa Manchester United katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ilirejea ndani ya timu nne za juu Serie A baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya timu inayoshika mkia, Venezia. Huo ulikuwa ushindi wake wa tano mfululizo katika mashindano yote. Wenyeji walitawala mchezo huo, lakini walihitaji mkwaju wa penalti ili kupata bao pekee, ambapo nahodha wa Como, Lucas Da Cunha, alitupia dakika ya 43 na kupata bao lake la kwanza msimu huu.
“Hii ni aina ya mechi ambazo tulikuwa tunapata ugumu kuzishinda msimu uliopita,” Da Cunha aliiambia DAZN baada ya mchezo huo kumalizika.
Nayo mabao ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Kerim Alajbegovic na Jeremie Boga yaliihakikishia Juventus kurejea kwenye ushindi baada ya kuichapa Napoli mabao 2-0. Napoli, ambayo ilikuwa na wachezaji 10 baada ya Luca Marianucci kuonyeshwa kadi nyekundu kipindi cha pili, ilipoteza mchezo huo na kupata kipigo chake cha nne msimu huu.
LIGUE 1 HAKUBOI
Katika Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), Lyon na Paris FC zote zilipata ushindi na hivyo kusogea karibu na mabingwa watetezi wa Ligue 1, PSG ambao walishinda dhidi ya Monaco kwa mabao 3-1. Lyon ilishinda 2-0 nyumbani dhidi ya Angers kupitia mabao yaliyofungwa katika kila kipindi na Ernest Nuamah na Corentin Tolisso.
Ushindi huo uliisaidia kujinasua baada ya kufungwa mabao 2-0 ugenini na PSG katika mchezo uliopita. Mabingwa hao wa Ufaransa mara saba wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa nyuma ya PSG kwa pointi tatu na Lille inayoshika nafasi ya pili kwa pointi moja.
Ushindi wa Lyon umekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba kocha Paulo Fonseca, anakaribia kuondoka klabuni hapo ili kurejea kwao Ureno.
“Najua kwamba kesho asubuhi nitakuwa pamoja na wachezaji, lakini kuhusu yatakayotokea baada ya hapo ni vigumu kusema,” alisema Fonseca akiwaambia waandishi wa habari.
Fonseca alionekana akitokwa na machozi alipokuwa akikumbatiana na wasaidizi wake wa benchi la ufundi mwishoni mwa mchezo huo.
Inadaiwa kuwa Fonseca anawaniwa na Sporting Lisbon, ambayo kocha wake Rui Borges anakabiliwa na presha. Paris FC inashika nafasi ya nne baada ya kuifunga Monaco katika Uwanja wa Stade Jean-Bouin. Mshambuliaji wa kimataifa wa Mali, Lassine Sinayoko, alifunga mabao mawili mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kuipa Paris FC faida, kabla ya Folarin Balogun kuifungia Monaco bao la kufutia machozi dakika ya 65.