Konsa ampa tahadhari Harry Kane
Muktasari:
- Konsa, mwenye umri wa miaka 28, anatarajia mtihani mkubwa dhidi ya Kane, mshambuliaji anayetambulika kwa uwezo wake wa kufunga mabao na kushuka katikati ya uwanja kusaidia kujenga mashambulizi.
LONDON, ENGLAND: BEKI Ezri Konsa ameweka wazi dhamira yake ya kuiongoza Arsenal kupata ushindi mwingine bila kuruhusu bao itakapokutana na Bayern Munich katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akitarajia kukabiliana na nahodha mwenzake wa timu ya taifa ya England, Harry Kane.
Konsa, mwenye umri wa miaka 28, anatarajia mtihani mkubwa dhidi ya Kane, mshambuliaji anayetambulika kwa uwezo wake wa kufunga mabao na kushuka katikati ya uwanja kusaidia kujenga mashambulizi.
Hata hivyo, beki huyo ana kumbukumbu nzuri dhidi ya mshambuliaji huyo. Miaka miwili iliyopita, akiwa na Aston Villa, alikuwa sehemu ya kikosi kilichoifunga Bayern Munich kwa bao 1-0 katika michuano hiyo.
Sasa akiwa Arsenal, Konsa anataka kurudia mafanikio hayo na kuhakikisha timu yake inapata ushindi ugenini.
Akizungumza kuhusu pambano hilo, Konsa amesema anafurahia kukutana na Kane, ambaye ni mwenzake katika timu ya taifa ya England.
"Ni furaha kwangu kukutana tena na Kane, nina hakika nitaiwezesha timu yangu kupata ushindi muhimu," amesema Konsa.
Amesema Kane amefanikiwa kumfunga mara mbili pekee katika michezo waliyokutana, na mabao yote mawili yalifungwa kwa penalti wakati mshambuliaji huyo alipokuwa Tottenham Hotspur.
Hata hivyo, Konsa alikiri kuwa Kane ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza maeneo mbalimbali, kusaidia wenzake na kufunga mabao.
Ameongeza kuwa Arsenal inatambua ugumu wa mchezo huo, hasa kutokana na ubora wa Bayern Munich, lakini kikosi hicho kitajiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
Akiwa Arsenal, anatamani mataji zaidi
Konsa amejiunga na Arsenal akitokea Aston Villa katika uhamisho ulioripotiwa kugharimu pauni milioni 55.
Beki huyo amewasili Emirates akiwa na uzoefu wa kutwaa taji la Europa League akiwa na Villa, lakini sasa ana malengo makubwa zaidi ya mafanikio katika soka la Ulaya.
Amesema alipojiunga na Arsenal, alikuwa na kiu ya kushinda mataji na anaamini kikosi hicho kina ubora na viwango vinavyoweza kukiwezesha kupigania kila kombe.