Kompyuta yatabiri… Bingwa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Sasa, baada ya droo ya Kombe la Dunia la 2026 kupangwa Marekani, mapema tu kompyuta imetumika kubashiri jinsi mashindano yote yatakavyoenda hadi bingwa kupatikana. Ni nani bingwa?
WASHINGTON DC, MAREKANI: NI taifa gani unaloamini litaenda kubeba Kombe la Dunia 2026 huko Marekani? Bila ya shaka una mtazamo wako kuhusu nchi gani itaenda kutwaa taji hilo kubwa na lenye heshima zaidi katika mchezo soka baada ya Argentina ya Lionel Messi kulitwaa taji la fainali zilizopita 2022 kule Qatar.
Sasa, baada ya droo ya Kombe la Dunia la 2026 kupangwa Marekani, mapema tu kompyuta imetumika kubashiri jinsi mashindano yote yatakavyoenda hadi bingwa kupatikana. Ni nani bingwa?
Bila shaka haiwezekani kutabiri bingwa wa Kombe la Dunia kwa usahihi, kwa kuwa kila wakati timu zinazoonekana kuwa ni dhaifu huibuka na kuangusha mibuyu huku mataifa makubwa yakionekana kushindwa kutimiza matarajio.
Hata hivyo, kilichofanyika hapa ni kutabiri jinsi hatua za mtoano zitakavyokuwa kama hakuna matokeo ya kushtukiza, ili kubaini mechi zinazotarajiwa zaidi na njia ambazo timu zinaweza kupita kwenda fainali.
Kwa kuangalia viwango rasmi vya FIFA, utabiri huu unaangalia kila mechi kuanzia mchujo hadi fainali.
Droo ya mwaka huu ilipangwa makusudi kuhakikisha kuwa mataifa manne bora duniani, Hispania, Argentina, Ufaransa na England hayakutani katika hatua moja ya mtoano iwapo yote yatamaliza makundi yao kama washindi. Hata hivyo, safari yao kuelekea nusu fainali bado inaonekana kuwa ngumu.
Hispania, mabingwa wa Ulaya, wanaonekana kuwa na njia nyepesi zaidi katika utabiri huu, wakitarajiwa kukutana na Austria, Croatia na Ubelgiji katika hatua tatu za mwanzo za mtoano. Kwa upande wa Ufaransa, mambo ni magumu zaidi, kwani ina uwezekano wa kukutana na vigogo wa Ulaya Ujerumani na Uholanzi kabla ya marudiano ya nusu fainali ya EURO 2024 dhidi ya kikosi cha Luis de la Fuente, Hispania.
England huenda ikapata safari ngumu zaidi, ikikabiliana na Norway ya straika matata Erling Haaland, wenyeji Mexico, na mabingwa mara tano wa Kombe la Dunia, Brazil.
Kwa mabingwa watetezi Argentina, wanatarajiwa kukutana na kocha maarufu Marcelo Bielsa na timu yake ya Uruguay kabla ya kukutana na Ureno katika robo fainali ya kuvutia ambayo inaweza kumshuhudia Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakivaana kwa mara ya mwisho kwenye jukwaa kubwa zaidi.Kwa upande mwingine, Brazil na Uholanzi huenda wakawa mataifa makubwa yaliyo katika hatari kubwa ya kutolewa mapema. Ukiachia mbali uwezekano wa matokeo kushangaza yanayoweza kutokea, utabiri huu unaonyesha kwamba timu zitakazotinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 ni Argentina ya Messi dhidi ya Ureno ya Ronaldo, England ya Harry Kane dhidi ya Brazil ya Neymar, Ubelgiji ya Romelu Lukaku dhidi ya Hispania ya Lamine Yamal, huku Uholanzi ya Coady Gakpo ikikutana na Ufaransa ya Kylian Mbappe.
Kwa mujibu wa utabiri huo, Messi atambwaga Ronaldo na hivyo Argentina kwenda nusu fainali ambako itakutana na England ambayo itaibwaga Brazil, wakati nusu fainali ya pili itazikutanisha Hispania ya Yamal na Ufaransa ya Mbappe.
Baada ya hapo utabiri huo umeendelea kuonyesha kwamba Yamal na Hispania watapenya kwenda fainali ambako watakutana na Argentina ya Messi na mwisho Hispania itabeba taji hilo kwa mara ya pili katika historia yake, baada ya awali kulibeba taji hilo mwaka 201, katika fainali zilifanyika barani Afrika kwa mara ya kwanza kule, Afrika Kusini.
Hata hivyo, utabiri huo ambao umezingatia viwango na ubora wa hivi karibuni wa timu zote shiriki, umeonya kuwa viwango pekee haviwezi kuamua kila kitu kuhusu soka hivyo matokeo haya yanaweza yasiwe na mashiko yoyote na bingwa wa dunia awe timu nyingine kabisa.