Croatia yaihofu Ghana Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Croatia watafungua kampeni yao dhidi ya England kisha kumaliza kundi kwa kukutana na Ghana.
WASHINGTON DC, MAREKANI: KOCHA mkuu wa Croatia, Zlatko Dalić, anasema timu yake haitaimdharau Ghana licha ya Black Stars kuingia kwenye droo ya Kombe la Dunia 2026 wakiwa katika Pot Four na kushika nafasi ya 72 duniani.
Mataifa hayo yamepangwa pamoja katika Kundi L, pamoja na England na Panama.
Kihistoria, Croatia ambao walifikia fainali 2018 na nusu fainali 2022, wanaonekana kama miongoni mwa wanaofaa kutinga hatua inayofuata.
Ghana walifika katika droo wakiwa miongoni mwa timu zilizo na viwango vya chini kabisa kwenye mashindano hayo. Lakini Dalić anasisitiza kuwa viwango hivyo haviathiri namna watakavyokabiliana.
Kocha huyo alitaja pia uelewa wake wa soka la Ghana kutokana na urafiki wake na nahodha wa zamani Asamoah Gyan, aliyemfundisha Uarabuni.
“Ninamjua rafiki yangu Asamoah Gyan. Alikuwa mchezaji wangu nikiwa LA,” Dalić aliambia Flashscore.
Amesema Ghana wana nguvu, kasi na ni timu isiyotabirika—kitu kinachoweza kusumbua timu yoyote.
“Najua zitakuwa mechi ngumu. Ghana ni timu imara na ya kasi.”
Pamoja na kuwepo kwa England kwenye kundi, na Panama kuibuka kama timu ya ushindani, Dalić amesema Croatia lazima iwe makini.
“Lengo letu ni kupita hatua ya makundi. Hatua kwa hatua. Si rahisi. Tunaiheshimu Ghana kabisa.”
Croatia watafungua kampeni yao dhidi ya England kisha kumaliza kundi kwa kukutana na Ghana.