Kocha Nigeria aahidi makubwa
Muktasari:
- Nigeria maarufu Super Falconets, ni miongoni mwa timu tatu ambazo zimewahi kushiriki kila toleo la Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2002, pamoja na Brazil na Marekani.
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria chini ya miaka 20, Moses Aduku, amesema kikosi chake kimejipanga kufanya makubwa katika Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 linakalofanyika Poland, huku akisisitiza kuwa hawajaenda kushiriki tu.
Nigeria maarufu Super Falconets, ni miongoni mwa timu tatu ambazo zimewahi kushiriki kila toleo la Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2002, pamoja na Brazil na Marekani.
Pamoja na historia hiyo, Nigeria bado haijawahi kubeba ubingwa wa dunia wa U-20, huku ikiwa imeshafika fainali mara mbili na kumaliza ikiwa mshindi wa pili.
Aduku alisema safari ya Poland ni nafasi nyingine kwa Nigeria kuonyesha uwezo wake na kuanza kujenga kizazi kitakachokuja kuwa tegemeo la timu ya taifa ya wakubwa.
“Nigeria imekuwa hapa tangu kuanza kwa mashindano haya, lakini safari hii tunataka kufanya tofauti,” alisema Aduku katika mahojiano na FIFA.
Kocha huyo aliongeza kuwa licha ya kuheshimu wapinzani wao, kikosi chake hakijaenda Poland kwa ajili ya kuwa mtazamaji, bali kinaamini kina uwezo wa kufanya vizuri na kuvuka hatua ya makundi.
Nigeria imepangwa Kundi B pamoja na mabingwa watetezi Hispania, China na New Caledonia, timu ambayo inashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza.
Aduku amesisitiza kuwa hawataki kuangalia ukubwa wa majina ya wapinzani wao bali watawasoma vizuri na kuwaheshimu.
“Tunawaheshimu wapinzani wote kwa sababu wote ni timu nzuri. Lakini tumekuja kwa ajili ya kazi. Tutachukua mchezo mmoja baada ya mwingine na ninaamini tutatoka kwenye kundi,” alisema.
Nigeria pia ina sababu nyingine ya kupambana kwa nguvu kutokana na kutofuzu kwa timu zake za taifa za wakubwa katika michuano mikubwa.
Baada ya Nigeria kushindwa kufuzu Kombe la Dunia la wanaume 2026 pamoja na Kombe la Dunia la wanawake 2027 nchini Brazil, Super Falconets wamebeba matumaini ya kurejesha furaha ya mashabiki wa taifa hilo.