Kobbie Mainoo kukomaa na Man United
Muktasari:
Mainoo amekosa mechi tatu zilizopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kigimbi huku akiwa hajaanzishwa kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu England msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND:KIUNGO, Kobbie Mainoo amebadili mawazo na kuamua kupambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United licha ya kuwekwa sana benchini na kocha Ruben Amorim.
Mainoo amekosa mechi tatu zilizopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kigimbi huku akiwa hajaanzishwa kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu England msimu huu.
Licha ya kuwapo na msuguano baina ya Mainoo na kocha Amorim, lakini kwa mujibu wa wale waliopo karibu na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 zao la kutoka kwenye akademia ya Man United anataka kupambana na kurudi kwenye ubora wake akiwa hapohapo Old Trafford.
Mainoo ameanzishwa kwenye mechi 16 tu kati ya 61 zilizoongozwa na kocha Amorim katika kikosi hicho cha Man United, huku kwa msimu huu alianza katika mchezo wa Kombe la Ligi, ambapo timu hiyo ilitupwa nje ya mashindano na klabu ya daraja la chini, Grimsby.
Man United ilizuia maombi ya Mainoo ya kutaka kuondoka kwa mkopo kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi na bila ya shaka itazuia pia kwenye dirisha hili kutokana na Bruno Fernandes kusumbuliwa na maumivu ya misuli.
Mkataba wa Mainoo huko Man United itafika tamati 2027, huku kuwa na kipengele cha kumwongezea mwaka mmoja. Na huenda kocha Amorim asimtumie kwenye mechi dhidi ya Leeds United kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England, Jumapili.