Kisa Welbeck, Alonso afumua safu ya ushambuliaji
Muktasari:
- Welbeck, mwenye umri wa miaka 35, yupo hatua za mwisho kutua Stamford Bridge kwa mkataba wa miaka miwili. Mshambuliaji huyo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kujiunga na wenzake katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya itakayohamia Hong Kong.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imeonyesha kubadili kabisa falsafa yake ya usajili baada ya kukaribia kumsajili mshambuliaji mkongwe Danny Welbeck, huku kocha Xabi Alonso akionekana kutaka kuchanganya vijana wenye vipaji na wachezaji wenye uzoefu katika kikosi chake.
Welbeck, mwenye umri wa miaka 35, yupo hatua za mwisho kutua Stamford Bridge kwa mkataba wa miaka miwili. Mshambuliaji huyo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kujiunga na wenzake katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya itakayohamia Hong Kong.
Ikiwa dili hilo litakamilika, straika huyo wa zamani wa Brighton atasaini mkataba wa kumuweka Chelsea hadi mwaka 2028, baada ya kutoka kwenye msimu mzuri alioufunga kwa mabao 13 katika Ligi Kuu England.
Usajili wa Welbeck unaonyesha wazi mabadiliko ya mkakati wa Alonso, ambaye tofauti na viongozi waliomtangulia, sasa anaonekana kuwinda zaidi wachezaji waliokwisha kuthibitisha uwezo wao katika kiwango cha juu.
Mbali na Welbeck, Chelsea pia inaendelea kumfuatilia kiungo mkongwe Jordan Henderson, huku awali Alonso akiwahi kuonyesha nia ya kuwasajili Granit Xhaka na John Stones, lakini mipango hiyo haikuzaa matunda.
Kwa sasa Chelsea ipo Australia kwa maandalizi ya msimu mpya, lakini baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Tottenham, kikosi hicho kitaelekea Hong Kong kabla ya kuendelea na ziara zake nchini Malaysia na Indonesia.
Wakati huo huo, Chelsea inaendelea kuimarisha safu nyingine za kikosi. Tayari imekamilisha usajili wa Morgan Rogers kwa ada ya pauni117 milioni, huku beki Maxence Lacroix akitarajiwa kutambulishwa rasmi baada ya makubaliano ya pauni52 milioni na Crystal Palace.
Welbeck afungua mlango wa wengine kuondoka
Kuwasili kwa Welbeck kunaweza kubadili kabisa ramani ya safu ya ushambuliaji ya Chelsea.
Kwa sasa Alonso anao Liam Delap, Emmanuel Emegha, Nicolas Jackson, Marc Guiu na Joao Pedro, lakini taarifa zinaeleza kuwa angalau washambuliaji wawili wataondoka kwa kuuzwa au kutolewa kwa mkopo, huku uwezekano wa watatu kuondoka pia ukiwa mkubwa.
Miongoni mwao, Joao Pedro ndiye anayeonekana kuwa salama zaidi. Chelsea haina mpango wa kumuuza baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika maandalizi ya msimu mpya.
Mshambuliaji huyo aliweka wazi ubora wake alipofunga hat-trick ndani ya dakika tisa katika ushindi wa mabao 6-4 dhidi ya Western Sydney Wanderers, akithibitisha kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaoaminika zaidi na Alonso.
Kwa upande mwingine, Liam Delap alishindwa kuvutia katika mchezo huo, ingawa alicheza kwa muda mwingi akiwa amezungukwa na wachezaji wa akademi, tofauti na Joao Pedro aliyeingia baadaye pamoja na kikosi cha kwanza.
Chelsea sasa inaendelea na maandalizi ya msimu huku Alonso akijenga kikosi anachokiamini, na ujio wa Welbeck unaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa ndani ya safu ya ushambuliaji ya The Blues.