Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuchel alivyojivisha mabomu England

Muktasari:

  • Tuchel hajawahi kuwa kocha wa kubembeleza majina makubwa na hilo limedhihirika tena baada ya kuwaacha nje baadhi ya mastaa waliokuwa wakitajwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.

LONDON, ENGLAND: WAINGEREZA hawaamini. Thomas Tuchel ameanza rasmi hesabu zake kwa kutuma ujumbe mzito kwa mastaa wa taifa hilo baada ya kufanya maamuzi magumu yaliyoitikisa wadau na mashabiki wa soka nchini humo kuelekea Kombe la Dunia ambalo litafanyika Amerika Kaskazini.

Tuchel hajawahi kuwa kocha wa kubembeleza majina makubwa na hilo limedhihirika tena baada ya kuwaacha nje baadhi ya mastaa waliokuwa wakitajwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho.

Iwe ni kumuacha nje Jude Bellingham wa Real Madrid au kumshusha hadhi Harry Maguire hadi kuwa chaguo la tano katika safu ya ulinzi wa kati, Tuchel ameonyesha wazi kuwa kwake jina kubwa halina nafasi mbele ya kile anachoamini.

Wakati mtangulizi wake Gareth Southgate akionekana kuwa mwangalifu kupita kiasi, Tuchel ameibuka na sura mpya ya England yenye uthubutu na maamuzi yasiyotetereka.

“Kuna wataalamu wa kila mazingira ndani ya kikosi hiki. Tunataka kuwa bora kwenye mipira ya adhabu, kona na hata penalti,”  anasema Tuchel kwa kujiamini.

Kauli hiyo imeonyesha wazi kuwa kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Bayern Munich ameandaa kikosi chake kwa hesabu maalum huku akionekana tayari kucheza kamari kubwa ili kufanikisha ndoto ya England.


KURUDI KWA TONEY

Miongoni mwa maamuzi yaliyoshangaza wengi ni kurejea kwa Ivan Toney ndani ya kikosi hicho baada ya kupotea kwa muda mrefu.

Straika huyo wa Al-Ahli amefunga mabao 42 msimu huu Saudi Arabia na sasa amepewa nafasi nyingine ya kuthibitisha ubora wake.

Wengi wanaamini Tuchel anatafuta mbadala wa uhakika wa Harry Kane endapo mshambuliaji huyo atapata matatizo wakati wa mashindano hayo. Hata hivyo, uteuzi wa Toney umeacha maswali mengi baada ya Tuchel kuwapa nafasi wachezaji wengine kama Dominic Calvert-Lewin huku akimpuuza mkongwe Danny Welbeck wa Brighton & Hove Albion.

FODEN, PALMER WAFUNGIWA VIOO

Katika eneo la kiungo, Tuchel ameibua mjadala mkubwa baada ya kuwaacha nje Phil Foden wa Manchester City na Cole Palmer wa Chelsea.

Badala yake, kocha huyo ameonekana kuweka zaidi nguvu kwenye uwiano wa kikosi kuliko majina makubwa.

Declan Rice na Elliot Anderson wanatajwa kuwa msingi wa kiungo hicho, huku kurejea kwa Kobbie Mainoo kukiongeza ushindani mkubwa. Pia nafasi ya namba 10 imeendelea kuwa mjadala mkubwa kati ya Bellingham na nyota wa Aston Villa, Morgan Rogers.


UKUTA WA ENGLAND WAZUA HOFU

Licha ya kujiamini kwake, Tuchel bado anakabiliwa na maswali mengi kwenye safu ya ulinzi.

John Stones ameendelea kusumbuliwa na majeraha huku Reece James na Tino Livramento nao wakiwa na historia nao ya majeraha ya mara kwa mara.

Kuitwa kwa Dan Burn wa Newcastle United nako kumezua mjadala mkubwa baada ya wachezaji kama Luke Shaw na Lewis Hall kuachwa nje.

Wakati huohuo, kuitwa kwa Djed Spence kumeibua tena mjadala kuhusu Trent Alexander-Arnold ambaye ameonekana kupoteza kabisa nafasi yake ndani ya kikosi hicho.

JESHI LA ENGLAND

Katika kikosi hicho, makipa ni Jordan Pickford (Everton), Dean Henderson (Crystal Palace) na James Trafford (Manchester City).

Mabeki; Reece James (Chelsea), Ezri Konsa (Aston Villa), Jarell Quansah (Bayer Leverkusen), John Stones (Manchester City), Marc Guehi (Manchester City), Dan Burn (Newcastle United), Nico O’€™Reilly (Manchester City), Djed Spence (Tottenham Hotspur) na Tino Livramento (Newcastle United).

Viungo wa kati ni Declan Rice (Arsenal), Elliot Anderson (Nottingham Forest), Kobbie Mainoo (Manchester United), Jordan Henderson (Brentford), Morgan Rogers (Aston Villa), Jude Bellingham (Real Madrid) na Eberechi Eze (Arsenal).

Washambuliaji; Harry Kane (Bayern Munich), Ivan Toney (Al-Ahli), Ollie Watkins (Aston Villa), Bukayo Saka (Arsenal), Marcus Rashford (Barcelona), Anthony Gordon (Newcastle United) na Noni Madueke (Arsenal).

England itaanza maandalizi ya Kombe la Dunia kwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya New Zealand, Juni 6 na Costa Rica, Juni 10 kabla ya kutua Amerika Kaskazini na kutupa karata yao ya kwanza dhidi ya Croatia, Juni 17.

UBABE WA ENGLAND

England ni moja ya mataifa yenye historia kubwa zaidi katika soka la dunia, lakini kwa miaka mingi imekuwa ikipewa lawama kwa kushindwa kuendana na ukubwa wa jina lake kwenye mashindano makubwa, hasa Kombe la Dunia.

Licha ya kuwa taifa lililoanzisha mchezo wa kisasa wa soka, England imewahi kushinda Kombe la Dunia mara moja tu mwaka 1966 walipobeba taji hilo nyumbani chini ya nahodha wao wa kihistoria, Bobby Moore.

Tangu ushindi huo wa kihistoria katika dimba la Wembley dhidi ya Ujerumani Magharibi, Waingereza wamekuwa wakisubiri kwa zaidi ya nusu karne kurejesha tena ubabe wao duniani.

Katika kipindi hicho, England imekuwa ikipeleka vikosi vyenye majina makubwa kama David Beckham, Steven Gerrard, Frank Lampard na Wayne Rooney lakini mara nyingi wameishia kuanguka kabla ya hatua ya mwisho.

Kizazi hicho cha mastaa kilionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kutwaa mataji lakini kilishindwa kuvuka presha na matarajio makubwa ya mashabiki wa England.

Katika Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini, England iliondolewa kwa fedheha baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Ujerumani, mechi iliyobaki kwenye kumbukumbu kutokana na bao la Lampard lililokataliwa.

Miaka minne baadaye nchini Brazil, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya England kuishia hatua ya makundi bila kushinda mchezo wowote, jambo lililoibua hasira kubwa kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari.

Kuibuka kwa Gareth Southgate kulianza kubadili sura ya timu hiyo baada ya kuijenga England yenye umoja, nidhamu na utulivu mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Southgate aliivusha England hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 Russia, hatua ambayo iliamsha matumaini mapya kwa taifa hilo baada ya miaka mingi ya maumivu.

Katika Euro 2020, England ilifika fainali lakini ikapoteza kwa penalti dhidi ya Italia mbele ya mashabiki wake Wembley huku wengi wakiamini nafasi kubwa ya kubeba taji ilikuwa imepotea.

Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar nalo lilimalizika kwa maumivu baada ya kutolewa na Ufaransa robo fainali, licha ya England kuonyesha kiwango kizuri katika sehemu kubwa ya mashindano hayo.

Sasa matumaini ya taifa hilo yapo mikononi mwa Tuchel ambaye amepewa jukumu la kuirudisha England kileleni mwa soka la dunia.


HUYU NDO TUCHEL

Tuchel ataiongoza England akiwa na rekodi kubwa barani Ulaya baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea mwaka 2021 na kujijengea sifa ya kuwa kocha mwenye mbinu kali na anayependa ushindani.

Tofauti na Southgate ambaye alijulikana kwa utulivu na kuwapa nafasi mastaa wake kujiamini, Tuchel ameanza kwa kutuma ujumbe kwamba hakuna mchezaji mwenye nafasi ya kudumu kikosini.

Ameonyesha kuwa yuko tayari kufanya maamuzi ya kushangaza, kuacha nje majina makubwa na kucheza kamari kubwa ikiwa ataamini ndiyo njia sahihi ya kuifikisha England kwenye mafanikio.

Changamoto kubwa kwa Tuchel haitakuwa tu kushinda mechi, bali kubeba presha kubwa ya taifa ambalo limekuwa likisubiri kwa miaka 60 kuona timu yao ikibeba tena Kombe la Dunia.

Waingereza wanaamini kizazi cha sasa kina vipaji vya kutosha kufanya makubwa kupitia mastaa kama Kane, Rice na Bellingham lakini swali kubwa limebaki kama Tuchel ataweza kugeuza vipaji hivyo kuwa taji.