Kiemba, Domayo zamu yenu kuchambuliwa
Muktasari:
- Maana kile walichokuwa wanafanya Amri Kiemba na Frank Domayo katika tasnia ya habari kwa maana ya uchambuzi kimeonekana ni kizuri hadi wakaweza kuwashawishi Kagera Sugar kuwachukua.
UNAPOONA waandamizi wawili wa uchambuzi wa soka wanaajiriwa katika klabu ya soka hiyo ni heshima kubwa kwa tasnia ya habari.
Maana kile walichokuwa wanafanya Amri Kiemba na Frank Domayo katika tasnia ya habari kwa maana ya uchambuzi kimeonekana ni kizuri hadi wakaweza kuwashawishi Kagera Sugar kuwachukua.
Mabosi wa Kagera Sugar tunaamini walikuwa na majina kibao ya makocha mezani wanaoomba kuwa makocha wasaidizi wa timu hiyo chini ya Cedrick Kaze.
Lakini uamuzi wa kuwachukua Kiemba na Domayo bila shaka umechagizwa na kile ambacho wachezaji hao wa zamani wa Taifa Stars wamekuwa wakikifanya katika luninga za Azam TV ambacho ni kuchambua soka.
Kwa hiyo kijiwe kinawaombea heri Domayo na Kiemba katika majukumu yao mapya na tunawakumbusha kuwa wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ya kumsaidia kocha mkuu ili Kagera Sugar itoke katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.
Wakifanya vizuri wataiheshimisha vilivyo tasnia ya habari za michezo kwa vile itaonekana ina watu smati na wanaoweza kufanyia kazi kwa vitendo kile ambacho wanakizungumza katika vipaza sauti na kamera.
Maana tunajua kuna watu wamekaa mkao wa kula kusubiria kuona Kiemba na Domayo watafanya kitu gani katika timu ya Kagera Sugar ili wapate cha kuongea.
Sasa dawa ni viungo hao wawili wa zamani, kupiga mzigo wa maana pale Kagera Sugar ili hata wakichambuliwa, basi uchambuzi uwe wenye kusifia mazuri wanayoyafanya ndani ya timu hiyo.
Maana lazima na wao watachambuliwa tu kama walivyokuwa wanachambua wenzao ila sasa huo uchambuzi tunatamani uwe wenye heri na sifa nzuri.