Kisa kupungua... Serena awashusha presha mashabiki
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 43 amefunguka kuhusu safari yake ya kupunguza uzito, akisema amepunguza kilo 14 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita
LONDON, ENGLAND: Mcheza tenisi mashuhuri duniani, Serena Williams, hatimaye amefichua siri ya mabadiliko yake makubwa ya mwili mwezi mmoja tu baada ya kuibua hofu miongoni mwa mashabiki wake kutokana na mwonekano wake mpya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 43 amefunguka kuhusu safari yake ya kupunguza uzito, akisema amepunguza kilo 14 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Staa huyo anaheshimika kutokana na kutwaa vikombe kadhaa vikubwa vya tenisi, huku akitwaa Grand Slam mara 23, Serena alikiri kuwa amekuwa akitumia dawa ya kupunguza uzito iitwayo Zepbound, na siyo kweli kuwa ana mawazo au ni mgonjwa kama ambavyo imekuwa ikielezwa kwenye mitandao.
Akihojiwa na jarida la Vogue, Williams alieleza kuwa dawa hiyo imemsaidia sana kudhibiti hamu ya kula na viwango vya sukari mwilini.
GLP-1 ni homoni ya asili ambayo husaidia katika kudhibiti kiwango cha sukari na hamu ya kula. Inapatikana katika dawa maarufu za kupunguza uzito duniani.
Maelezo haya yanakuja wiki chache baada ya Serena kuweka picha zake akiwa kwenye mazoezi, zikionesha misuli yake iliyochongwa vyema, hali iliyozua uvumi kuwa huenda alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa au ana msongo wa wa mawazo.
Serena pia alihojiwa na People Magazine na kipindi cha TODAY Show, akisisitiza kuwa dawa hiyo imemfanya ajisikie “mwepesi kimwili na kiakili”.
Serena alistaafu rasmi kutoka kwenye tenisi ya ushindani baada ya US Open 2022, na alieleza kuwa alianza kupambana na uzito wake baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza, Alexis Olympia, mwaka 2017. Hali hiyo ilijirudia tena baada ya kujifungua mtoto wake wa pili, Adira River, mwezi Agosti 2023.
Akiwa amezoea maisha ya mchezaji wa kiwango cha juu, Serena alisema aliendelea kushindwa kupunguza uzito licha ya kula vyema na kufanya mazoezi kwa bidii. “Sikuwahi kufikia uzito ninaoutaka, haijalishi nilijituma kiasi gani,” alisema.
“Mimi si mtu wa njia za mkato. Nimejifunza kuwa bingwa kwa bidii. Hivyo ilikuwa changamoto sana kufanya kila kitu kwa usahihi lakini nisione mabadiliko yoyote mwilini,” aliongeza.
Serena alisema dawa hiyo haikumchukua nafasi ya mazoezi au lishe bora, bali ilikuza kile alichokuwa tayari anakifanya. “Ninajisikia mwenye nguvu zaidi, viungo vyangu haviumi sana, na mwili wangu uko katika hali nzuri,” alisema.
Hata hivyo, Serena alikiri kuwa kuna unyanyapaa kuhusu matumizi ya dawa za kupunguza uzito. Alisisitiza kuwa kupunguza uzito hakupaswi kubadilisha mtazamo wa mtu kuhusu mwonekano wake. “Sikuwahi kuona hitaji la kuonekana kwa namna fulani. Lakini wakati huo, nilikuwa na maumivu kwenye viungo, kitu ambacho sikuzoea kabla ya kupata watoto,” alieleza.
Mwezi uliopita, mashabiki walizua hofu baada ya Serena kupakia picha akivaa bikini akiwa ufukweni, huku akionesha umbo lake jembamba lililowafanya baadhi ya watu kumtupia lawama kwa kupunguza mwili wake kupita kiasi huku wengine wakiamiani anasumbuliwa na magonjwa.
Wengine walimtetea vikali, wakisema bado anaonekana mwenye afya na kujiamini. Mmoja aliandika, “Serena anaishi maisha yake. Acheni mtu aishi vile anavyotaka.”
Serena, ambaye ni mke wa mwanzilishi wa Reddit, Alexis Ohanian, alihudhuria tuzo za 2024 ESPYs akiwa na mumewe, akionekana kung’ara kwa mtindo wake wa kipekee.
Mbali na mafanikio yake uwanjani, yakiwemo mataji 23 ya Grand Slam na kuongoza kwa wiki 319 kama mchezaji namba moja duniani, Serena sasa ni mama, mfanyabiashara, mfadhili, na mrembo wa mitindo ya hali ya juu.
Aliagwa rasmi kwenye uwanja wa tenisi US Open 2022, katika mechi ya kusisimua dhidi ya Ajla Tomljanovic.
Kwa sasa, Serena Williams anaendelea kuishi maisha yake kwa furaha, akiweka afya yake mbele na kuonyesha kuwa mabadiliko, hata kwa mashujaa wakubwa, ni sehemu ya maisha.