Kisa Krismasi, Arsenal hesabu hazitaki
Muktasari:
- Arsenal hadi kufikia Krismasi msimu huu iko kileleni mwa msimamo wa ligi tofauti ya pointi sita dhidi ya Manchester City na suala la kuchukua ubingwa ni kama limeachwa kwao kutokana na vita kali inayoendelea pale juu.
LONDON, ENGLAND: ITAKUAJE? Ndicho wanachojiuliza mashabiki wa Arsenal ambao kila wakifikiria rekodi za nyuma za timu hiyo katika mchaka mchaka wa Ligi Kuu England ifikapo Krismasi, hesabu za msimu huu hazisomi.
Arsenal hadi kufikia Krismasi msimu huu iko kileleni mwa msimamo wa ligi tofauti ya pointi sita dhidi ya Manchester City na suala la kuchukua ubingwa ni kama limeachwa kwao kutokana na vita kali inayoendelea pale juu.
Hata hivyo, kwa Arsenal, licha ya kufurahia kuwa kileleni kipindi hiki cha Krisimasi, rekodi zinaonyesha timu inayokuwa katika nafasi hiyo hadi Mwaka Mpya, ina nafasi kubwa ya kuwa bingwa mweisho wa msimu. Hapo ndipo mashabiki wanapopata wasiwasi wakizifikiria rekodi hizo kwani zinaenda tofauti na chama lao hilo la Emirates.
Katika rekodi zake ikiwa katika nafasi hiyo, msimu wa 2002-03 ilikuwa na tofauti ya pointi nane dhidi ya Manchester United na baadaye ikaangukia pua, ikarudia pia kufanya hivyo mwaka 2007-08, 2022-23 na 2023-24.
Rekodi pia zinaonyesha kabla hata ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Ligi Kuu England mwaka 1992, huko nyuma Arsenal haikuwahi kutoboa ilipokuwa kileleni hadi kufikia Desemba 25.
Kwa mujibu wa takwimu za Opta Analysis, Arsenal haijawahi kushinda ligi katika mara saba za mwisho ilipoongoza kwenye msimamo kufikia Desemba 25.
Mara ya mwisho washika mitutu hao kushinda taji la ligi baada ya kuwa kileleni wakati wa Krismasi ilikuwa ni msimu wa 1947-48.
Mbali ya rekodi mbaya za Arsenal katika mara zote ilizoongoza ligi hadi kufikia Desemba 25, kijumla pia takwimu zinaonyesha katika ligi hiyo ni timu chache sana zilishinda taji baada ya kuwa inaongoza ligi hadi kufikia siku hiyo.
Kati ya misimu 126, tangu 1888, timu zilizokaa kileleni Desemba 25 zilishinda taji mara 56 tu ambayo ni sawa na asilimia 44 tu.
Vilevile kwa takwimu za kuanzia mwaka 1992, timu 17 kati ya 33 zilizokuwa kileleni siku ya Krismasi ndizo zilizoshinda taji.
Historia inaonyesha kukaa kileleni katika kipindi hiki hakuwapi Arsenal uhakika itashinda taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 20.
Kocha wa washika mitutu hao, Mikel Arteta alipoulizwa juu ya uwezekano wa ubingwa msimu huu, alisema anapata matumaini juu ya kiwango ambacho timu yake inakionyesha, lakini yeye anachoangalia kwa sasa ni namna atakavyoweza kushinda mechi inayofuata badala ya kufikiria ubingwa.
Arsenal kwa sasa haijashinda taji lolote tangu mara ya mwisho iliposhinda FA Cup mwaka 2020.