Kisa kichapo, Salah atupa kijembe kwa Slot
Muktasari:
- Liverpool ilipokea kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Aston Villa Ijumaa usiku, matokeo yaliyoongeza presha kwa Slot ikiwa ni mwendelezo wa matokeo mabovu waliyoyapata msimu huu.
LIVERPOOL, ENGLAND: NYOTA wa Liverpool, Mohamed Salah ameonekana kumrushia kijembe kocha wa timu hiyo Arne Slot katika ujumbe mzito aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Liverpool ilipokea kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Aston Villa Ijumaa usiku, matokeo yaliyoongeza presha kwa Slot ikiwa ni mwendelezo wa matokeo mabovu waliyoyapata msimu huu.
Kwa sasa Liverpool ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na bado haijajihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, jambo linalozidisha presha zaidi kwa Slot.
Salah, ambaye alirejea kutoka kwenye majeraha na kuingia kama mchezaji wa akiba mwishoni mwa mechi dhidi ya Villa, anatarajiwa kuondoka klabuni hapo mwisho wa msimu huu ikiwa ni baada ya vipindi kadhaa vya uhusiano wake na Slot kupitia panda shuka nyingi.
Baada ya kipigo hicho, Salah alichapisha ujumbe uliotafsiriwa na wengi kama ukosoaji wa moja kwa moja kwa kocha huyo.
“Nimeshuhudia klabu hii ikitoka chini hadi kuwa mabingwa. Ilikuwa ni kazi ngumu na siku zote nilifanya kila nilichoweza kusaidia klabu kufika hapo, hakuna kinachonifanya nijivunie zaidi ya hilo. Kuona tukiporomoka tena kwa kipigo kingine msimu huu kuliumiza sana na si kitu ambacho mashabiki wetu wanastahili. Nataka kuona Liverpool ikirejea kuwa timu ya kushambulia kwa nguvu kubwa ambayo wapinzani wanaogopa na kurejea kuwa timu inayoshinda mataji," amesema Salah.
"Huo ndiyo mpira ninaoujua kucheza na huo ndiyo utambulisho unaotakiwa kurejeshwa na kubaki milele katika hii klabu. Hilo halipaswi kuwa jambo la kujadiliana na kila anayekuja ndani ya klabu hii lazima aendane nalo."
Kauli zake zilionekana kukumbushia aina ya soka ambalo ilikuwa ikichezwa zamani Liverpool chini ya Kocha Jurgen Klopp, ambaye aliinoa klabu hiyo kati ya mwaka 2015 hadi 2024.
Ujumbe wa Salah ulipata sapoti kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Liverpool, huku Curtis Jones akiweka emoji ya makofi.
Wachezaji wengine waliotoa maoni ni Dominik Szoboszlai, Andrew Robertson, Hugo Ekitike, Milos Kerkez, Jeremie Frimpong, Wataru Endo, Giovanni Leoni pamoja na Harvey Elliott.
Katika ujumbe mwingine tofauti, Curtis Jones aliandika:
“Asanteni kwa kuendelea kutuunga mkono katika msimu huu wa kukatisha tamaa. Tupo mbali sana na viwango vinavyotarajiwa ndani ya klabu hii.”
Ingawa baadhi ya watu waliona ujumbe wa Salah kama hamasa kwa timu, upande mwingine ulionekana kama sehemu ya kumshambulia Slot ambaye miezi mitatu iliyopita hawakuwa na mahusiano mazuri kabisa.
Baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Leeds United Desemba mwaka jana katika mechi ambayo Salah alisugua benchi mwanzo mwisho, mshambuliaji huyo raia wa Misri alifanya mahojiano na kutupa lawama za kutosha kwa benchi la ufundi.
"Sikuamini nilikaa benchi dakika 90 zote. Nafikiri ni mara ya kwanza katika maisha yangu,” amesema Salah.
“Nimevunjika moyo sana. Nimeifanyia mengi klabu hii kwa miaka mingi, hasa msimu uliopita. Inaonekana klabu imenitupa chini ya basi. Hivyo ndivyo ninavyohisi.
"Kuna mtu fulani anataka nibebe lawama zote. Klabu iliniahidi mambo mengi majira ya kiangazi. Sasa niko benchi hivyo naweza kusema hawakutimiza ahadi hizo. Nilikuwa na uhusiano mzuri na Slot. Sasa hatuna tena uhusiano wowote na sijui kwa nini. Inaonekana kuna mtu hataki nibaki katika hii klabu."
Salah, ambaye ameshinda mataji tisa katika miaka tisa akiwa Anfield, msimu huu hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita na alifunga mabao 29 na kutoa pasi 18 za mabao.
Nyota huyo atapata nafasi ya mwisho kucheza katika dimba la Anfield Jumapili ya wiki hii wakati Liverpool itakapowakaribisha Brentford.