Kisa Arsenal, Henry amvaa Mikel Arteta

Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa zamani wa Ufaransa amesema hayo baada ya timu yake ya zamani kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, safari hii wakipoteza taji kwa Liverpool, huku misimu miwili iliyopita ikiwa dhidi ya Manchester City.
LONDON, ENGLAND: LEJENDI wa Arsenal, Thienry Henry amekosoa Arsenal kwa kushindwa kwao kupata mataji akiwalinganisha na Manchester United ambayo kila tu anaicheka kutokana na kiwango chao.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Ufaransa amesema hayo baada ya timu yake ya zamani kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa msimu wa tatu mfululizo, safari hii wakipoteza taji kwa Liverpool, huku misimu miwili iliyopita ikiwa dhidi ya Manchester City.
Arsenal wamekuwa washindani wa mara kwa mara kwenye mbio za ubingwa chini ya Mikel Arteta, na pia wameanza kufika hatua za juu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, ukosefu wa – ya ndani au ya nje chini ya Arteta umepelekea baadhi ya watu kumkosoa kocha huyo wa kimataifa wa Hispania.
Msimu huu baada ya Tottenham kushinda Europa League ambalo lilikuwa ni taji lao la kwanza baada ya miaka 17 , sasa Arsenal wanashikilia rekodi ya kutoshinda taji kwa muda mrefu zaidi katika orodha ya timu sita kubwa.
Taji lao la mwisho au hata fainali ya mwisho lilikuwa msimu wa kwanza wa Arteta kama kocha aliposhinda FA Cup baada ya kumrithi Unai Emery katika msimu wa 2019/20.
Tangu hapo licha Manchester United kuwa wakisuasua kwenye ligi lakini wamefika fainali tano mbili za Europa League, mbili za FA Cup, na moja ya League Cup na wamefanikiwa kushinda mataji mawili.
Henry, anaamini ni sahihi watu kuuliza maswali kuhusu ukosefu wa mataji chini ya Arteta licha ya timu kutumia fedha nyingi katika usajili.
Akizungumza kwenye podcast ya Stick to Football iliyoandaliwa Henry alisema:”Ninaelewa kwamba mwanzoni kabisa alihitaji muda kwa sababu alikuta timu ambayo sio yake. Unahitaji walau madirisha matatu au manne ya usajili kubadilisha vitu.”
“Kawaida huwa inachukua muda na lazima umpatie kocha muda kutekeleza anachotaka.
Lakini kwa miaka mitatu iliyopita, Arsenal wamekuwa katika nafasi ambayo walipaswa angalau kupata taji moja au kufika fainali. Manchester United wamecheza fainali tano katika miaka mitano iliyopita, Man United ambayo watu huwacheka, lakini Arsenal katika miaka hii mitatu ya kujenga, hawajafika hata fainali.
Kwa hiyo, ninaelewa watu wanapouliza kuhusu hilo.”
“Sisemi kwamba nimevunjika moyo na Arsenal, lakini ni kawaida kwa watu kuuliza maswali kuhusu kile timu inafanya.”
Akizungumza na mashabiki katika Uwanja wa Emirates baada ya mechi yao ya mwisho ya nyumbani ya msimu iliyomalizika kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Newcastle, Arteta aliwahimiza mashabiki waendelee kuunga mkono timu ili kufanya ndoto ya kushinda taji kuwa halisi.