Kisa Amorim, Ratcliffe apata wasiwasi
Muktasari:
- Wasiwasi wa Ratclifee unakuja baada ya hivi karibuni Amorim aliyetua Old Trafford akitokea Sporting Lisbon ya Ureno kudai yuko tayari kuwajibika kujiuzulu ikiwa ataona mambo hayaendi.
MANCHESTER, ENGLAND: TAJIRI wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe amesema yuko tayari kumuunga mkono Kocha Roben Amorim katika kuijenga Manchester United, ila ana wasiwasi kama ataendelea kusalia klabuni hapo.
Wasiwasi wa Ratclifee unakuja baada ya hivi karibuni Amorim aliyetua Old Trafford akitokea Sporting Lisbon ya Ureno kudai yuko tayari kuwajibika kujiuzulu ikiwa ataona mambo hayaendi.
"Huu ni wakati wa maamuzi katika historia ya klabu. Tunahitaji kuwa imara sana dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kuwa na ujasiri kwa sababu hatutaki kufanya vibaya msimu ujao kama ilivyo msimu huu."
"Ikiwa tutaanza kama hivi, ikiwa hali hii itaendelea, basi ni bora sisi tuondoke na tuwapishe watu wengine."
Ratcliffe ambaye ni mmiliki mwenza wa Man United ana nia ya kutenga kiasi kikubwa cha pesa na kumsaidia Amorim dirisha lijalo la majira ya kiangazi kupata wachezaji anaohitaji, ingawa ujumbe huo unaonekana kumchanganya na ana hofu Mreno huyo anaweza kuondoka kwa kuona kazi ya kujenga upya timu hiyo ni ngumu mno kwake, ingawa anamwona ndiye mtu sahihi wa kuleta mageuzi.
Hata hivyo, kabla ya mechi ya usiku wa Ijumaa, Man United ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Chelsea mechi ya Ijumaa usiku walifungwa 1-0 na Chelsea, Amorim alisisitiza hataondoka.
Tovuti ya The Sun, inaeleza Ratcliffe bado ana wasiwasi kocha huyo wa zamani wa Sporting Lisbon anaweza kuamua kuachana na kazi hiyo baada ya kufanya vibaya msimu huu hata atakapochukua Kombe la Europa League.
Ratcliffe anataka kujua ikiwa kocha huyo atabaki au ana mpango mwingine na kuna wasiwasi hata kama Man United itabeba kombe la Europa League itakapocheza fainali dhidi ya Tottenham Jumatano hii, huko Hispania na kufuzu Ligi ya Mabingwa, bado huenda isiwe sababu ya kumzuia Amorim kuondoka.
Tangu kukamilisha ununuaji wa hisa za asilimia 27.7 kwa kutumia Pauni 1.3 bilioni miezi 15 iliyopita Ratcliffe amekuwa akisimamia sana upunguzaji mkubwa wa gharama ndani ya timu hiyo lakini bado ana matumaini na Amorim na yupo tayari kutoa fungu kubwa la usajili kwa dirisha lijalo.
Hadi sasa Man United inaonekana kulenga zaidi eneo la ushambuliaji na inadaiwa kutaka kumsajili mshambuliaji Matheus Cunha kutoka Wolves kwa ada ya Pauni 60 milioni pamoja na mshambuliaji wa Ipswich Liam Delap anayeuzwa Pauni 30 milioni.
Wakati huohuo, mastaa kama Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo wanaweza kuuzwa ili kukusanya pesa zitakazotumika kwa ajili ya usajili.