Kipa wa ligi ya England aula ufalme Uganda
Muktasari:
- George Desmond Kamurasi, mwenye umri wa miaka 36, ni nahodha wa Klabu ya SE Dons ya Kusini-mashariki mwa London, lakini hivi karibuni anaweza kuachana na glovu zake za ukipa na kuvaa taji baada ya kuchaguliwa kuwa Omukama, yaani mfalme wa watu wa Tooro, Uganda.
KAMPALA, UGANDA: KIPA Mganda anayechezea timu ya Daraja la Tisa England amechaguliwa kuwa mfalme ajaye wa ufalme wa jadi nchini Uganda, ingawa huenda akakataa nafasi hiyo iwapo atapenda.
George Desmond Kamurasi, mwenye umri wa miaka 36, ni nahodha wa Klabu ya SE Dons ya Kusini-mashariki mwa London, lakini hivi karibuni anaweza kuachana na glovu zake za ukipa na kuvaa taji baada ya kuchaguliwa kuwa Omukama, yaani mfalme wa watu wa Tooro, Uganda.
Kamurasi, anayefahamika kwa jina la Big G katika klabu hiyo iliyopo Bexleyheath, alichaguliwa baada ya kifo cha binamu yake, Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV, mwezi uliopita. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Uganda, wajumbe 15 kati ya 18 wa kamati ya urithi wa kifalme ya Tooro waliokuwepo walimpigia kura Kamurasi.
Kamurasi ni mjukuu wa Mfalme George Rukidi III, aliyewahi kuwa mfalme wa Tooro kuanzia 1928 hadi 1965. Hivyo ni sehemu ya ukoo wa kifalme wa eneo hilo.
Tangazo rasmi juu ya kuchaguliwa kwake linatarajiwa kufanyika baada ya mazishi ya Oyo yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.
Kamurasi bado hajatoa kauli hadharani kuhusu kuchaguliwa kwake, huku chombo kimoja cha habari cha Uganda kikiripoti kwa kunukuu vyanzo vilivyo karibu na mchakato wa urithi kwamba hataki kuachana na maisha yake ya London ili kwenda kushika nafasi hiyo.
Kipa huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 6 akiwa na mkewe na mtoto wao wa kiume amekuwa mtu maarufu katika Klabu ya SE Dons iliyoanzishwa 2014 na rapa wa Uingereza, Don Strapzy ambayo awali ilipata mashabiki wengi kupitia YouTube kabla ya kuingia katika mfumo wa soka la England.
Kamurasi mara kwa mara huonekana katika maudhui ya mitandao ya kijamii ya klabu hiyo na anafahamika kwa kutoa hotuba zenye hamasa kubwa, ambazo mara nyingi huwa na lugha kali kwa wachezaji wenzake kabla ya mechi. SE Dons inafurahia msimu wake wa kwanza kushiriki Kombe la FA na Jumamosi iliifunga Erith Town kwa mabao 2-0 na kutinga raundi ya pili ya mchujo.
Majukumu ya Kamurasi katika soka yanaweza hata kugongana na matukio yanayohusiana na urithi wa kifalme, hivyo huenda akaachana na mchezo huo.
Zaidi ya hayo, kuna mjadala nchini Uganda kuhusu kama mtu aliyekulia Uingereza iwapo anaweza kuwakilisha kikamilifu watu wa Tooro katika nafasi ya ufalme.
Wapo wanaomuona kama kiongozi mwenye nguvu, msimamo na uwezo wa kuhamasisha watu, lakini wengine wanaohoji juu ya malezi yake ya Uingereza iwapo yanaweza kumfanya asiwe mbali na utamaduni na maisha ya watu wa Tooro
KAGUSA GEREZANI
Kamurasi ni mchezaji wa soka aliyezaliwa na kukulia nchini Uingereza na akiwa mdogo aliwahi kufungwa gerezani kutokana na kujihusisha na kundi la kihalifu ya mtaani nchini humo.
Inaelezwa kwamba Big G alipitia kipindi kigumu ujanani baada ya mama yake kufariki dunia alipokuwa na umri wa miaka 14, ambapo maisha yake yalibadilika na akaingia katika kundi la uporaji ambalo hatimaye lilimfanya afungwe gerezani.
Lakini, akiwa gerezani ndipo alianza kutafakari upya namna ya kuishi maisha bora na kutambua kwamba mtaani kwao alikuwa akifanya mambo ya kipuuzi ya unyang'anyi, hivyo akaanza kujihusisha na soka na hatimaye likawa sehemu muhimu ya kumsaidia kubadilika na kuanza maisha mapya.
Bahati mbaya ni kwamba licha ya kucheza vyema kama kipa, hakubahatika kupata timu kubwa na hilo huenda lilitokana na kujikita katika mchezo huo tayari akiwa mtu mkubwa ambaye hakuwahi kupitia katika misingi ya soka.
Baada ya kugeukia soka maisha ya Kamurasi yaliendelea vizuri akichezea timu ndogondogo za mitaani. Kwa sasa ana miaka 36 na ni kipa pamoja na nahodha wa SE Dons, katika klabu ambayo amejijengea sifa ya kuwa kiongozi mwenye nguvu, anayependa kuhamasisha wachezaji wenzake na kutoa hotuba zenye msisimko kabla ya mechi.
Soka kwake halijawa tu kazi ya kucheza; pia lilimsaidia kuwa kocha na mlezi wa vijana akitumia uzoefu wake kuwasaidia wengine wasipitie makosa aliyowahi kuyafanya huko nyuma.
Akizungumzia uwezekano wa Kamurasi kuwa mfalme, mwandishi mmoja kutoka Uganda, Cynthia Nakoto aliandika kwenye X: “Kwa kuangalia video, mfalme mpya Desmond Kamurasi anaonekana kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuhamasisha watu, asiye na mzaha na mwenye msimamo mkali. Kwa watu wa Tooro, hilo ni jambo zuri. Ni wakati muafaka kuwa na mfalme wa aina hiyo.”
Mazishi ya Oyo aliyeingia kwenye kiti cha enzi 1995 akiwa na umri wa miaka mitatu yanatarajiwa kufanyika Uganda mwishoni mwa wiki hii, wakati huohuo SE Dons ikiwa imepangwa kucheza dhidi ya Greenways katika raundi ya pili ya mchujo ya FA Vase.
Uganda inaongozwa na rais na bunge waliochaguliwa, lakini falme kadhaa za jadi bado zina ushawishi mkubwa wa kitamaduni licha ya kutokuwa na mamlaka ya kisiasa.