Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipa aanguka na kufa akiokoa penalti

KIFO Pict

Muktasari:

  • Antonio mwenye umri wa miaka 34 alifariki dunia jana wakati wa mazoezi ya soka la sakafuni maarufu kama Futsal nchini Brazil, baada ya kuanguka ghafla muda mfupi alipookoa penalti kwa kifua.

BRASILIA, BRAZIL: Kipa Antonio Edson dos Santos Sousa wa timu ya Sind Motos ameanguka na kufa muda mfupi baada ya kuokoa penalti katika tukio ambalo limewaacha mashabiki vinywa wazi. 

Antonio mwenye umri wa miaka 34 alifariki dunia jana wakati wa mazoezi ya soka la sakafuni maarufu kama Futsal nchini Brazil, baada ya kuanguka ghafla muda mfupi alipookoa penalti kwa kifua.

Tukio hilo lilinaswa moja kwa moja kupitia matangazo ya mtandaoni, ambapo Antonio alionekana akianguka alipokuwa akikimbia kufurahi na mwenzake namna alivyookoa penalti hiyo.

Licha ya msaada wa haraka wa kitabibu uliofanyika, lakini alithibitishwa kufariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali, kufuatia jitihada zilizoshindikana za kumrejeshea uhai.

Tukio hilo la kushtua lilitokea kwenye uwanja uliopo ndani ya ukumbi wa mazoezi katika Manispaa ya Augusto Correa, Jimbo la Kaskazini la Para nchini Brazil. 

Antonio anayejulikana kwa jina la utani la Pixe alikuwa akiichezea Sind Motos kwenye mashindano ya wachezaji wa ridhaa yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 200 ya uhuru wa Brazil kutoka Ureno.

Video ya tukio hilo ilionyesha Antonio akiokoa penalti kwa kifua na mwanzoni alionekana kuwa fiti kiasi cha  kuinua mikono juu kushukuru kabla ya kuelekea kusherehekea na mwenzake. 

Hata hivyo, alipomfikia mchezaji mwenzake aliyekuwa akimkimbilia ghafla alionekana akitetemeka na kuanguka. Bado haijulikani iwapo athari ya mpira alioupokea kifuani ndiyo uliochangia kifo chake. 

Mwezi Juni, mwaka huu, tukio la aina hiyo lilitokea nchini Brazil ambapo mchezaji wa Futsal, Roberto Peterson mwenye umri wa miaka 33 alifariki dunia baada ya kugongwa na mpira tumboni wakati wa mechi huko Santa Catarina, Kusini mwa nchi hiyo. 

Peterson, baba wa watoto watatu alipatwa na mshtuko wa moyo muda mfupi baada ya tukio hilo.

Futsal ni mchezo wa ndani wenye wachezaji watano kila upande unaochezwa kwenye uwanja mdogo zaidi kuliko ule wa soka la kawaida. Mchezo huo ni maarufu zaidi Amerika Kusini, Hispania na Ureno ambako kuna timu nyingi za wachezaji wa kulipwa.

Kutokana na msiba huo, viongozi wa eneo hilo walisitisha michezo iliyokuwa ipigwe siku inayofuata, ambapo Shirikisho la Futsal la Para lilitoa taarifa pamoja na picha iliyoambatana na utepe mweusi kumuenzi mchezaji huyo na kueleza:

"Ni kwa huzuni kubwa tumepokea taarifa za kifo cha Antonio Edson dos Santos Sousa, mchezaji ambaye aliandika historia yake kwa kujitolea, kipaji chenye moyo wa mshikamano. Uwepo wake utakumbukwa daima ndani na nje ya uwanja, si tu kwa uchezaji wake wa kipekee, bali pia kwa utu uliogusa kila mmoja. 

"Katika kipindi hiki cha majonzi tunawapa pole za dhati familia yake, marafiki na jumuiya nzima ya michezo wapate faraja kupitia kumbukumbu nzuri na hakika kwamba Antonio Edson ameacha urithi wa msukumo na mapenzi makubwa kwa Futsal."

Brazil ni mabingwa wa Kombe la Dunia mara sita wa Futsal na pia ndio mabingwa watetezi baada ya kuwashinda mahasimu wao Argentina katika fainali zilizopigwa nchini Uzbekistan 2024.